Wakati
wanasiasa na wasomi wakimnyooshea kidole Msajili wa Vyama vya Siasa,
Jaji Francis Mutungi (pichani) kwa uamuzi wake wa kumtambua aliyekuwa
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, mwenyewe ameibuka na kusema
kuwa hatua yake hiyo haikulenga kumrudishia msomi huyo nafasi yake ya
uenyekiti.
Jaji Mutungi jana alisema kuwa alichofanya ni kukishauri chama hicho kuhusu mgogoro uliokuwa ukikisonga na Lipumba aliamua kutumia ushauri huo kurudi mwenyewe kwenye nafasi yake hiyo kinyemela.
Kauli
hiyo ya Jaji Mutungi imekuja siku mbili tangu alipotoa waraka
unaoelezwa kumtambua Profesa Lipumba kama kiongozi halali wa CUF licha
ya kuandika barua ya kujiuzulu Agosti 6, mwaka jana akipinga vyama
vinavyounda Ukawa kumpa fursa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
kugombea urais.
“Isome
barua yangu…, mimi nimeamua watu waijadili umenielewa? Ni vizuri
wanavyoijadili, ila nilitarajia waijadili kwa tija sio kwa hasira,” alisema Jaji Mutungi.
Alipoulizwa kuhusu polisi kumsaidia Profesa Lipumba kuingia katika makao makuu ya CUF kwa mtutu alisema: “Hizo ni taratibu ambazo (polisi) wanatumia kwa kuzingatia sheria nyingine za nchi.”
Juni
mwaka huu, Profesa Lipumba alimwandikia barua Katibu Mkuu wa CUF,
Maalim Seif Sharif Hamad kutengua barua yake ya kujiuzulu na kutaka
arejee kwenye kiti chake, uamuzi uliozusha mtafaruku huku Mkutano Mkuu
wa chama hicho ulioketi Agosti 21 ukiridhia kujiuzulu kwake licha ya
kuwa ulivunjika.
“Barua
yangu inajieleza sina haja ya kuichambua. Nimekujibu baada ya kuona
mjadala huo (katika mitandao) nilitegemea (waliomtukana) wawashauri CUF
cha kufanya badala ya kuanza kunitukana,” alisema Jaji Mutungi.
“Sasa huko mahakamani wanakotaka kwenda kama mahakama ikiamua kama Mutungi alivyoshauri huko nako watatukana pia?” alihoji.
Wanasiasa na wasomi
Mwenyekiti
wa Chama cha Kijamii (CCK), Constatine Akitanda alisema alichofanya
msajili ni kupandikiza zogo ndani ya CUF jambo ambalo linasikitisha.
Akitanda
alisema ndani ya CUF kuna bundi ambaye alikuwa anasumbua watu ila
msajili ameongezea mgogoro huo na kuwa alichokifanya si sawa kwa mujibu
wa mamlaka yake.
“Unajua
hii nchi inachezewa sana hivi mtu anajiuzulu mwenyewe halafu anaamua
kurejea mwenyewe bila kufuata taratibu ni aibu, lakini nadhani kuna
mkono wa mtu,’ alisema.
Mwenyekiti
wa Chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira alisema anachokiona ndani ya
CUF ni uwepo wa biashara haramu ambayo inaweza kuua chama hicho.
Alisema
ni wakati mwafaka kwa wafanyabiashara haramu hao wakajulikana katika
pande zote kwani ni aibu kuvumilia kasoro hizo zitawale vyama vya siasa.
Naibu
Katibu Mkuu wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Dominata Rwechungura
alisema migogoro ndani ya vyama vya siasa ipo, hivyo ni jukumu la CUF
kutatua ili kurejesha amani na upendo kati yao.
Mwenyekiti
wa Chama cha United People Democratic Party (UPDP), Fahimu Dovutwa
alisema kinachotokea ni msiba unaoacha pengo ndani ya CUF na vyama vya
siasa nchini.
Dovutwa
alisema pia pengo la mwasisi wa CUF, marehemu Shaban Mloo linaonekana
na kuwataka wazee wa chama hicho kukaa ili kukinusuru chama.
“Huu
ni msiba katika siasa za Tanzania, naomba CUF watafute wazee wao ili
waweze kusuluhisha hali hiyo kwa maslahi ya chama chao kwani pengo la
Mloo linaonekana,” alisema.
Katibu
wa Habari na Uenezi wa NCCR Mageuzi, David Kafulila alisema mgogoro wa
CUF unaweza kutolewa uamuzi na mahakama pekee kwa kuwa msajili hana
mamlaka ya kufanya alichokifanya. Kafulila alisema msajili anapaswa
kushauri kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa na si kama
alivyoelekeza kwani anaongeza mgogoro zaidi.
Mwenyekiti
wa ADC, Hamad Rashid alishauri CUF kutumia vikao kumaliza tofauti zao,
huku akibainisha kuwa ndani ya chama hicho kuna viashiria vya udikteta
na usultani.
Mbunge
wa Tandahimba CUF, Katani Katani alisema kwa sasa wamethibitisha jinsi
Lipumba anavyotumika kwani pamoja na Jeshi la Polisi kukataza
maandamano, wafuasi wa Lipumba waliandamana bila kuzuiwa.
Alisema haiwezekani chama kikaendeshwa kwa ajenda za watu wachache ambao wanatumikia matumbo yao na makundi yao na si chama.
Mhadhiri
Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Kitivo cha Sheria,
Dk. Onesmo Kyauke alisema msajili anakosea na kuwataka CUF wakimbilie
mahakamani kupata haki.
Credit: Jamboleo
Credit: Jamboleo
Social Plugin