Kufuatia vyombo vya habari mbalimbali nchini kutoa habari ambayo inamhusu Mkurugenzi wa Makampuni ya IPP, Dk. Reginald Mengi kuwa anatakiwa kufika mahakamani Agosti, 24 mwaka huu kujieleza kwanini asifungwe kwa kushindwa kutekeleza hukumu ya kulipa Dola 598,750 (Bil. 1.20), wakili wa Dk. Mengi, Deogratias Ringia amekanusha habari hiyo.
Katika taarifa ambayo imetolewa na wakili Ringia, amesema kuwa akiulizwa na watu mbalimbali kama ni kweli kuna hati imetolewa na Mahakama Kuu ikimtaka mteja wake Dk. Mengi kufika mahakamani kujieleza kwanini asifungwe baada ya vyombo mbalimbali kuripoti kuwa anatakiwa kufika mahakamani lakini jambo hilo halina ukweli.
“Mhusika mkuu katika kesi hiyo ni kampuni nayoitwa KM Prospecting Limited ambayo Dk. Mengi siyo mwanahisa wala mkurugenzi katika kampuni hiyo. Kampuni hiyo ndiyo iliingia kwenye mkataba na wadai iliyopelekea kesi hiyo ya madai,” alisema Ringia.
Ringia alisema hatua ya kumuunganisha Dk. Mengi katika kesi hiyo lilikuja baada ya mahakama kuamua hoja mbili zinazohusu kesi hiyo ndipo wadai ambao ni wafanyabiashara Muganyizi Lutagwaba, Eric Mshauri na Charles Mgweo kumuingiza Dk. Mengi katika kesi licha ya kuwa hausiki.
Baadhi ya vyombo vya habari vilivyoandika habari hiyo ni pamoja na gazeti la Jambo Leo, Daily News, The Citizen na mtandao wa Habari Leo Online.
Social Plugin