KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amewasilisha tuhuma sita dhidi ya Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, ambaye amefukuzwa uanachama.
Maalim Seif aliwasilisha hoja hizo mbele ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la chama hicho kilichofanyika jana mjini Unguja visiwani Zanzibar, ambapo wajumbe walitumia Katiba ya CUF, Ibara 10(1)(C), kumfukuza uanachama Profesa Lipumba.
Wakati Baraza Kuu likichukua hatua hiyo, Profesa Lipumba alitumia siku ya jana kuendesha kongamano lililofanyika Buguruni jijini Dar es Salaam, ambapo amepinga uamuzi huo na kusema kuwa kikao hicho ni batili kwa mujibu wa katiba ya CUF.
Akisoma maazimio ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi, Mwenyekiti wa kikao hicho, Katani Ahmed , alisema walijadili kwa kina mashtaka dhidi ya Profesa Lipumba kutokana na kile alichodai hujuma alizofanya Ofisi Kuu za CUF Buguruni jijini Dar es Salaam Septemba 24, mwaka huu.
Alisema kutokana na hali hiyo Baraza Kuu limepokea mashtaka dhidi ya Prof. Lipumba yaliyoandaliwa na Kamati ya Utendaji ya Taifa ambayo kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, Ibara ya 108 (1) ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia nidhamu ya chama katika ngazi ya Taifa na kuyawasilisha mapendekezo yake mbele ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.
“Baraza Kuu limeridhika kwamba Kamati ya Utendaji ya Taifa imefuata masharti yote ya katiba ya chama ya 1992 (Toleo la 2014) katika kuandaa mashtaka hayo kutokana na mtuhumiwa, Prof. Ibrahim Lipumba, kuvunja katiba ya chama, Ibara ya 12 inayohusu ‘Wajibu wa Mwanachama” hasa Ibara ndogo za 12 (6), 12(7) na 12(16).
“Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limeridhika kwamba Kamati ya Utendaji ya Taifa ilimfikishia mtuhumiwa, Prof. Ibrahim Lipumba, barua ya wito Kumb. Nam. CUFHQ /OKM /WM /2016 /Vol.1 /49 ya Septemba 24 mwaka huu ambayo pia ilikuwa na maelezo ya tuhuma na kumtaka afike mbele ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kilichofanyika leo (jana) kuja kujieleza na kujitetea kwa nini asichukuliwe hatua za kinidhamu kwa mujibu wa katiba ya chama kwa kuvunja masharti yanayohusu “Wajibu wa Mwanachama”,” alisema Katani .
Mwenyekiti huyo wa kikao ambaye pia ni Mbunge wa Tandahimba, alisema Baraza Kuu limesikitishwa na dharau iliyooneshwa na Prof. Lipumba dhidi ya kikao hicho ambacho ni chombo cha juu chenye mamlaka ya kusimamia uongozi wa chama licha ya kupelekewa wito wa kumtaka afike mbele yake.
Alisema kitendo cha dharau kinaonesha jinsi gani heshima na uaminifu wa Prof. Lipumba kwa chama ulivyoshuka na wameridhika kwamba kwa kuwa Prof. Lipumba akiwa mtuhumiwa alichagua mwenyewe kudharau wito wa kufika kujieleza na kujitetea ambayo ni haki yake kama mwanachama kwa mujibu wa Ibara ya 11(6) ya katiba ya chama, halikuwa na sababu ya kutoendelea kumjadili na kuchukua hatua dhidi yake.
“Baraza Kuu limeridhika na mashtaka dhidi ya Prof. Ibrahim Lipumba kwamba kwa kitendo chake cha kuongoza na kusimamia kikundi cha wahuni kuvamia Ofisi Kuu ya chama, Buguruni, Dar es Salaam, siku ya Jumamosi, Septemba 24 Septemba, 2016 na watu hao aliowaongoza na kuwasimamia kupiga walinzi waliokuwepo.
“Kuvunja na kuharibu mali za chama na hivyo kuharibu heshima na taswira ya chama mbele ya jamii ndani na nje kwamba ametenda makosa kinyume na “Wajibu wa Mwanachama” kama ilivyoelezwa kwenye Ibara ya 12(6), 12(7) na 12(16) za katiba ya chama.
“Baada ya kuridhika na mashtaka hayo, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa limeamua kwa kutumia uwezo wake kwa mujibu wa Ibara ya 10 (1) (c) na kwa kura zote 43 za wajumbe wake waliohudhuria kumfukuza uanachama Prof. Ibrahim Lipumba, kuanzia leo (jana).
“Kwa maamuzi haya, Baraza Kuu linaweka bayana kwa wanachama wa CUF, Watanzania na mamlaka zote nchini kwamba kuanzia leo, Prof. Ibrahim Lipumba hana haki ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na shughuli zozote za chama,” alisema Katani.
Pamoja na hali hiyo alisema CUF inawapa pole wanachama wake walioathirika kutokana hatua ya msajili kuingilia mambo ya chama kinyume na uwezo alionao na pia kwa matendo ya kihuni yaliyofanywa na Prof. Ibrahim Lipumba na kikundi chake kuvamia ofisi kuu ya chama hicho.
Barua ya Msajili
Mbali na kuchukua hatua hiyo Katani alisema kikao hicho cha dharura kilichohudhuriwa na wajumbe 43 kati ya 53 kilikuwa na ajenda tatu ikiwemo barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa ya Septemba 23, mwaka huu.
