Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MSAFARA WA MAKAMU WA RAIS SAMIA SULUHU WAPATA AJALI


MSAFARA wa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ukiwa unaelekea wilayani Tandahimba ukitokea Mtwara Mjini, umepata ajali wakati gari moja katika msafara huo lililokuwa limebeba wasaidizi wake, lilipoacha njia na kupinduka na kusababisha majeruhi wanne.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Thobias Sedoyeka amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, na kueleza kuwa ajali hiyo imetokea leo saa nne na nusu asubuhi katika Kijiji cha Malanje wilayani Mtwara ambako gari aina ya Toyota V8 yenye namba za usajili ST 244 A liliacha njia na kupinduka.

“Ni kweli ajali imetokea katika Kijiji cha Malanje ambapo gari hiyo iliyokuwa imewabeba wasaidizi wa Makamu wa Rais iliacha njia na kupinduka,” alisema Kamanda Sedoyeka na kuwataja waliopata ajali kuwa ni Vincent Mbwana (35), Edward Andrew (26), Nehemia Mandia (36) na Maulida Hassan (32), wote ni wasaidizi wa Makamu wa Rais.

Aidha, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dk Wedson Sichwale alisema majeruhi hao wamepelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Ligula kwa ajili ya matibabu zaidi. “Baada ya ajali kutokea majeruhi tuliwakimbiza Kituo cha Afya cha Nanguruwe na baadaye tumewapeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Ligula kwa matibabu zaidi,” alisema Dk Sichwale.

Makamu wa Rais, Samia yupo mkoani Mtwara kwa ziara ya siku nne ambako anatembelea miradi mbalimbali ya maendeleo na kuzungumza na wananchi na kuhimiza shughuli za utekelezaji wa miradi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com