DENI la Taifa limezidi kupanda kutoka dola za Marekani bilioni 19. 69 Juni mwaka jana na kufikia Dola 23.2 ambazo ni zaidi ya Sh trilioni 51, sawa na ongezeko la asilimia 18.
Katika deni hilo ambalo limeongezeka kwa asilimia 18, Serikali inadaiwa Dola za Marekani bilioni 20.5 huku sekta binafsi zikiwa Dola bilioni 2.7.
Taarifa ya kupanda kwa deni la taifa ilitolewa jana bungeni na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, alipokuwa akijibu swali na Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema).
Kubenea aliitaka Serikali ieleze ina deni kiasi gani na mikakati yake katika kukabiliana na ongezeko la deni hilo.
Katika swali lake, Kubenea alisema kuwa Serikali ya awamu ya nne ilikopa fedha kwenye benki za nje za kibiashara, kwamba mwaka 2011 ilikopa Sh trilioni 15 na kufanya deni la taifa kufikia Sh trilioni 21 kabla ya mwaka 2015 na ilikopa tena Sh trilioni 9 na kulifanya kufikia Sh trilioni 39.
Akijibu swali hilo la msingi, Dk. Kijaji alisema deni la Serikali lilitokana na mikopo ya ndani na nje kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo, ikiwamo ya kimkakati ya kuboresha majiji, ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa KV 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga, mabasi yaendayo haraka, ujenzi wa bomba la gesi, mitambo ya kusafirisha gesi, upanuzi wa Uwanja wa Ndege Dar es Salaam na mradi wa maji Ruvu chini na Ruvu juu.
Alisema mikakati ya Serikali kukabiliana na deni hilo, ni pamoja na kuongeza ukusanyaji wa mapato, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuendelea kutafuta misaada na mikopo nafuu na kukopa mikopo michache ya kibiashara kwa miradi yenye kuchochea kwa haraka ukuaji wa pato la taifa.
“Kudhibiti ulimbikizaji wa madai ya kimkataba kwa makandarasi na watoa huduma na kudhibiti madeni yatokanayo na dhamana za Serikali kwenye mashirika ya umma kwa kufanya ufuatiliaji wa karibu,” alisema Dk. Kijaji.
Alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2010/2011 Serikali ilipokea mikopo ya nje yenye masharti nafuu na ya biashara Sh trilioni 1.3 na mwaka 2014/2015 ilipokea mkopo wa Sh trilioni 2.3. Mikopo hiyo haikufikia Sh trilioni 15 kwa mwaka 2011 na trilioni 9 kabla ya mwaka 2015.
Kutokana na hali hiyo, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni ambaye pia ni Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema), alisema kwa mujibu wa takwimu hadi kufikia Juni mwaka huu deni la taifa ni zaidi ya Sh trilioni 51, ambazo ukigawa kwa Watanzania kila mmoja anadaiwa zaidi ya Sh milioni 1.
Mbunge huyo alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kurejea katika Mpango wa Kusamehewa Madeni (HIPC).
Akijibu swali hilo, Dk. Kijaji alisema zipo nchi ikiwamo Iran na Iraq zilikuwa katika mpango wa kusamehe madeni hayo, lakini kutokana na migogoro katika nchi hizo hatua hiyo imeshindwa kufikiwa.
Swali hilo pia lilijibiwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba ambaye alisema Serikali haikopi fedha kwa ajili ya matumizi ya kawaida bali ni kwa shughuli za maendeleo ya nchi.
WADAU WAZUNGUMZIA
Akizungumzia hali hiyo, Mkurugenzi wa Mtandao wa Madeni na Maendeleo Tanzania (TGDD), Hebron Mwakagenda, alisema kitendo cha kukopa mara kwa mara lazima deni hilo liongezeke.
Alisema awali deni hilo lilifikia asilimia 38 na kwamba iwapo litafikia asilimia 50, Serikali inapaswa kusimama kukopa hadi watakapoanza kulipa madeni.
“Ikiwa deni la taifa limefikia asilimia 50, lazima tusimame kwanza kukopa hadi tutakapoanza kulipa madeni hayo, la sivyo hakutakuwa na sifa ya kukopa tena,” alisema Mwakagenda.
PROFESA NGOWI
Kwa upandewake mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe na mchambuzi wa masuala ya uchumi, Profesa Honest Ngowi, alisema kukua kwa kasi deni hilo ni suala linalotisha.
“Jambo la msingi la kujiuliza ni kwanini deni linakua, linakua kwa sababu tunakopa na tunakopa kwa sababu fedha za makusanyo yetu ya ndani hazitoshi kwenda kutoa huduma mbalimbali kwa umma.
“Lakini kwa muda mrefu tumekuwa tunasema kwamba kati ya vitu vinavyotisha si deni, bali ni kule kukua kwa kasi kwa deni hilo,” alisema.
Profesa Ngowi alisema kukua kwa deni hilo kunatisha kwani jinsi ilivyo linapaswa kulipwa, wakati fedha hizo zingeenda kuwekezwa kwenye miradi mingine ya maendeleo.
