MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi ya Bukombe mkoani Geita imemhukumu Mwalimu wa Shule ya Msingi Umoja, Daniel Nyingati kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya Sh milioni 1.6 baada ya kupatikana na makosa ya kuomba na kupokea rushwa, anaripoti Benjamin Masese wa gazeti la Mtanzania.
Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Bukombe, Gabriel Kurwijila.
Alisema mshitakiwa Nyingati amekutwa na hatia ya kuomba rushwa ya Sh 130,000 kutoka Marco Elias aweze kumdahili mtoto wake aliyekuwa amehitimu masomo ya shule ya msingi kinyume na sheria.
Hakimu Kurwijila alisema ushahidi ulitolewa mahakamani pande zote mbele ya waendesha mashitaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kudhibiti Rushwa Tanzania (Takukuru), Kelvin Murusuri na Husna Kiboko umejitosheleza na kumtia hatiani mwalimu Nyingati.
Alisema mahakama inamhukumu mwalimu Nyingati kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya Sh milioni 1.6 kwa kuwa alitenda kosa la kuomba na kupokea rushwa.