Aidha, mbali ya serikali kuokoa Sh bilioni 16.15 kwa mwezi huu wa Agosti baada ya watumishi hewa hao kuondolewa kwenye mfumo wa utumishi, ambao kama wasingeondolewa fedha hizo zilikuwa ziwalipe mshahara, posho na malipo mengine, waajiri 145 hawajawasilisha taarifa kuhusu uhakiki wao.
Hayo
yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki alipozungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu utekelezaji wa agizo la Rais
Magufuli la kuwataka waajiri wote wa umma na serikali, kuwaondoa
watumishi hewa.
Akifafanua
taarifa hiyo, Kairuki alisema Agosti 26, mwaka huu watamkabidhi rais
taarifa rasmi ya utekelezaji wa agizo hilo huku akiwataka waajiri 145
ambao hawajawasilisha taarifa za ama uwepo wa watumishi hewa au la,
kuhakikisha wanaziwasilisha taarifa hizo kabla ya Ijumaa wiki ijayo.
“Tunawapa
muda hadi Ijumaa wiki ijayo wawe wamewasilisha taarifa za kama wana
watumishi hewa au la na sisi Agosti 26, mwaka huu ndio tunamkabidhi rais
taarifa rasmi ya mwisho ya utekelezaji wa agizo alilotoa,” alisema Kairuki akizungumzia hatua ya Rais Magufuli kuagiza uhakiki huo Machi mwaka huu.
Akielezea
hatua zilizochukuliwa hadi sasa na waajiri hao, Kairuki alisema nchi
ina jumla ya waajiri 409 wa serikali na taasisi mbalimbali za umma, na
kati ya waajiri hao, hadi sasa waajiri 264 ndio waliowasilisha taarifa
za utekelezaji wa agizo hilo.
Alisema
kati ya waajiri hao 264 waliowasilisha, waajiri 63 wamethibitisha
hawana watumishi hewa, huku waajiri 201 wakibaini uwepo wa watumishi
hewa kuanzia mmoja na kuendelea.
“Tumepokea
taarifa za utekelezaji wa agizo la rais alilitoa Machi 15, mwaka huu na
hadi sasa waajiri 264 kati waliotekeleza agizo hilo, 201 wamebaini wana
watumishi hewa,” alisema Kairuki.
Akizungumzia
hatua zitakazochukuliwa baada ya kufikia tarehe ya mwisho wa kupeleka
taarifa hizo, Kairuki alisema jukumu lao ni kuzipokea na kukabidhi
mamlaka ya uteuzi ambayo ndiyo iliagiza na ambayo ndiyo itaamua hatua za
kuchukua.
Sambamba
na hilo, Kairuki alisema hadi sasa jumla ya watumishi hewa 606,
wameanza kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo mashauri yao kupelekwa
polisi na hivi sasa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru),
wanafanya uchunguzi na hatimaye watuhumiwa hao wafikishwe kwenye vyombo
vya juu vya sheria.
Aidha,
maofisa utumishi 233 waliohusika kwenye malipo ya mishahara hewa
mashauri yao, wamefikishwa kwenye mamlaka husika kwa uchunguzi, ilhali
watatu wamefukuzwa kazi, huku wizara ikiendelea kufanya uchunguzi kwenye
taasisi 75 za umma ili kujiridhisha kuhusu suala la watumishi hewa.
Kuhusu
waajiri 145 ambao hawajawasilisha taarifa za uhakiki wa watumishi wao,
Kairuki alisema zimo taasisi, wakala, bodi, mabaraza, vyuo, hospitali,
ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa, tume na mamlaka kadhaa ambazo
hazijawasilisha taarifa zao.
Kwa
upande wa mabaraza nchini, Kairuki alisema mabaraza mbalimbali 10
hayajawasilisha taarifa za uhakiki wa watumishi na baadhi yao ni kama
vile Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC), Baraza la Elimu ya Ufundi
(Nacte), Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Baraza la Mitihani la Taifa
(NECTA) na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Aidha,
jumla ya vyuo vya umma 25 nchini havijawasilisha taarifa zao za uhakiki
wa watumishi hewa na baadhi yao ni Dodoma (Udom), Chuo KIkuu Huria
(OUT), Chuo Kikuu Mzumbe, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi
Muhimbili (MUHAS), Chuo cha Diplomasia, Chuo Kikuu cha Elimu Dar es
Salaam (Duce), Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na Chuo cha Kumbukumbu
ya Mwalimu Nyerere na Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
Upande
wa Bodi mbalimbali ambazo hazijawasilisha taarifa zao jumla yake ni 10
na baadhi ya bodi hizo ni pamoja na Bodi ya Korosho Tanzania, Bodi ya
Tumbaku, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Bodi ya
Utalii na Bodi ya Maziwa.
Pia
zimo hospitali teule za rufaa tatu ambazo ni Hospitali ya CCBRT,
Hospitali ya Rufaa Bugando na Hospitali ya Rufaa KCMC na kwamba katika
hospitali kama hizo zilizowasilisha taarifa zake, wamebainika na
kuondolewa watumishi hewa 4,000.
Kwenye
taasisi za Umma na Wakala ambazo hazijawasilisha taarifa zao jumla ziko
30 na baadhi yao ni Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mfuko wa
Pembejeo za Kilimo, Makumbusho ya Taifa, Shirika la Utangazaji la Taifa
(TBC), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Shirika la Madini la Taifa
(Stamico), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Wakala wa Vitambulisho vya
Taifa (NIDA) na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC).
Pia
zipo Ofisi za Makatibu Tawala wa Mikoa 12 ambazo baadhi yake ni Ofisi
ya Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Dodoma, Dar es Salam, Mbeya, Pwani na
Kagera; kwa upande wa mamlaka zipo sita ambazo ni Mamlaka ya Elimu
Tanzania (TEA), Mamlaka ya Maeneo Maalumu ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje
(EPZA), Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na
Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA).
Aidha,
zipo tume 10 ambazo hazijawasilisha taarifa zake na baadhi yake ni Tume
ya Pamoja ya Fedha, Tume ya Atomiki, Tume ya Elimu Taifa, Tume ya
Kudhibiti Dawa za Kulevya, Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania na
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Pia
zipo Mamlaka za Serikali za Mitaa 38 zikiwemo Halmashauri ya Jiji la
Mwanza, Manispaa ya Iringa, Nyamagana, Halmashauri ya Mji, Kasulu,
Halmashauri ya Wilaya ya Dodoma na Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi.