Watu wawili wamekutwa wamefariki katika nyumba ya wageni
ya Kings Rest House iliyopo Mtaa wa Bumila, Gongo la Mboto jijini Dar
huku miili yao ikiwa imeungua moto.
Mmiliki wa gesti hiyo, Damian
Mng’ong’o alisema alifuatwa kanisani jana saa 1.30 asubuhi na kuambiwa
kuna chumba kimoja katika gesti yake kinafuka moshi na aliondoka
kanisani kuelekea ilipo nyumba hiyo.
Alisema alipofika aliona moshi bado
unafuka huku nje kukiwa na umati mkubwa wa watu wakishangaa.
“Tulifanya
uamuzi wa kufungua mlango lakini hatukuona mtu yeyote chumbani, ndipo
mmoja wa wafanyakazi alipofungua mlango wa choo ndani ya chumba tukakuta
maiti mbili zikiwa zimechomwa. "
Alisema mhudumu wa gesti alitueleza
kuwa jana (juzi) saa tano asubuhi alikuja mwanamume mmoja akachukua
chumba na baadaye jioni alikuja kijana mwingine wakawa wameingia wote
katika chumba hicho.
“Baada ya muda nilipiga simu polisi kuripoti tukio
hilo nao waliwasili ndani ya muda mfupi wakafanya uchunguzi wao na
kuhoji baadhi ya watu, baadaye wakawaleta madaktari kupima, kisha
wakaondoka na maiti hizo mbili kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa
ajili ya hatua nyingine.”
Mfanyakazi wa jikoni katika gesti hiyo ambaye
hakupenda jina lake litajwe alisema watu hao waliofariki ni
wafanyabiashara wanaouza ng’ombe katika mnada wa Pugu na mara nyingi
wakija Dar es Salaam hufikia hapo.
“Wengi wanaofanya biashara ya ng’ombe
wakija hufikia hapa, mpaka sasa sijajua kilichotokea kwa hawa
waliokufa, lakini tukio hili limewashtua wenzao kwani baadhi walipoona
tukio hili wameingiwa na hofu na kuondoka,” alisema.
Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni alisema wanaendelea kuchunguza na taarifa
za awali hazijathibitisha kama waliuawa hapo gesti au sehemu nyingine na
kupelekwa hapo.
“Kuna viashiria kuwa huenda waliuawa wakaletwa pale
kwani wana alama ya kamba katika shingo kama vile kuna mtu aliwanyonga
na katika matumbo yao kuna majeraha kama wamechomwa kitu chenye ncha
kali,” alisema na kuongeza:
“Mpaka sasa uchunguzi unaendelea na Jeshi la
Polisi linafanya kazi yake na tunasubiri taarifa kutoka kwa wataalamu
wa masuala ya uchunguzi na alama za vidole ambayo itaeleza kwa nini wao
waungue lakini nguo zao zisiungue. Pia kitanda na vitu vingine visiungue
na kwa nini watu waende kuzima moto, wakati watu wameshafariki,”
alisema Hamduni.
Hamduni alisema mmoja wa waliofariki alijiandikisha
kama Lameck Ludovick, mfanyabiashara na mkazi wa Dar es Salaam.