BODI YA MIKOPO YAGOMA KUTOA MIKOPO KWA WAOMBAJI WAPYA BAADA YA TCU KUSHUSHA VIWANGO VYA UDAHILI

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imesema haiwezi kutoa mikopo kwa waombaji wapya walioomba baada ya Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kushusha viwango vya udahili.

Wiki iliyopita, TCU ilitangaza kushusha viwango vya udahili bila kueleza sababu za kufanya hivyo.

Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa, amesema tume  hiyo haiwezi kuongeza muda kwa wanafunzi wapya kwa ajili ya kuomba mkopo kutokana na mchakato huo kufungwa.

Amesema tofauti na tume ya vyuo vikuu ambayo inaweza kufungua udahili na kutoa majina ya wale waliopata nafasi ndani ya siku tatu, HESLB huhitaji muda mrefu kupitia taarifa za waombaji hadi kutoa matokeo.

Kuhusu marejesho ya mikopo kwa wahitimu wa elimu ya juu waliokopeshwa na bodi hiyo, Mwaisobwa amesema idadi kubwa ya wadaiwa na waajiri wamejitokeza kulipa madeni yao na kuhakiki taarifa za madeni yao.

“Idadi kubwa ya wadaiwa wamejitokeza kulipa na kuhakiki taarifa zao, pia hata waajiri wengi wamejitokeza na kuthibitisha hili ni kwamba mapato tuliyokusanya yameongezeka kwa kiasi kikubwa” amesema Mwaisobwa.

Amesema wanaokaidi kulipa, watambue kuna sheria zitakazowabana, ikiwa ni pamoja na vifungo na penati, lakini hilo halitangulizwi bali mpaka mkopaji aonekane kukaidi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post