Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS MAGUFULI ATAWATANGAZIA VITA WATU WALIOFICHA FEDHA MAJUMBANI

Rais John Magufuli amewataka watu walioficha fedha majumbani kuziachia ziingie kwenye mzunguko vinginevyo anaweza kuamua kuzibadili ili wakose mahali pa kuzipeleka. 

Amesema watu hao wamekuwa na utaratibu wa kutoa fedha zao katika benki na kuzificha kwa kuogopa kuwa atabaini kiasi walichonacho, hivyo akawataka kuachana na tabia hiyo kwa sababu fedha hizo ni mali yao. 

Akizungumza katika mkutano wa 14 wa mwaka wa wahandisi uliofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jana, Rais Magufuli aliyetumia dakika 73 kuzungumza na wahandisi hao na kueleza mikakati na changamoto zinazoikabili Serikali ukiwamo wizi na ufisadi, alisisitiza;  
“Huu ujumbe ni kwa wale wanaoficha fedha, waziachie na wajiandae, naweza kuamua baada ya siku mbili tatu nabadilisha fedha na hizo zilizofichwa katika magodoro ziozee huko. Ni nafuu mzitoe mziweke katika mzunguko zikafanye kazi,” alisema. 

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu na wahandisi kutoka ndani na nje ya nchi, Rais Magufuli alisema katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano hakuna fedha za bure. 

Alibainisha kuwa kipindi cha nyuma, fedha zilikuwa nyingi mitaani kwa sababu baadhi ya watu walikuwa wakiiba fedha za Serikali, huku akitoa mfano wa jinsi mabilioni ya fedha za watumishi hewa yalivyotafunwa, jambo alilosema sasa limedhibitiwa. 

“Nyinyi wahandisi ni wachapa kazi, huu ndiyo wakati wa kutajirika.Tumieni nafasi hii maana watu walizoea kupata fedha za bure. Waliokuwa wanatafuta dili katika wizara hawapati kitu na sasa nikijua mtendaji wa Serikali umepiga dili utaondoka tu,” alisema. 

“Fedha za bure hazipo na ndiyo maana thamani ya nchi na fedha yetu imeanza kuongezeka na mfumuko wa bei umeshuka mpaka asilimia 5.1.” 

Alisema wakati fulani akiwa anatoka mkoani Geita, mfuko wa saruji ulikuwa unauzwa Sh26,000 lakini sasa unauzwa Sh16,000. 

"Wanaoficha fedha ni wachache. Watu watapata fedha za kutosha kwa kufanya kazi. Wafikirie kufanya uwekezaji wa viwanda vyao na nyinyi wahandisi muwe namba moja.” 

Changamoto na mikakati ya serikali yake
Alisema licha ya Serikali kuamua kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka 87,000 hadi 137,000, imebainika kuwa wilaya moja mkoani Arusha ina wanafunzi hewa zaidi ya 10,000 na wilaya nyingine iliyopo Mwanza ina wanafunzi hewa zaidi ya 8,000. 

Kuhusu mapato ya Serikali, alisema baada ya kuingia madarakani yalipanda kutoka Sh800 bilioni hadi Sh1.3 trilioni lakini wakati hayo yanafanyika, Serikali imebaini wafanyakazi hewa zaidi ya 16,500 na kusema hiyo ndiyo Tanzana aliyoikuta. 

Rais Magufuli pia alieleza mikakati ya kununua meli mbili, kujenga reli ya kisasa, kukarabati viwanja vya ndege na kufafanua sababu za Serikali kununua ndege mbili aina ya Bombadier Q400, ambazo zimeshalipiwa asilimia 40. 

“Hizi ndege hazili mafuta, kasi yake nzuri, zinatua uwanja wowote hata wa changarawe. Wapo wanaoziponda eti hazina kasi, kama unataka kasi kapande za jeshi,” alisema huku akicheka. 

