HIZI HAPA HOJA 11 ZILIZOMREJESHA LIPUMBA CUF...ATINGA OFISINI KWA MDUNDIKO,RISASI ZARINDIMA

 
HOJA 11 zilizotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, zimetosha kumrejesha katika wadhifa wake, Mwenyekiti ‘aliyejiuzulu’ wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba.


Mbali ya Lipumba viongozi wengine ambao msimamo wa Msajili unawarejesha madarakani moja kwa moja baada ya kusimamishwa na Baraza Kuu la Uongozi la CUF, katika kikao chake cha Agosti 30, mwaka huu kilichofanyika jijini Dar es Salaam ni Naibu Katibu Mkuu Bara Magdalena Sakaya ambaye pia ni Mbunge wa Kaliua na Naibu Mkurugenzi wa Habari Taifa, Abdul Kambaya.

Wengine ni Mbunge wa Mtwara, Maftaha Nachuma, wajumbe wa Baraza Kuu Taifa, Masudi Omari Mhina, Thomas Malima, Ashura Mustafa na Kapasha Kapasha. Pia Musa Haji Kombo, Habibu Mnyaa na Haroub Shamis ambao wataendelea kuhesabika kama wanachama halali wa chama hicho.

Katika barua yake kwa viongozi wa CUF, Msajili alieleza kuwa amefikia msimamo wake huo baada ya kupata nafasi ya kusikiliza pande zote zinazosigana katika mgogoro huo wa uongozi ndani ya chama hicho.

Alisema katika kufikia maamuzi hayo amezingatia Mamlaka na wajibu wa Msajili kushughulikia mgogoro huo, Kujiuzulu kwa Profesa Lipumba, Profesa Lipumba kutengua barua yake ya kujiuzulu, Uhalali wa Mkutano Mkuu Maalumu wa CUF wa Agosti 21, mwaka huu na baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu kuhitaji Profesa Lipumba aitwe katika chumba cha mkutano kujieleza.

Nyingine ni uhalali wa kura zilizopigwa kukubali au kukataa Profesa Lipumba kujiuzulu, uhalali wa kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Agosti 28, mwaka huu, utaratibu wa kuchukua hatua za kinidhamu, uhalali wa kamati iliyoundwa na Baraza Kuu la Uongozi la Agosti 28 ili kufanya kazi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Taifa na mwisho ni kuhusu uhalali wa uteuzi wa viongozi wa kitaifa uliofanywa na kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa cha Agosti 28, mwaka huu.

Kutokana na hoja hizo, Jaji Mutungi katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana alisema: “Hivyo, baada ya upembuzi kama nilivyobainisha hapo juu, msimamo na mwongozo wangu ni kwamba Profesa Ibrahim Lipumba bado ni Mwenyekiti halali wa Taifa wa CUF na walalamikaji wanachama waliosimamishwa na waliofukuzwa uanachama wote bado ni wanachama halali wa CUF.

“Aidha viongozi ambao uongozi wao uliathirika na maamuzi yasiyo halali ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa cha Agosti 28, mwaka huu, bado ni viongozi halali. Natumia fursa hii kuwapa angalizo kwamba, kwa kuwa kamati iliyoundwa kuongoza chama na viongozi walioteuliwa na kikao hicho si halali na kwa kifungu cha 88 (2) cha Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258, hawaruhusiwi kufanya shughuli yoyote ya chama.”

Msajili kushughulikia mgogoro

Msajili akifafanua hilo alisema kwa kifungu cha 10 (f) cha Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258 kinahitaji chama cha siasa kuwasilisha orodha ya viongozi wake wa kitaifa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na kwa kuwa Kifungu 8A (1) kinampa mamlaka Msajili kuhifadhi taarifa za viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa na kwa kuwa Kanuni ya 5 (1) ya Kanuni za Usajili wa Vyama vya Siasa toleo namba 111 la mwaka 1992 inakitaka kila chama kuwasilisha taarifa kwa Msajili panapotokea mabadiliko ya uongozi wa kitaifa wa chama husika.

“Hivyo kwa mustakabali wa majukumu yanayotolewa na vifungu hivyo, Msajili wa Vyama vya Siasa anao wajibu wa kuhakikisha taarifa za mabadiliko ya uongozi anazoletewa na chama cha siasa ni sahihi, kwa maana ya kujiridhisha kuwa mabadiliko hayo ya uongozi yamefanyika na mamlaka halali ya chama na pia yametekelezwa kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za chama husika. “Kwa mantiki hiyo basi na nikijielekeza kwenye vifungu vya sheria nilivyoainisha, ni dhahiri kwamba Msajili wa Vyama vya Siasa anayo mamlaka na wajibu wa kisheria, kuchunguza na kujiridhisha kuhusu usahihi wa mabadiliko katika uongozi wa kitaifa wa chama yaliyofanyika na masuala yote yanayohusiana na mabadiliko hayo,” alisema Msajili.

