Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANAFUNZI WALIOKOSA SIFA YA KURUDISHWA UDOM NA VYUO VINGINE WAPANGIWA VYUO VINGINE



 WIZARA ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imewapangia vyuo vya serikali wanafunzi 1,450 ambao walikosa sifa ya kurudishwa katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) pamoja na vyuo vingine baada ya serikali kuwachuja na kuwarejesha wale waliokuwa wanastahili katika awamu ya kwanza.


Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Leornard Akwilapo alisema jana alipokuwa akitoa taarifa za ziada kuhusu wanafunzi waliokuwa wanasoma Stashahada Maalumu ya Ualimu wa Sayansi chuoni Udom.

Dk Akwilapo alisema kati ya wanafunzi hao 1,450, 290 walikuwa wanasomea programu ya Stashahada ya Ualimu wa Sekondari na 1,181 walikuwa wakisoma programu ya Stashahada ya Ualimu wa Msingi.

“Wanafunzi waliokuwa wanachukua Stashahada ya Ualimu wa Sekondari na kukosa sifa ni 290. Kati yao hawa, wanafunzi 269 walikuwa na daraja la kwanza hadi la tatu, hawa tumewapangia kuanza masomo ya ualimu wa shule za msingi. Hawa watakuwa katika Chuo cha Mtwara kawaida. Katika kundi hili wanafunzi 21 hatujawapangia kwa sababu wana daraja la 1V,” alisema Dk Akwilapo.

Alisema wanafunzi hao 1,181 waliokuwa wanachukua Stashahada ya Ualimu wa Msingi waliagizwa waombe mafunzo watakayoona yanawafaa kulingana na ufaulu wao kupitia Baraza la Taifa la Mafunzo ya Ufundi.

“Kwa kweli baada ya taarifa hii tulipokea maombi mengi sana kutoka kwa vijana hawa wakiomba kupangiwa moja kwa moja na wizara. Hapa wizara imetafakari kwa kina baada ya kupokea maombi mengi sana kutoka kwao. Na kwa kweli walionesha nia ya dhati ya kusomea ualimu. Kwa hiyo tumeamua nao kuwapangia katika vyuo vyetu vya Serikali. Hawa watakwenda katika vyuo vya ualimu vya Marangu na Tabora,” alisema Naibu Katibu Mkuu huyo.

Alisema fomu zenye maelezo ya kujiunga na vyuo vya ualimu vya serikali zinapatikana katika tovuti ya wizara vile vile katika tovuti za vyuo husika.

Alisema vyuo hivyo vinatarajiwa kufunguliwa Oktoba 15, mwaka huu.

Aliongeza kuwa wanafunzi hao wote watatakiwa kujigharimia wenyewe kwenye vyuo hivyo. Mei 28, mwaka huu, serikali iliwarejesha nyumbani wanafunzi 7,805 waliokuwa wanasoma Stashahada Maalumu ya Ualimu wa Sayansi na Hisabati Udom.

Aidha, Julai 19, mwaka huu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alitoa uamuzi kuhusu wanafunzi hao wakiwamo baadhi yao kukosa sifa za kurudi chuoni hapo. Kwa hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu alisema mitihani ya darasa la nne na kidato cha pili itaendelea kuwepo na mwaka huu itafanyika kama kawaida.

“Kama kuna watu wanawaambia kuwa haitafanyika wawapuuze kabisa. Narudia kusema kuwa mitihani hii ina umuhimu mkubwa katika kupima maendeleo ya mwanafunzi kwa lengo la kufanya marekebisho kitaaluma,” alisisitiza kuwa wanafunzi ambao watakuwa hawajafikia viwango vya ufaulu vilivyowekwa watatakiwa kukariri darasa au kidato mara moja.
 
Imeandikwa na Lucy Ngowi –Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com