“Kama nilivyosema deni linapaswa kulipwa, lakini inatisha kuona linakua kwa kasi wakati huo huo lazima lilipwe, lakini kama fedha hizo zilikopwa na kupelekwa kwenye maendeleo ni sawa… si mbaya. Lakini kama hazikupelekwa kwenye shughuli za maendeleo itakuwa ‘isssue’,” alisema.
PROFESA SEMBOJA
Mtaalamu wa Masuala ya Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Haji Semboja, alisema kuendelea kukua kwa deni hilo ni changamoto kwa Serikali iliyopo madarakani.
“Kwa kawaida nchi masikini hulazimika kukopa fedha kutoka nchi nyingine kwa ajili ya kuziweka kwenye miradi ya maendeleo. Lakini kadiri unavyochukua ikiwa uwezo wako wa kulipa deni ni mdogo, maana yake ni kwamba mzigo wa deni unazidi kuongezeka,” alisema Profesa Semboja.
Alisema iwapo deni linaongezeka wakati fedha zikiwa zimewekezwa kwenye miradi ya maendeleo ni rahisi kulilipa.
“Lakini kama tulikopa kwa ajili ya shughuli zisizo za maendeleo, kwa ajili ya kula tu, ni hatari,” alisema.
Aliongeza: “Hata hivyo Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli imeanza vizuri, inasisitiza kuwekeza kwenye maendeleo, hiyo ni sahihi kwa sababu nchi itapata fedha na mkiwa na miradi mingi ya maendeleo ni rahisi kukopesheka zaidi.”
Hata hivyo, alisema Rais Magufuli ameonyesha nia ya kuwekeza kwenye shughuli za kimaendeleo ikiwamo kilimo, ujenzi wa madaraja, barabara na nyinginezo, ni vema akasimamia kwa dhati suala hilo ili kwamba fedha zinazokopwa zitumike vile inavyopaswa kuwa.
“Tukichukulia mfano daraja la Kigamboni ni mradi mzuri wa maendeleo, ingawa inaweza kuchukua muda mrefu kupatikana fedha za kulipa deni. Lakini ndivyo inavyotakiwa, kwamba fedha ziwekezwe kwenye miradi na si vinginevyo,” alisema.
ZITTO
Akizungumza na waandishi wa habari juzi Dar es Salaam, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema katika kipindi cha miezi sita tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, uchumi wa taifa umeporomoka kwa asilimia nne.
Akinukuu taarifa ya Benki Kuu (BoT), alisema katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba mwaka jana, pato la taifa lilikua kwa asilimia tisa. Lakini kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu, limepungua na kufikia asilimia 5.5.
Alisema kulingana na mwenendo wa uchumi, Kamati Kuu ya chama hicho imeitaka Serikali izingatie sayansi ya uchumi katika kuendesha nchi.
Zitto alisema uamuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kuitelekeza Serikali kwa mwanasiasa mmoja na kudhani ndiye anayejua kila kitu na kuwa mshauri wa washauri wa uchumi, itasambaratisha uwekezaji nchini na kuua kabisa juhudi za miaka 20 za kuvutia uwekezaji na kujenga uchumi shirikishi.
“Tunawahimiza wananchi kuzingatia kuwa msingi wa uchumi wetu ni uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi, hivyo msingi wa kuvutia uwekezaji ni utawala bora. Serikali ya CCM inapaswa kujua kuwa kuua utawala wa sheria ni kuua uwekezaji pamoja na uchumi wa nchini.
“Hali hiyo inamaanisha kuwa ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo wa awamu ya tano umepungua kwa asilimia 4,” alisema Zitto.
Zitto ambaye alikuwa akitoa msimamo wa Kamati Kuu ya chama chake iliyoketi mapema wiki hii Dar es Salaam, alisema katika sekta ya kilimo ambayo hutegemewa na wananchi kwa asilimia 70, pato la uchumi limezidi kushuka kutoka kasi ya ukuaji wa asilimia 10 kwa robo ya mwisho wa mwaka jana hadi kufikia asilimia 2.7 katika kipindi cha Januari hadi Machi, mwaka huu.
Aprili 21, mwaka huu wakati wa mkutano wa Bunge la bajeti, Mwenyeikiti wa Kamati ya Bajeti, Hawa Ghasia, alisema deni la taifa limeendelea kukua na kufikia Sh trilioni 36.39 hadi kufikia Desemba 2015, ikiwa ni tofauti na ililivyokuwa Sh trilioni 14.4 kwa mwaka 2011/12.
“Kwa sasa deni limefikia takribani asilimia 44.9 ya pato la taifa, limeendelea kukua kutokana na Serikali kuendelea kukopa kwa ajili ya kugharimia nakisi ya bajeti,” alisema.
Habari hii imeandaliwa na Rachel Mrisho (Dodoma), Patricia Kimelemeta na Veronica Romwald (Dar)-Mtanzania
Social Plugin