“Baraza Kuu limeukataa ushauri, msimamo na mwongozo wa Msajili wa Vyama vya Siasa alioutoa kupitia barua yake ya tarehe 23/09/2016 kwa sababu Sheria ya Vyama vya Siasa (Political Parties Act, No. 5 of 1992) – Sura ya 258 haimpi mamlaka wala uwezo wowote kutoa ushauri, msimamo au mwongozo kwa vyama vya siasa kuhusiana na maamuzi ya vikao vya chama.
“Na kwa kulitambua hilo ndiyo maana katika matamko yake yote aliyoyatoa, Msajili ameshindwa kutaja kifungu gani cha sheria hiyo kinampa uwezo huo. Baraza Kuu limesikitishwa sana na kitendo cha Jaji Francis Mutungi kujishushia hadhi, kujifedhehesha na kujivunjia heshima mbele ya macho ya jamii ndani na nje ya nchi.
“Na hili amejivunjia heshima yeye na ofisi anayoiongoza kwa kuvunja sheria na kudharau maamuzi ya Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia auamuzi Mei 5, 2005 wa Jaji T.B. Mihayo katika kesi ya Emmanuel Nyenyemela na Magnus Msambila v/s Registrar of Political Parties & Others (Civil Case No. 6 of 2003) ambapo Jaji Mihayo aliamua kwamba:
“… I do not see anywhere in the Political Parties Act where the Registrar has power to bless or condemn meetings of political parties or decisions that they make.”
Tafsiri yake ikiwa ni kwamba, “… Sioni popote katika Sheria ya Vyama vya Siasa ambapo Msajili ana madaraka ya kubariki au kupinga vikao vya vyama vya siasa au maamuzi ambayo vikao hivyo vinafanya,” alinukuu.
Katani ambaye alichaguliwa kuongoza kikao hicho baada ya mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi Julius Mtatiro kutokuwepo, alisema wanamtanabahisha Msajili wa Vyama vya Siasa kwamba atabeba dhamana kwa yote yaliyofanywa na yatakayofanywa na Prof. Lipumba na kikundi chake alichodai cha wahuni.
Kauli ya Lipumba
Akizungumza na MTANZANIA jana kuhusu uamuzi uliochukuliwa na Baraza Kuu dhidi yake, Prof. Lipumba alisema chombo chenye mamlaka ya kumvua uanachama kiongozi huyo ni Mkutano Mkuu na si Baraza Kuu hata kama limeongozwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.
Alisema kabla ya kufikia uamuzi huo, Katibu Mkuu alipaswa kuitisha Mkutano Mkuu ambao pamoja na mambo mengine, ulitakiwa kumjadili ili wajumbe waweze kumpigia kura ya kumwondoa.
Prof. Lipumba, alisema baada ya kufanyika kwa kikao hicho, wajumbe wanapaswa kumjadili na kumpa nafasi ya kujitetea ili atakapomaliza waweze kuamua kama wanamfukuza ama laa.
“Kwa mujibu wa katiba ya CUF, Baraza Kuu la Uongozi halina mamlaka ya kunivua uanachama mimi, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu Bara, kutokana na Katiba yetu inavyojieleza. Chombo chenye mamlaka ya kufanya hivyo ni Mkutano Mkuu na si vinginevyo,” alisema Prof. Lipumba.
Alisema chama hicho kinaendeshwa kwa kufuata kanuni na katiba, na si uamuzi wa watu wachache kwa masilahi yao binafsi, hivyo basi uamuzi wa kumfukuza uanachama haukuzingatia katiba ambao alisisitiza kuwa ni batili.
“Hakuna mtu au kiongozi anayeongoza chama kwa kufuata utaratibu wake binafsi, bali tunafuata kanuni na katiba ya chama ambayo ndio inayotoa mwongozo wa nini kifanyike ndani ya chama hicho,” alisema.
Wafuasi wakamatwa
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limekamata watu 22 wanaosadikiwa kuwa wanachama wa CUF kwa tuhuma za kufanya fujo katika ofisi za chama hicho.
Akizungumza jana Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simoni Sirro alisema watuhumiwa hao walikamatwa eneo la Kinondoni wakiwa na zana za kufanyia uhalifu katika makao makuu ya CUF Buguruni.
Alisema watuhumiwa hao walieleza kuwa ni wanachama wa CUF kutoka kisiwani Unguja na waliokuja kwa ajili ya kazi maalumu ambao wapo katika kitengo cha ulinzi cha chama hicho.
“Watuhumiwa hao wanaosadikiwa ni wanachama wa CUF walikamatwa maeneo ya Kinondoni wakiwa na zana za kufanyia uhalifu ambazo ni jambia, visu vitano pamoja na chupa za kupulizia (spray) zikiwa kwenye boksi zenye chupa 10 zenye maandishi ya kichina.
“Baada ya kuwakamata na kuhojiwa, walisema wametoka Unguja kwenye matawi mbalimbali na wapo zaidi ya 100 na wamekuja kwa maelekezo ya kiongozi wao waliomtaja Nassoro Ahmed Mazrui (Naibu Katibu Mkuu CUF-Zanzibar) aliwaamuru kuungana na walinzi wenzao wengine waliopo katika ofisi za chama hicho zilizopo Buguruni ,” alisema Kamishna Sirro.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Saidi Mohamedi Zaharani, Hamis Hamis, Mohisin Ally, Masoud Igasa Fumu, Juma Omary, Mbaruku Hamis, Juma Haji Mwanga, Hamis Nassoro Hemedi, Mohamed Omary Mohamedi, Nassoro Mohamedi Ally na wengine 12.
Chanzo-Mtanzania
Social Plugin