Kujiuzulu kwa Profesa

Lipumba Kuhusu hilo Msajili alisema kwa mujibu wa Ibara ya 117 (2), kiongozi wa Chama cha CUF, hata kama mhusika amebainisha tarehe ya kujiuzulu katika barua yake ya kujiuzulu, atahesabika kuwa amejiuzulu baada tu ya mamlaka iliyomchagua au kumteua kukubali.

Alisema kwa mujibu wa Ibara hiyo, ni sahihi kusema kwamba Profesa Lipumba alikuwa bado ni Mwenyekiti halali wa Taifa wa CUF hata wakati wa kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Agosti 21, hivyo hata yeye kujiita Mwenyekiti wa Taifa mstaafu kabla ya kujiuzulu kwake kukubaliwa na mamlaka husika si sahihi.

Kutengua barua yake ya kujiuzulu

Akizungumzia hilo Msajili alisema, “Katiba ya CUF iko kimya kuhusu hilo, hivyo hapakuwa na kizuizi kwa Profesa Lipumba kutengua barua yake ya kujizulu kwa kuzingatia ukimya huo kwa upande wa uongozi wa CUF kuchukua hatua pindi walipopokea barua yake ya kujiuzulu na hivyo kutoa mwanya kwa mhusika kuitengua barua yake ya kujiuzulu.

“Si hivyo tu, bali pia barua yake ya kutengua kujiuzulu haikukataliwa na uongozi wa CUF.Alichoelezwa Profesa Lipumba ni kwamba asianze kazi tarehe aliyopanga kuanza kazi ili asubiri kwanza Katibu Mkuu ashauriane na wanasheria wa chama, ambapo mpaka suala hili linawasilishwa mbele yangu, Profesa Lipumba alikuwa bado hajapewa mwongozo wowote kuhusiana na barua yake ya kutengua kujiuzulu,” alisema Msajili.

Uhalali wa hoja

Msajili akitoa msimamo wake kuhusu hoja ya uhalali wa Mkutano Mkuu wa Agosti 21, alisema pamoja na malumbano kuhusu akidi ya wajumbe lakini kwa vyovyote vile mkutano huo ulikidhi matakwa ya Ibara ya 114 inayosema kuwa ili akidi kutimia idadi ya wajumbe waliohudhuria kikao inapaswa kuzidi nusu ya wajumbe wote, na hivyo idadi ya wajumbe 700 ilikidhi matakwa ya Katiba.

Kuhusu hoja ya baadhi ya wajumbe kuhitaji Profesa Lipumba aitwe katika chumba cha mkutano kujieleza, Msajili alisema hata kama Profesa Lipumba angekuwa si mjumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu ili mradi uwepo wake yalikuwa ni matakwa ya wajumbe wa mkutano huo, basi alipaswa kupewa fursa katika mkutano huo kuthibitisha kuwa, barua iliyosomwa na Katibu Mkuu kuhusu kujiuzulu kwake ni yake na kueleza sababu za kujiuzulu na hivyo kumkatalia ilikuwa ni kukiuka Ibara ya 116 ya Katiba ya chama hicho.

Kwa hoja za uhalali wa kura zilizopigwa kukubali au kukataa Profesa Lipumba kujiuzulu, Msajili alisema zoezi la kupiga kura za kukubali au kukataa kujiuzulu kwa Profesa Lipumba lilifanyika katika mazingira ya vurugu na hivyo kufanya zoezi hilo kukosa uhalali na kutoa mfano kuwa zoezi la kujua idadi ya wapiga kura kabla ya kupiga kura halikufanyika, ukizingatia kuwa baada ya vurugu kuzuka, kuna wajumbe walitoka nje ya ukumbi kuogopa vurugu na watu wasio wajumbe kuingia ndani ya ukumbi.

Kuhusu uhalali wa uteuzi wa viongozi wa kitaifa uliofanywa na kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa cha Agosti 28, Msajili alisema kwa mujibu wa Ibara ya 115 (1) iwapo nafasi ya kiongozi yeyote ipo wazi, basi mamlaka yake ya uteuzi itamteua mtu wa kukaimu nafasi hiyo.

“Kwa mujibu wa Ibara ya 91 (1) (m) mamlaka ya uteuzi wa Naibu Katibu Mkuu ni Baraza Kuu la Taifa, hivyo laiti uamuzi wa kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa cha Agosti 28 ungekuwa si batili, basi uteuzi wa Joran Bashange kuwa Kaimu Naibu Katibu Mkuu ungekuwa sahihi, kwa maana ya kwamba Baraza Kuu la Uongozi lina mamlaka hayo.

