Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Majanga Kigoma! WATOTO 8 WAFARIKI KWA KUTEKETEA KWA MOTO MAMA ZAO WAKIWA KWENYE NGOMA YA KIENYEJI


Mabaki ya nyumba zilizoungua kwa moto na kusababisha vifo vya watoto nane mkoani Kigoma
 *****
Watoto nane wamefariki dunia katika ajali ya moto katika kitongoji cha Tandala eneo la Kona nne Kijiji cha Chakulu katika wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.Mwandishi wa Malunde1 blog mkoani Kigoma,Rhoda Ezekiel anaripoti.


Inaelezwa kuwa chanzo cha moto huo ni jiko lililokuwa ndani ya nyumba hiyo kuachwa likiwa na moto na baada ya upepo mkali kupeperusha moto huo huku mama zao wakiwa kwenye sherehe ya ngoma ya kienyeji.


Akizungumza na waandishi wa habari leo kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Kigoma ,DCP Fredinand Mtui amesema tukio hilo limetokea Septemba 4 mwaka huu katika kijiji cha Chakulu,ambapo nyumba moja mali ya Samke John mkazi wa eneo hilo iliungua na kusababisha vifo vya watoto wake wawili na wadada yake wawili na wa majirani watatu na mmoja wa jirani kujeruhiwa.


Mtui ametaja majina ya watoto wa mwenye nyumba hiyo waliofariki kuwa ni Masanja Samke (8), na Majaliwa Samke (2) na Leonard Luhende (08) na Raphaeli Luhende (06) ambao ni watoto wa dada yake pamoja na Hamiss Bala (06), Jala Magere (04) watoto wa jirani majeruhi mmoja ambaye ni mtoto wa jirani aliyetambulika kwa jina la Magere Ngusa.


Akifafanua zaidi kuhusu tukio hilo amesema mwenye nyumba aliondoka nyumbani kwake takribani siku mbili zilizopita kwenda kufanya vibarua na kuwaacha wake zake wawili na watoto wao.

“Siku ya tukio ilipofika saa sita usiku wake zake hao waliondoka kwenda kwenye sherehe ya ngoma za kienyeji wakiwa na majirani na kuwaacha watoto wao wakiwa wamelala katika nyumba moja ambayo ni mali ya Samike John”,ameeleza Kamanda Mtui.

“Ilipofika saa saba usiku nyumba hiyo ilishika moto na kuteketea na kusababisha vifo na majeruhi vya watoto hao, jitihada za kuwaokoa watoto hao zilifanyika na kushindikana ambapo mtoto mmoja aliokolewa Mariam Bala (06)”,ameongeza kamanda Mtui.


Hata hivyo Malunde1 blog imeambiwa kuwa mtoto Mariam Bala aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Urambo mkoani Tabora kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo ,amefariki dunia leo jioni na kufanya idadi ya watoto waliopoteza maisha kuwa nane.

Kamanda Mtui amesema chanzo cha moto huo ni jiko lililopo ndani ya nyumba hiyo lililoachwa likiwa na moto na baada ya upepo mkali kupeperusha moto huo ulipelekea nyumba hiyo kushika moto na kuteketeza nyumba na kusababisha vifo hivyo.

Amesema hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wanawake hao na kwamba mazishi ya watoto saba yamefanyika leo wilayani humo yakiongozwa na mkuu wa wilaya ya Uvinza.

Akizungumzia tukio hilo alipotembele eneo la tukio mkuu wa mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali mstaafu Emmanuel Maganga amesema serikali itafanya uchunguzi ili kujua kama moto huo ni wa bahati mbaya au mkono wa mtu polisi itafanya uchunguzi na hatua zitachukuliwa.

Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Nguruka Staphord Chamgeni amesema jitihada za kuokoa maisha ya watoto hao zilishindikana kutokana na majeraha waliyokuwa nayo kutokana na kuungua sana na kupoteza fahamu.
Na Rhoda Ezekiel-Malunde1 blog Kigoma

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com