Mtoto aliyetambuliwa kwa jina la Hellena Peter Maulid mwenye umri wa miezi 11 amefariki dunia baada ya kutumbukia kwenye kisima cha maji chenye urefu wa futi 60 kilichopo karibu na nyumba yao katika eneo la Mapinduzi,kata ya Ndala katika manispaa ya Shinyanga.
Tukio hilo limetokea Septemba 14 mwaka huu majira ya moja
usiku.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio walisema mama mzazi wa mtoto huyo Catherine Cosmas alikuwa anachota maji huku akiwa amebeba mtoto lakini ghafla mtoto akatumbukia kisimani kasha mama huyo akaanza kupiga kelele kuomba msaada kutoka kwa majirani.
“Mama alikuwa anachota maji kwenye kisimani….unajua huku hatuna maji,Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira katika manispaa ya Shinyanga SHUWASA wamekata maji,leo ni siku ya pili kata ya Ndala na Masekelo maji yamekatika,kwa hiyo huyu mama alikuwa anachota maji bahati mbaya mwanaye katumbukia kisimani”,walieleza wakazi wa eneo hilo ambao hawakutaka kutaja majina yao.
Waliongeza kuwa kuna taarifa zinaenea kuwa mtoto
huyo alitumbukia kisimani wakati akitambaa eneo la kisima lakini ukweli ni
kwamba mama huyo alikuwa amembeba mtoto huyo wakati anachota maji.
“Wananchi walitaka kumshambulia mama wa mtoto
huyo kwa kusababisha kifo cha mtoto wake,hivyo ili kumnusuru ndiyo wakaanza
kusema mtoto alikuwa anatambaa eneo la kisima,kama mama hakuwepo eneo la kisima
alijuaje kama mwanaye katumbukia kisimani muda huo huo?”,walihoji wananchi hao.
Kwa mujibu wa taarifa ya kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga
ACP Muliro Jumanne Muliro alisema mtoto huyo ambaye alikuwa anaishi na mama
yake Catherine Cosmas Malimi(23) mkazi wa Ndala alitumbukia kwenye kisima hicho
chenye urefu wa futi 60 kilicho karibu na nyumba yao.
Akizungumzia chanzo cha kifo hicho,Muliro alisema awali
kabla ya kifo chake,mtoto huyo alikuwa anamfuata mama yake kipindi alipokwenda
katika kisima hicho kuchota maji na mama yake alimrudisha nyumbani na baadaye
mama huyo akiwa anaendelea na shughuli za nyumbani,mtoto huyo alirudi peke yake
katika eneo la kisima kisha kutumbukia.
Aliongeza kuwa mtoto huyo aliopolewa katika kisima hicho na
majirani akiwa amepoteza fahamu na kupelekwa katika hospitali ya mkoa wa
Shinyanga na kabla ya kuanza kupatiwa matibabu alifariki dunia.
Kamanda Muliro alisema mwili umefanyiwa uchunguzi na
kukabidhiwa ndugu zake kwa ajili ya kwenda kufanya mazishi wilayani Kahama
nyumbani kwa baba wa marehemu Peter Maulid Sabu na kwamba hakuna mtu yeyote
anayetuhumiwa kuhusiana na tukio hilo.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Social Plugin