TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
The
Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi) kimepokea kutoka Ofisi ya
Msajili wa Vyama vya Siasa kile kinachoitwa “Msimamo na Ushauri wa
Vyama vya Siasa kuhusu Mgogoro wa Uongozi wa Kitaifa wa Chama cha Civic
United Front (CUF)” ambao uliwasilishwa Ofisi Kuu ya Chama, Buguruni,
jana usiku.
Baada ya kupokea Ushauri huo, The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi) kinapenda kueleza yafuatayo:
1.
Sheria ya Vyama vya Siasa (Political Parties Act, No. 5 of 1992) haimpi
mamlaka wala uwezo wowote Msajili wa Vyama vya Siasa kutoa ushauri,
msimamo au mwongozo kwa vyama vya siasa kuhusiana na maamuzi ya vikao
vya Chama.
2.
Msimamo huo wa kisheria wa nchi hii umetiliwa nguvu na kuthibitishwa na
Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia UAMUZI wa
tarehe 9/5/2005 wa Jaji T.B. Mihayo katika kesi ya Emmanuel Nyenyemela
na Magnus Msambila v/s Registrar of Political Parties & Others
(Civil Case No. 6 of 2003) ambapo Jaji Mihayo aliamua kwamba:
“…
I do not see anywhere in the Political Parties Act where the Registrar
has power to bless or condemn meetings of political parties or decisions
that they make.”
Tafsiri
ya uamuzi huo ni kwamba, “… Sioni popote katika Sheria ya Vyama vya
Siasa ambapo Msajili ana madaraka ya kubariki au kupinga vikao vya vyama
vya siasa au maamuzi ambayo vikao hivyo vinafanya.”
3. Kwa msingi huo, CUF hatukuomba ushauri kwa Msajili na hivyo tunamwambia ushauri wake abaki nao mwenyewe.
4.
Kwa msingi huo huo, tunawataka wanachama wa CUF na wananchi wote
kutambua kwamba Msajili hana uwezo kisheria wa kusikiliza mashauri
yanayohusiana na malalamiko dhidi ya maamuzi ya vikao vya vyama vya
siasa na na kuyatolea uamuzi. Uwezo huo ni wa Mahakama. Hivyo tunawataka
wanachama wa CUF na wananchi wote kupuuza ushauri huo wa Msajili na
wamwachie mwenyewe ndoto zake na propaganda za kitoto.
5.
Ni fedheha na aibu kwa Msajili wa Vyama vya Siasa mwenye hadhi ya Ujaji
kukubali kutumiwa kiasi hicho na kushindwa hata kufanya rejea kuhusu
uamuzi wa Mahakama Kuu tulioutaja hapo juu ambao umeweka bayana kwamba
hana madaraka na uwezo aliojifanya anao.
Itakumbukwa
kwamba Wabunge wa CUF walifanya mkutano na waandishi wa habari mjini
Dodoma tarehe 15 Septemba, 2016 na kumtahadharisha Msajili asikubali
kutumiwa kufanya alichokuwa anatakiwa kukifanya. Ni bahati mbaya sana
kwamba amefanya kile kile ambacho Wabunge wa CUF walieleza kwamba
walikuwa na taarifa kuwa ameagizwa kukifanya.
6.
Tunajua kwamba baada ya hatua hiyo ya Msajili kufanya kazi asiyo na
uwezo wala mamalaka nayo na katika kutimiza malengo ya wanaomtuma,
mchana wa leo Prof. Ibrahim Lipumba na kikundi chake cha wahuni
kimevamia Ofisi Kuu ya CUF, Buguruni, Dar es Salaam na kupiga watu na
kufanya uharibifu wa mali. Tunamwambia Msajili wa Vyama vya Siasa
atabeba dhamana kwa yote yaliyofanywa na yatakayofanywa na kikundi hicho
ikiwemo watu watakaoumizwa na uharibifu wa mali utakaofanywa kutokana
na tamko lake hilo ambalo halina msingi wa kisheria.
7.
Tunatambua yote haya yanafanywa kwa sababu watawala wameingiwa kiwewe
kutokana na hatua kubwa ambazo zimefikiwa na CUF katika kupigania haki
yake ya ushindi ulioporwa katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa tarehe 25
Oktoba, 2015.
CCM
haijakaa sawa tokea iliposhindwa vibaya na CUF katika uchaguzi wa Rais,
Wawakilishi na Madiwani mwaka 2015 na sasa imepata mfadhaiko kutokana
na jinsi jumuiya ya kimataifa ilivyosimama kidete kutetea maamuzi hayo
ya
kidemokrasia na haki za binadamu za Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.
Ni
vyema watawala na kibaraka wao Prof. Ibrahim Lipumba na kikundi chake
pamoja Msajili anayewatumikia wakatambua kwamba CUF haiyumbishwi na
michezo yao ya kitoto na itaendelea kusimamia malengo yake ya kupigania
haki za kidemokrasia za wananchi wa Zanzibar na Tanzania kikamilifu.
8.
Chama kinasisitiza tena kwamba maamuzi ya Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa
wa tarehe 21 Agosti, 2016 na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la tarehe 28
Agosti, 2016 ni halali na yako pale pale na kwamba Prof. Ibrahim
Lipumba si Mwenyekiti wa CUF na wanachama waliosimamishwa au kufukuzwa
wataendelea kubakia wamesimamishwa au kufukuzwa isipokuwa tu iwapo vikao
vya Chama vitakapofanya maamuzi mengine.
9.
Chama kinawataka viongozi wake wote na wanachama wake katika ngazi zote
kuanzia Taifa hadi Tawi kuendelea na kazi zao za ujenzi wa Chama kama
kawaida na kuendelea kufuatilia harakati za Chama chao kupigania ushindi
wetu wa tarehe 25 Oktoba, 2015.
HAKI SAWA KWA WOTE
NASSOR AHMED MAZRUI
NAIBU KATIBU MKUU - CUF