Rais Dkt. John Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa
wa Mwanza John Mongella kufuatia vifo vya watu 13 vilivyosababishwa na
ajali ya barabarani iliyotokana na basi la abiria la Kampuni ya Super
Shem kuligonga basi dogo la abiria (Daladala) katika kijiji cha Mwamaya
kilichopo katika Kata ya Hungumalwa, Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza.
Ajali hiyo imetokea leo saa 12:15 asubuhi baada ya basi hilo dogo
lililokuwa likitoka Kijiji cha Shirima kwenda Nyegezi Mjini Mwanza
kuingia ghafla barabara kuu na kisha kugongwa na basi la Kampuni ya
Super Shem lililokuwa likitoka Mkoani Mbeya kwenda Mwanza.
Katika ajali hiyo watu wote 13 waliopoteza maisha na majeruhi 15 waliolazwa hospitali walikuwa abiria wa basi dogo lililogongwa.
Rais Magufuli ameelezea kupokea taarifa za ajali hiyo kwa mshituko
mkubwa hasa ikizingatiwa kuwa imetokea siku moja tu tangu Watanzania
wengine 12 wapoteze maisha katika ajali ya basi la Kampuni ya New Force
iliyotokea katika kijiji cha Lilombwi, Kata ya Kifanya, Tarafa ya
Igominyi Mkoani Njombe.
"Nimesikitishwa sana na vifo vingine vya watanzania wenzetu
waliopoteza maisha katika ajali huko Mwanza, nakuomba Mkuu wa Mkoa wa
Mwanza, John Mongella unifikishie salamu za pole kwa familia zote
zilizopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika ajali hii.
"Nawaombea wote
waliotangulia mbele za haki wapumzishwe mahali pema na pia wote
walioguswa na msiba wawe na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu
katika kipindi kigumu cha majonzi ya kuondokewa na jamaa zao,"
amesisitiza Rais Magufuli.
Rais Magufuli pia amewaombea majeruhi wote wa ajali hii wapone haraka
ili waungane na familia zao na kuendelea na shughuli za ujenzi wa
Taifa.