1. Utangulizi
Jana
Jumatatu, 5 Septemba 2016, Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo
ilikutana katika kikao chake cha kawaida. Pamoja na mambo mengine,
Kamati Kuu ilipokea, kujadili na kuidhinisha Taarifa kuhusu HALI YA
NCHI. Taarifa hii sasa inatolewa rasmi kwa umma. Taarifa ipo katika
maeneo makubwa manne: Hali ya kisiasa, hali ya kiuchumi, umoja wa
kitaifa na hitimisho.
2. Hali ya Kisiasa
Kamati
Kuu imezingatia kuwa Kikatiba, nchi yetu inafuata mfumo wa demokrasia
ya vyama vingi. Katiba na Sheria mbalimbali zimeanisha utaratibu wa kazi
na shughuli za vyama vya siasa. Ili kuhakikisha kwamba kazi na shughuli
za vyama vya siasa zinakuwa endelevu, vyama vyenye kukidhi vigezo
hupewa ruzuku kupitia Bajeti ya Serikali inayopitishwa na Bunge la
Jamhuri ya Muungano Tanzania.
Hata
hivyo, katika awamu hii ya tano, Serikali ya Chama cha Mapinduzi
imeamua kuzuia shughuli za siasa kwa kutumia nguvu ya Jeshi la Polisi na
hata Jeshi la Wananchi. Kwa mujibu wa serikali ya CCM, shughuli za
kiuenezi za vyama vya siasa kama vile mikutano ya hadhara, maandamano,
makongamano, mijadala na hata mikutano ya ndani inapaswa kukoma mapema
baada ya uchaguzi.
Kisheria,
huu ni uvunjifu wa Katiba na Sheria za nchi. Kisiasa, tunatambua kwamba
Viongozi wa CCM wamepoteza mvuto kwa wananchi na sasa wanamsukuma
Mwenyekiti wao Rais Magufuli kutumia jeshi katika kuokoa taswira ya
Chama cha Mapinduzi mbele ya umma.
Kwa kuzingatia hali ya kisiasa nchini kwa sasa, Kamati Kuu ya chama chetu:
i)
Tunalaani na kupinga kwa nguvu zetu zote hatua za Serikali ya Chama cha
Mapinduzi za kuvunja Katiba na kujaribu kuweka pembeni utawala wa
sheria.
ii)
Tunapinga vitendo vinavyozidi kushamiri katika serikali hii ya CCM ya
kujaribu kuendesha nchi kwa ubabe na matamko ya viongozi badala ya
utawala wa sharia.
iii)
Tutasimama imara, na tutaungana na vyama vingine vya siasa pamoja na
taasisi zingine za kiraia katika kulinda mfumo wa demokrasia ya vyama
vingi, uhuru wa maoni, na utawala wa sheria katika nchi yetu
3. Hali ya Kiuchumi
Katika
miaka 10-15 iliyopita, nchi yetu imejenga uchumi ambao umekuwa ukikua
kwa kiwango cha asilimia 6-7 kwa mwaka katika kipindi chote hiki. Ukuaji
huu wa uchumi ulitokana na juhudi za nchi katika kuvutia wawekezaji na
kuchochea shughuli za uzalishaji mali kwa wananchi wenye kipata cha
chini. Awamu ya tano ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi imerithi
changamoto ya uchumi unaokua bila kuwafaidisha wananchi wa kawaida. Hili
ndilo tulitegemea Serikali mpya ishughulike nalo.