“Hata hivyo kwa upande mwingine, uteuzi wa Mbaraka Maharagande kuwa Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma una dosari nao si sahihi kwa sababu kwa mujibu wa Ibara ya 91 (1) (f) mamlaka yake ya uteuzi ni Mwenyekiti wa Taifa na si Baraza Kuu la Taifa,” alisema Msajili na kusema adhabu kwa mtu anayefanya shughuli za chama bila kufuata taratibu ni kifungo cha miezi sita, faini isiyozidi Sh milioni moja au vyote kwa pamoja.

Lipumba atinga ofisini kwa mdundiko

Katika tukio lingine mchana jana Profesa Lipumba alifika katika ofisi za chama hicho zilizopo Buguruni jijini Dar es Salaam huku akiandamana na umati wa wafuasi wa chama hicho huku wakisindikizwa na ngoma maarufu katika ukanda wa Pwani ya Mdundiko.

Wafuasi wa Profesa

Lipumba walianza kukusanyika katika ofisi hizo kuanzia asubuhi baada ya kupata taarifa za kuwepo kwa barua kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, ikimtambua mwanasiasa huyo kama Mwenyekiti halali wa chama hicho kwa mujibu wa Katiba ya chama.

Ilipotimu saa saba mchana Profesa Lipumba alifika katika eneo zilipo ofisi hizo akiwa na kundi la wafuasi wake waliokuwa wakicheza kwa ustadi ngoma ya mdundiko, lakini walikumbana na kizuizi cha kuingia ndani kutokana na geti kuu kuwa limefungwa.

Zuio hilo lilidumu kwa muda usiozidi dakika nne, ambapo baadaye baadhi ya wafuasi wa kiongozi huyo waliamua kuruka ukuta ili kuingia ndani kumfungulia geti kumwezesha kuingia ndani.

Wakati matukio hayo yakiendelea, polisi waliokuwa wamefika mapema ili kudhibiti usalama katika eneo hilo walikuwa wakishuhudia wakiwa ndani ya magari matatu yaliyokuwa yamesimama kando ya geti, wakiwatazama wafuasi hao wakitumia nguvu ili kuingia ndani ya ofisi hizo.

Hata hivyo haikuwa kazi rahisi kuingia ndani ya ofisi hizo kwani wakati wakiendelea kuruka ukuta, zilisikika risasi zikipigwa na askari wa kampuni binafsi ya ulinzi aliyekuwa analinda ofisi hizo, lakini alidhibitiwa baadaye na wafuasi hao ambao walimnyang’anya silaha na kuikabidhi kwa polisi.

Baadaye wafuasi hao walianza kumpa kichapo askari huyo wa ulinzi kabla ya wazee wa chama hicho kujitokeza na kumuokoa na kulazimika kumfungia katika choo kimojawapo cha ofisi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuingia ofisini kwake, Profesa Lipumba alisema kurejea kwake kunatokana na uamuzi uliotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa, huku akieleza hatua mbalimbali alizochukua tangu alipoandika barua ya kujiuzulu, barua ya kutengua uamuzi wake na yaliyotokea katika vikao mbalimbali vya chama hicho, ambazo kimsingi zinamfanya kuwa na sifa ya kuendelea kuwa Mwenyekiti halali kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho.

CUF wajibu mapigo

Hata hivyo jana jioni Chama cha CUF kilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kikisema kuwa Sheria ya Vyama vya Siasa Namba 5 ya mwaka 1992 haimpi mamlaka wala uwezo wowote Msajili wa Vyama vya Siasa kutoa ushauri, msimamo au mwongozo kwa vyama vya siasa kuhusiana na maamuzi ya vikao vya chama.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui ilisema katika taarifa ya chama hicho kuwa, “Chama kimepokea kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kile kinachoitwa “Msimamo na Ushauri wa Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu Mgogoro wa Uongozi wa Kitaifa wa Chama cha Civic United Front (CUF)” ambao uliwasilishwa Ofisi Kuu ya Chama, Buguruni, jana usiku. Chama hakikuomba ushauri kwa Msajili na hivyo tunamwambia ushauri wake abaki nao mwenyewe.”

Alisema chama hicho kinawataka wanachama wake na wananchi wote kutambua kwamba Msajili hana uwezo kisheria wa kusikiliza mashauri yanayohusiana na malalamiko dhidi ya maamuzi ya vikao vya vyama vya siasa na kuyatolea uamuzi na kwamba uwezo huo ni wa Mahakama pekee.

Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko- Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post