MKOA wa Dodoma wakishirikiana na Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu (CDA) wametekeleza agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa la kuandaa na kuwasilisha mapendekezo ya awali ya namna serikali itakavyohamia Dodoma.
Aidha, imeelezwa kuwa kuanzia sasa Waziri Mkuu ataweka hadharani maelekezo ya wizara na watumishi kuhamia Dodoma.
Hayo yamebainishwa katika mahojiano yaliyofanyika jana na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Rehema Madenge.
Mwishoni mwa mwezi uliopita, Waziri Mkuu wakati akizungumza na viongozi wa serikali, taasisi, watendaji na wananchi wa Mkoa wa Dodoma alielezea azma ya serikali kuhamia Dodoma na kutoa siku 14 kwa Mkoa na CDA, kuwasilisha mapendekezo ya awali kwa namna serikali itakavyohamia Dodoma.
Akitoa siku hizo kwa Serikali ya Mkoa wa Dodoma kukaa na taasisi zake, hususani CDA kuandaa na kutoa mpango kazi wake, Majaliwa alisema, “Ndani ya siku 14 nipate proposal (mapendekezo) ya kwanza namna mtakavyotekeleza, naagiza kiundwe kikosi kazi chini yenu kitakachowajumuisha makundi yote. Baada ya siku 14 nipate mpango wenu.”
Madenge alisema kwamba Mkuu wa Mkoa huo, Jordan Rugimbana yuko Dar es Salaam alitarajiwa kuwasilisha mpango kazi huo kwa Waziri Mkuu na kwamba muda wowote Waziri Mkuu atatangaza utaratibu wa kuhamia Dodoma.
“Tumeandaa mpango kazi kulingana na maelekezo ya waziri mkuu na mkuu wa mkoa amekwenda kukabidhi mpango huo,” alisema Katibu Tawala Dodoma.
Akizungumzia taarifa za baadhi ya wizara kuanza kuhamia huko, Katibu tawala huyo alisema kwamba kama mkoa hawana taarifa za wizara na watumishi kuanza kuhamia Dodoma.
“Tunasubiri maelekezo ya waziri mkuu, baada ya mpango kazi kukamilika utawekwa hadharani mambo yote ya serikali kuhamia Dodoma,” alisema Madenge.
Akifafanua zaidi, alisema anachojua yeye mpango unakabidhiwa Ofisi ya Waziri Mkuu na na wizara zitajipanga kwa mujibu wa maelekezo ya Waziri Mkuu Majaliwa.
Mkoa wa Dodoma umekuwa katika hekaheka za kutekeleza maagizo ya serikali ya kuhamia Dodoma, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba huduma muhimu kama upatikanaji wa viwanja zinakwenda kwa taratibu zinazotakiwa.
Ili kuondoa mhemko na udalali wa viwanja unaoweza kupandisha bei na pia kuzuia vurugu, mkuu wa mkoa amepiga marufuku uuzaji wa viwanja ndani ya mji wa Dodoma. Sababu kubwa ya kupiga marufuku kunatokana na kundi la madalali kutoka mikoa mbalimbali kuvamia mji.
Kupokewa kwa mpango kazi huo ni moja ya hatua za kukamilisha uhamiaji wa serikali Dodoma, ambapo hatua nyingine ni kwa serikali kuwasilisha bungeni muswada wa kuitambua Dodoma kama makao makuu ya nchi ili uthibitishwe kisheria.
Muswada huo utawasilishwa katika Bunge linaloanza Septemba 6, mwaka huu.
Waziri Mkuu Majaliwa alisema muswada huo wa sheria ya serikali kuhamia Dodoma, utapelekwa bungeni ili azma ya Rais John Magufuli na serikali yake uwe na nguvu kisheria, baada ya Rais Magufuli kutangaza hivi karibuni kuwa ndani ya miaka minne na ushee iliyobaki ya kumaliza muhula wake wa kwanza wa urais, Serikali ya Awamu ya Tano itakuwa imehamia katika mji wa Dodoma, ambao mwaka 1973 ulitangazwa kuwa Makao Makuu ya Tanzania.