NB-Picha Haihusiani na habari hapa chini
******
Katika hali isiyokuwa ya kawaida mkazi wa Mandewa, Manispaa ya Singida, Said Juma (24), amelazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Singida baada ya kung’atwa hadi kunyofolewa zaidi ya theluthi moja ya ulimi wake na mwanamke waliyekuwa wakinyonyana ndimi.
Tukio hilo la aina yake limetokea Septemba 12, mwaka huu saa 3:30 usiku wa sikukuu ya Idd el Hajj ambapo kutokana na kung’atwa huko kwa ulimi imesababisha kijana huyo apoteze uwezo wa kuongea zaidi ya kutoa maelezo kwa njia ya maandishi.
Akizungumza kwa njia ya maandishi kijana huyo aliyelazwa katika chumba cha wagonjwa wa kinywa na meno amesema siku ya tukio akiwa njiani kutoka kwenye sherehe za Idd El Hajj alikutana na mwanamke huyo kwenye grosari iliyopo eneo la Mandewa na baadaye mwanamama huyo alimwomba amsindikize nyumbani kwake.
Kijana huyo anaeleza kuwa akiwa njiani,mwanamke huyo alimtaka wafanye mapenzi na baada ya kumkatalia alimuomba amuage kwa kumpa ulimi “kula denda” ndipo alipomng’ata hadi kumnyofoa kipande cha ulimi na kutoweka nacho.
“Nilikubali kumsindikiza, tukiwa njiani aliniomba tufanye mapenzi,nilipokataa alinilazimisha na baada ya kuona sitaki aliomba tuagane kwa kunyonyana ndimi, nilikubali ombi hilo,wakati tukiendelea, alianza kunivua mkanda wa suruali lakini nilimzuia ndipo aliponing’ata ulimi wangu na kuondoka na kipande”,anaeleza kijana huyo.
Madaktari wanaomtibu kijana huyo wanasema kidonda hicho baada ya kuacha kutoa damu kilitengeneza maambukizi kukawa na harufu inatoka mdomoni na kwamba hali yake inaendelea vizuri.
Wamesema ingawa amepata ulemavu lakini kijana huyo anaweza kuongea tena baada ya kupona japo matamshi yake ya maneno hayatakuwa kama alivyokuwa anaongea mwanzo.
Mama mzazi wa kijana huyo tayari ameripoti tukio hilo kituo cha polisi kwani mbali na mtoto wake kupata ulemavu pia alipata kipigo kutoka kwa mwanamke huyo.
Bado mtuhumiwa hajakamatwa na polisi wanafanya ufuatiliaji.
Chanzo- Kipindi cha Matukio Radio Free Africa
Social Plugin