Serikali imeendelea kupigwa mweleka katika kesi ya uchochezi dhidi ya mshitakiwa Tundu Lissu baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutupa pingamizi la Wakili wa Serikali wakitaka wakili Peter Kibatala kujitoa kumtetea mwanasiasa huyo.
Lissu, ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya Chadema alipandishwa kizimbani Agosti 5, na kusomewa mashtaka matatu, mawili kati yake yakiwa ni ya uchochezi na moja la kuidharau mahakama.
Pigo la kwanza la upande wa mashtaka ni pale Lissu alipopangua hoja na kufanikiwa kupata dhamana, wakati kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza.
Jana ilikuwa ushindi mwingine kwa upande wa utetezi, baada ya Mahakama kutupa pingamizi la upande wa mashtaka lililotaka Kibatala ajitoe katika jopo la mawakili wanaomtetea Lissu.
Upande wa mashtaka ulioongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, uliweka pingamizi hilo kwa maelezo Kibatala ni shahidi wao kwa kuwa alikuwapo siku na mahali wakati Lissu akitoa maneno yanayodaiwa ya uchochezi.
Wakili Kibatala ambaye ni kiongozi wa jopo la mawakili wanaomtetea Lissu, alipinga hoja za Serikali za kutaka ajitoe katika kesi hiyo, mvutano ambao ulisababisha kesi hiyo kuahirishwa mara mbili.
Wakili Kibatala alipinga kuwa hakuna kifungu cha sheria kinachomzuia wakili kumtetea mteja wake kwa sababu tu ya kushuhudia akitoa maelezo yake Polisi.
Akitoa uamuzi wa pingamizi hilo la Serikali, Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha anayesikiliza kesi hiyo, hakukubaliana na hoja za upande wa Jamhuri (mashtaka) na hivyo akalitupa pingamizi hilo.
Hakimu Mkeha alikubaliana na hoja za wakili Kibatala kuwa hakuna kifungu chochote cha sheria kinachomzuia kumtetea Lissu.
Alisisitiza kuwa Kibatala ataendelea kuwa wakili wa Lissu katika kesi hiyo na kwamba kama upande wa mashtaka ukimhitaji awe shahidi wao utalazimika kumuomba. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Septemba 19.