Kamati
Kuu imeshtushwa na hali ya kuanza kudorora kwa shughuli za uchumi
katika kipindi cha miezi kumi ya utawala wa awamu ya tano. Kwa mfano:
a)
Taarifa za Benki Kuu zilizopo kwenye tovuti yake (Quarterly Economic
Review na Monthly Economic Review) kwa robo ya mwisho ya mwaka 2015
(Oktoba - Desemba 2015 ) zinaonesha kuwa kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa
ilikuwa 9%. Katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 (Januari - Machi 2016)
kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa ilishuka hadi kufikia 5.5%. Kiuchumi,
hii inamaanisha kuwa ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika kipindi cha
miezi 6 ya mwanzo ya utawala wa awamu ya tano chini ya Rais Magufuli
umepungua kwa 4%.
b)
Shughuli za uchumi zinazohusu wananchi masikini zimeshuka kutoka kasi
ya ukuaji ya 10.20% robo ya mwisho ya mwaka 2015 mpaka 2.7% katika robo
ya kwanza ya mwaka 2016, ikiwa ni punguzo la 8% ndani ya kipindi
kisichozidi miezi sita. Hii ina maanisha kwamba Wananchi wetu wanazidi
kudumbukia kwenye ufukara kwa kasi tangu awamu ya tano ya Serikali ya
Chama Mapinduzi iingie madarakani
c)
Ukuaji wa sekta ya ujenzi katika robo ya mwisho ya mwaka 2015 ilikuwa
13.8% lakini ukuaji wa sekta hii katika robo ya kwanza ya mwaka 2016
ilikuwa ni 4.30%, ikiwa ni tofauti ya takribani -10%. Hii ni kwa sababu
uwekezaji katika sekta hii umeanza kushuka.
d)
Kasi ya ukuaji wa sekta ya usafirishaji imeporomoka kutoka kukua kwa
14.50% robo ya mwisho ya 2015 mpaka kukua kwa 7.9% robo ya kwanza ya
2016, ikiwa ni kuporoka kwa 7% katika kipindi cha miezi 6 tu ya kwanza
ya utawala wa Rais Magufuli. Kuporomoka kwa sekta ya usafirishaji
itaathiri watu wengi, wakiwemo madereva, matingo, pamoja na mama Ntilie
wanaowauzia chakula. .
Kwa kuzingatia mwenendo wa hali ya uchumi katika nchi, Kamati Kuu:
a)
Tunaitaka serikali izingatie sayansi ya uchumi katika kuendesha uchumi
wa nchi. Uamuzi wa CCM wa kuitelekeza serikali yake kwa mwanasiasa mmoja
anayedhani ndiye anayejua kila kitu na yeye kugeuka kuwa mshauri wa
washauri wa uchumi itasambaratisha uwekezaji nchini na kuua kabisa
juhudi za miaka 20 za kuvutia wawekezaji na kujenga uchumi shirikishi.
b)
Inahimiza wananchi kuzingatia kuwa msingi wa uchumi wetu ni uwekezaji
kutoka ndani na nje ya nchi. Msingi wa kuvutia wawekezaji ni utawala wa
sheria. Juhudi za serikali ya CCM za kuua utawala wa sheria zitaua
uwekezaji na kuangamiza uchumi wa nchi. Tusirihusu CCM iue uchumi wa
nchi kwa maslahi yake ya kisiasa na viongozi wake.
4. Umoja wa Kitaifa
Nchi
yetu imefanya juhudi kubwa katika miaka 50 iliyopita katika kujenga
umoja na mshikamano wa kitaifa kwa kuhakikisha kuwa makabila, dini na
baadaye vyama vya siasa tunaishi bila kukamiana. Juhudi za dhati za
kupambana na ubaguzi ndiyo umekuwa msingi imara wa kujenga Umoja wa
Kitaifa na amani tunayojivunia.
Hata
hivyo, Kamati Kuu imezingatia kuwa utawala mpya wa Serikali ya CCM,
kupitia Mwenyekiti wake mpya na Rais wa Jamhuri wa Muungo, umeanza kwa
juhudi na kasi kubwa kuchokonoa na kumomonyoa misingi ya utaifa na umoja
wetu. Sasa tunaye Rais asiyechagua maneno na asiyejua aongee nini na
wapi. Vijana waliosoma kwa bidii katika mazingira ya shule
zilizotelekezwa na serikali ya CCM anawaita VILAZA.
