ZAIDI ya Wanawake 270 wamefariki dunia mkoani Katavi katika kipindi cha mwaka 2015/16, kutokana na vifo vinavyotokana na uzazi.
Hayo yalisemwa jana na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Dk. Obeid Mahenge, katika tamasha la vijana lililoandaliwa na Shirika la Marie Stopes Tanzania kwa kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi kwa lengo la kutoa elimu kuhusu uzazi wa mpango katika Manispaa ya Mpanda.
Alisema matumizi ya njia za uzazi wa mpango mkoani Katavi kwa mwaka jana ilikuwa ni asilimia 41.1 tu kiwango ambacho ni cha chini kikilinganishwa na kiwango cha taifa cha asilimia 60.
“Aidha imani potofu na taarifa zisizo sahihi kuhusu uzazi wa mpango zimesababisha wanawake wengi kuwa waoga wa kutumia njia hizi na kuishia kushika mimba zisizotarajiwa.
“Wanawake wana haki ya kutumia njia ya uzazi wa mpango kwa ajili ya afya zao na familia zao kwa ujumla hivyo wanaume mnatakiwa kuwa bega kwa bega na wake zenu kwani mwisho wa siku mtafaidika wote kwa kuwa na familia yenye afya bora,” alisema.
Mratibu wa Marie Stopes Tanzania, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Noelia Mbeyela alisema wanawake wengi nchini wamekuwa wakipata mimba za utotoni jambo ambalo ni hatari kwa afya zao.
Alisema kitendo hicho husababisha kupoteza maisha wakati wa kujifungua na kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU), kutokana na kutojua kujikinga na maambukizi hayo.
“Lakini pia, ushiriki wa wanaume kwenye masuala ya uzazi wa mpango ni mdogo ni wanawake pekee wamekuwa wakiifuata lakini bila ushiriki wa wanaume ni kazi bure.
“Athari ya kuzaa katika umri mdogo ni kwamba msichana anachukua jukumu la kuanza kulea familia wakati hajafikia umri wa kutunza familia na matokeo yake imekuwa ikiathiri uchumi wa nchi kwa kuwa na wategemezi wengi,” alisema.
Social Plugin