JESHI la Polisi katika Mkoa wa Mara linamshikilia Juritha Lucas (60), mkazi wa Kijiji cha Masinki Wilaya ya Serengeti mkoani humo, kwa tuhuma ya kufanya biashara haramu ya kuuza binadamu kinyume cha sheria.
Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Ramadhani Ng'anzi, aliliambia gazeti hili kwa njia ya simu kutoka mjini Musoma jana kuwa, mwanamke huyo alikamatwa na polisi akiwa na mabinti watano wenye umri kati ya miaka 15 na 23 aliokuwa anataka kuwauza.
Kamanda Ng'anzi alisema mabinti hao ni wakazi wa kijiji cha Muruvyagiza, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, ambako ndiko mwanamke huyo aliwatoa na kuwasafirisha hadi katika kijiji cha Masinki wilayani Serengeti, kwa nia ya kuwauza kwa kuwaozesha kwa wanaume kwa bei kati ya Sh 150,000 hadi Sh 300,000 kila mmoja, kulingana na umri, uzuri na tabia ya binti husika.
Polisi walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu biashara hiyo, waliweka mtego na ndipo Septemba 4, mwaka huu, walimkamata mwanamke huyo na kumhoji na akakiri kuwachukua mabinti hao kutoka mkoani Kagera kwa ajili ya kuwauza.
Jitihada zinafanyika ili kuwasiliana na wazazi wa mabinti hao ili kuwachukua.
Kamanda Ng'anzi hakuwataja majina kwa sababu za kiusalama zaidi, lakini alisema wanaendelea na uchunguzi wa kina na kuwa baada ya upelelezi kukamilika, watamfikisha mahakamani kujibu tuhuma ya kufanya biashara ya binadamu kinyume cha sheria.
Katika tukio jingine, polisi mkoani hapa, kwa kushirikiana na Kikosi cha Kuzuia Ujangili (KDU), wamewakamata watu wawili, Godfrey James (39), mkazi wa Chalinze mkoani Pwani na Adeus Evarist (34) mkazi wa Mwanza, wakiwa na nyara za serikali kinyume cha sheria.
Walikamatwa juzi katika Kijiji cha Hunyari wilayani Bunda wakiwa na vipande vitatu vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilogramu 15 ambavyo vina thamani ya zaidi ya Sh milioni 18.
- Imeandikwa na Ahmed Makongo-Mtanzania
Social Plugin