Wabunge
wameibana Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB) kwa
kuongeza posho na kufikia jumla ya Sh1 bilioni katika kipindi kifupi
kiasi ambacho hakilingani na kazi wanayoifanya.
Kwa
kipindi kirefu, bodi hiyo imekuwa ikitupiwa lawama kwa kuchelewesha
mikopo, kushindwa kukusanya fedha za wanafunzi waliokopa na kutoa mikopo
kwa wanafunzi hewa.
Hivi
karibuni, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce
Ndalichako alisema bodi hiyo imetoa fedha za kujikimu na mafunzo kwa
vitendo kwa zaidi ya wanafunzi hewa 1,000.
Hata
hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa HELSB, Abdul-Razaq Badru alijitetea mbele
ya kamati hiyo akisema ni mgeni katika bodi hiyo na kwamba wanaweka
mikakati mizuri ya kurekebisha mambo hayo ili kuhakikisha inafanya kazi
kwa weledi zaidi.
Wakizungumza
katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) cha
kukagua Ripoti ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
ya mwaka wa fedha 2014/15 ya bodi hiyo, wabunge hao walisikitishwa na
kitendo cha bodi hiyo kushindwa kukusanya zaidi ya Sh3 trilioni
walizowakopesha wanafunzi mbalimbali tangu ianze kutoa mikopo kwa
wanafunzi wa elimu ya juu.
Walisema isipobadilika katika utendaji wake, kuna haja ya Serikali kuivunja na kuchagua benki moja kusimamia shughuli hiyo.
“Mnatakiwa
kuongeza juhudi na mikakati ili kuhakikisha kwamba madeni yote
yanakusanywa kwa wakati la sivyo naona kuna haja ya Serikali kuivunja
bodi nakutafuta njia nyingine,” alisema Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Raisa Mussa.
Mbunge
wa Same Mashariki (Chadema), Naghenjwa Kaboyoka alihoji kwa nini pamoja
na bodi hiyo kuwa na mameneja 18 na wafanyakazi wa kudumu 144, bado
utendaji wao umekuwa siyo wakuridhisha.
“Kwa idadi yenu tulitegemea kupata ripoti inayojitosheleza na hata utendaji wenu ulitakiwa kuwa wa ufanisi zaidi,” alisema.
Akijitetea
zaidi, Badru alisema kuna changamoto nyingi zinazoikabili bodi yake
lakini kwa sasa wamepiga hatua kubwa katika ukusanyaji wa madeni kutoka
kwa wanufaika wa mfuko huo.
“Kwa mfano Mei mwaka huu tulikusanya kiasi cha Sh2 bilioni na Juni tulikusanya Sh6 bilioni,” alisema.
Aliongeza
kuwa ipo mikakati mingi ambayo wamejiwekea katika kuhakikisha kwamba
bodi hiyo inakusanya madeni kikamilifu kutoka kwa wadeni wake wote.
“Kwa
kupitia mikakati yetu, tumeweza kuongeza idadi ya wanafunzi ambao
tunawapa mikopo kutoka 42,729 hadi 123,783. Katika kipindi hicho fedha
za mikopo zimeongezeka kutoka Sh56 bilioni hadi kufikia Sh465.3
bilioni,” alisema.