Tundu Lissu, ambaye ni wakili wa Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya jana alitumia muda wa saa mbili kupangua maombi ya wananchi wanne wanaopinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu yaliyompa ushindi mteja wake.
Kesi hiyo imeanza kusikilizwa tena baada ya Mahakama ya Rufaa kufuta uamuzi wa Mahakama Kuu uliotupilia mbali hoja za kupinga matokeo hayo, ambazo ziliwasilishwa na wafuasi wanne wa aliyekuwa mgombea wa jimbo hilo, Steven Wasira (CCM).
Jaji Mohamed Gwae wa Mahakama Kuu, alitupilia mbali kesi hiyo baada ya kukubali pingamizi la Lissu kuwa wafuasi hao hawakuwa na haki ya kisheria kufungua kesi hiyo.
Wakazi hao wa Bunda wanadai kuwa uchaguzi haukuwa huru na haki kutokana na kugubikwa na vitendo vya rushwa, mgombea wanayemuunga mkono kunyimwa fursa ya kuhakiki matokeo na pia kuongezeka kwa idadi ya vituo vya kupigia kura.
Jana, Lissu, ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema na wakili wa kujitegemea, alitoa majibu ya utetezi mbele ya Jaji Lameck Mlacha kuanzia saa 4.10 asubuhi na kukamilisha saa 6.02 mchana wakati shauri hilo lilipoahirishwa kwa muda hadi saa 8:00 mchana kutoa fursa kwa mawakili wa upande wa wadai, Constantine Mutalemwa kujibu.
Lissu alidai kuwa waleta maombi wameshindwa kutoa hoja mahususi kuonyesha ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi wanazodai ulikuwepo katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana.
Wakili Lissu pia alidai kuwa walalamikaji ambao ni Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Ascetic Malegele, pia wameshindwa kuonyesha madhara waliyopata kama wapigakura kuishawishi mahakama kutengua matokeo yaliyompa ushindi Bulaya dhidi ya mwanasiasa huyo mkongwe.
“Waleta maombi wanadai uchaguzi haukuwa huru na haki, idadi ya wapigakura kutofautiana kwa kila kituo na uwepo wa vitendo vya rushwa, lakini hawabainishi wazi nani mhusika wa mambo wanayoyalalamikia na madhara waliyopata kwa nafasi yao ya wapigakura,” alisema wakili Lissu.
Alisema vitendo vya rushwa katika uchaguzi ni kosa kubwa linaloweza kusababisha kubatilishwa kwa matokeo ya uchaguzi mzima, lakini walalamikaji wana wajibu wa kumtaja mhusika wa vitendo hivyo ili kuipa mahakama fursa ya kutafsiri vyema sheria na kutoa haki.
“Lakini madai ya juujuu tena ya jumla kuwa aliyetoa rushwa ni wakala wa mteja wangu, hayakubaliki mbele ya macho ya sheria kwa sababu mtu huyo hajulikani na jukumu la kuthibitisha madai ni la mleta maombi na uthibitisho huo haumo kwenye hati yao ya maombi,” alidai Lissu.
Aliomba maombi hayo yafutwe kwa hoja kwamba wadai hawajataja vifungu vinavyoipa mahakama haki na mamlaka ya kuyasikiliza na kuyaamua.