Katikati
ya uhasama mkubwa wa kisiasa na kijamii huko Zanzibar Rais wetu
amefunga safari, sio kujaribu kutibu majeraha yaliyosababishwa na
kuchezewa kwa sanduku la kura, bali kuchochea uhasama chini ya ulinzi wa
vyombo vyetu vya dola vyenye jukumu la kulinda na kudumisha amani. Sasa
Rais wetu, kupitia kauli zake, ameanza kuubomoa muungano wetu
uliojengwa kwa unyenyekevu na katika mazingira magumu.
Kila
asimamapo kuhutubia, jambo moja la kutarajiwa kutoka katika kinywa cha
Rais wetu ni matamshi yanayodhoofisha nguzo fulani ya umoja, mshikamano
na undugu wetu kama taifa. Yote haya yakitokea chama chake cha CCM ama
kimekaa kimya au kinachekelea.
Inasikitikitisha
kwamba Chama kilichoasisiwa na Mwalimu Nyerere kinamruhusu kiongozi
wake kubomoa misingi ya umoja wa kitaifa na kuchochea chuki katika jamii
ya watanzania.
Kwa kuzingatia mtikisiko mkubwa katika umoja na mshikamano wa kitaifa unaoendelea nchini, Kamati Kuu:
a)
Tunalaani juhudi zinazofanywa na Serikali ya CCM kupitia Mwenyekiti wao
za kuchochea chuki katika jamii ya watanzania na kubomoa misingi ya
umoja wa kitaifa na amani ya nchi
b)
Tunatoa wito kwa watanzania wote waipendayo nchi yao kusimama kidete
katika kulinda misingi ya nchi yetu na kukataa chuki inayoanza kujengwa
na utawala wa CCM
c)
Tunatoa wito wa kipekee kwa viongozi wetu wa dini na wakuu wa nchi
waliopita, hususani Mzee Ali Hassan Mwinyi, Mzee Benjamin Mkapa na Mzee
Jakaya Mrisho Kikwete, pamoja na wazee wengine wanaoheshimika katika
nchi yetu wavae ujasiri wa kumuonya Mwenyekiti wa CCM kuwa juhudi zake
za kuchochea chuki katika jamii yetu ya watanzania zitasambaratisha
Taifa letu.
5. Hitimisho
i)
Sisi kama chama cha siasa, tunaendelea kusisitiza kuwa tutaunga mkono
juhudi za serikali ya awamu ya tano katika kupambana na ufisadi na
kujenga uwajibikaji nchini.
ii)
Tunaamini kwa dhati kabisa kuwa kuheshimu na kulinda demokrasia na
kuzingatia utawala wa sheria nidyo msingi wa mapambano dhidi ya ufisadi.
Tunasisitiza kuwa mtu yeyote, wa kawaida au kiongozi, anayesema kwamba
anaweza akapambana na ufisadi kwa kukanyaga misingi ya demokrasia na
utawala wa sheria mtu huyo ni mwomgo na kwa kweli ni fisadi na anataka
kujenga himaya mpya ya ufisadi. Mtu huyo, pamoja na mambo yake yote,
yafaa akataliwe na kudharauliwa haraka!
iii)
Tunasisitiza kuwa msingi wa uchumi wetu ni kuvutia uwekezaji wa ndani
nan je ya nchi. Kuzingatia utawala wa sheria ndiyo msingi wa kuvutia
uwekezaji. Juhuzi za hivi karibuni za serikali ya CCM za kujaribu kuua
utawala wa sharia ni juhudi ovu za kuua uchumi wa nchi yetu. TUZIKATAE
juhudi za kuua utawala wa sheria kwa kuwa zitaangamiza taifa letu
kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto, Mb
Kiongozi wa Chama
Dar es Salaam,
Jumanne 6 Septemba 2016.
Social Plugin