Huku akieleza jinsi wahandisi wa nje wanavyotekeleza miradi kwa gharama kubwa, alisema katika bajeti ya mwaka 2016/17, Serikali ilitumia Sh100 bilioni kwa ajili ya kukarabati viwanja saba vya ndege vya lami, lakini wapo waliotumia Sh105 bilioni kujenga barabara ya kuruka na kutua ndege katika Uwanja wa Ndege Mwanza, fedha ambazo ni nyingi. 

“Uwanja wa ndege Dar es Salaam unaokarabatiwa sasa, zimejengwa njia tatu (za kuruka ndege) na lile jengo (la abiria) lakini zimetumia Sh650 bilioni na gharama hizo zimewekwa na wahandisi. Tunahitaji kufanya uchunguzi, maana gharama hizi ni kubwa sana, kwa nini Watanzania tunachezewa hivi?” alihoji na kuongeza, “Ni bora wangepewa wahandisi wa Tanzania wakala hizi hela.” 

Alisema wahandisi wazawa wanaweza kujipanga na kupata tenda ya kujenga reli ya kisasa, kujenga bomba la gesi kutoka Tanga kwenda Uganda na hata kujenga viwanja vya ndege. 

Wizi unavyofanyika sekta ya madini
Alisema katika sekta ya madini, nchi inaibiwa na kutoa mfano jinsi dhahabu inavyochimbwa wilayani Kahama, kisha wahusika kuchukua mchanga na kwenda nao nje ya nchi kwa ajili ya kusafishwa.

“Kinachosafishwa huko nje hatujawahi kukiona, wahandisi mmekaa kimya. Kuna uhakika gani katika kontena kama hakuna kilo 200 za dhahabu ambazo wameziyeyusha na kuzichanganya na mchanga? Hivi wahandisi tumeshindwa kuweka utaratibu wa kubaini kilichomo katika mchanga? Tunashangilia mtu anasafirisha mchanga na sisi tunakubali kuwa wanasafirisha mchanga, mchanga unaondoka na viongozi wetu hata majeshi yetu na polisi unasindikiza mali yako.”

Alisema suala hilo pia linapaswa kuwa changamoto kwa viongozi na wanasiasa na akahoji sababu za kila mgodi wa dhahabu kuwa na uwanja wa ndege, 

“Tena hizi ndege wakati mwingine zinaruka moja kwa moja. Sisi Watanzania ni watu wa ajabu sana. 

“Nasikia Profesa Muhongo (Sospeter – Waziri wa Nishati na Madini) atatoa mada katika mkutano huu, atueleze kwa namna gani mchanga wetu utaacha kupelekwa nje? Katika vitu vinavyoniumiza ni pamoja na hili. Haya mamchanga tuyashike tuangalie kilichomo humo ndani. Tanzania tumechezewa na kuibiwa mno, nipo serikalini najua. Kila mahali ni dili, ukigeuka huku dili, ukienda huku dili, kila mahali ni dili tu,” alisema.

Siri ya kuteua wahandisi wengi serikalini 
Rais Magufuli alisema, wakati akiomba kura katika kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita, alinadi mkakati wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, lakini hakuwahi kusema watu watakaomsaidia kwa sababu aliamini wahandisi hawatamtupa mkono katika kufanikisha hilo. 

Huku akifichua siri ya kujaza wahandisi katika serikali yake, alisema taaluma hiyo ni muhimu katika maendeleo ya nchi na kuwataka kuwatumia viongozi hao kujenga uchumi wa Taifa, ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda. 

“Tusipotumia wahandisi kamwe tusizungumze kuhusu maendeleo ya nchi yetu, tusahau. Nimeteua wahandisi kutekeleza mambo kwa niaba ya wahandisi. Mnatumika kujenga uchumi wa watu wengine. Jipangeni nawaunga mkono, anzisheni viwanda… kampuni zenu na kupata kazi maana hakuna nchi duniani isiyotaka kujenga watu wake,” alisema. ...

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com