Vikundi vya wafuasi wa Profesa Ibrahim Lipumba wamekusanyika katika Ofisi za CUF Buguruni wakisubiri kumpokea mwenyekiti huyo wa zamani na kumwingiza ofisini.
Wanachama hao wanadai wana barua ya Msajili wa vyama vya siasa inayomtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti halali wa CUF.
Geti la ofisi za CUF limefungwa na ndani hakuna kiongozi yeyote wa chama.
Mashabiki hao wa Lipumba wanaoimba na kucheza, wanasema msafara wa Profesa uko njiani kuelekea kwenye ofisi hizo za makao makuu ya chama hicho.
Alipoulizwa kuhusu hali hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro amesema ndio wamepokea barua ya msajili na bado wanaisoma ili kuona imeelekeza kitu gani.
Hata hivyo, Mtatiro amesema kwa vyovyote vile msajili wa vyama vya siasa hana mamlaka ya kuingilia maamuzi ya vikao vya chama chochote cha siasa.
TAARIFA KUHUSU BARUA YA MSAJILI
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amesema kuwa Prof. Ibrahim Lipumba bado ni mwenyekiti halali wa Chama cha Wananchi (CUF).
Jaji Mutungi ameyasema hayo leo baada ya shauri hilo kufikishwa mezani kwake siku kadhaa zilizopita kuhusu nafasi ya uenyekiti ndani ya CUF.
Awali Prof. Lipumba ndiye alikuwa mwenyekiti, lakini alijiuzulu Agosti 2015, mwezi Agosti 2016 chama hicho kikamteua Julius Mtatiro kuwa mwenyekiti wa muda hadi hapo uchaguzi wa kumtafuta mwenyekiti mwingine utakapofanyika.
Lakini Prof Lipumba alirudi na kusema yeye ndiye mwenyekiti halali wa CUF kwa sababu barua yake ya kujiuzulu haikuwa imekubaliwa na Mkutano Mkuu wa CUF.
Baada ya mvutano wa muda mrefu ndani ya chama hicho, shauri hilo lilifikishwa katika ofisi ya msajili wa vyama vya siasa ambapo ametangaza rasmi kuwa Prof. Lipumba bado ni mwenyekiti.
Hapa chini ni ndiyo maamuzi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.