Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WASANII WAWILI KIZIMBANI KWA KUMDHALILISHA NA KUMUUDHI RAIS MAGUFULI KWENYE MTANDAO WA YOU TUBE

WAFUASI wawili wa Chadema, akiwemo Mwanamuziki Fulgency Mapunda (32) “Mwana Cotide”, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka ya kumuudhi Rais John Magufuli kupitia mtandao wa ‘YouTube’.




Mapunda na mtayarishaji wa muziki Mnesa Sikabwe (39), walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Wakili wa Serikali, Dereck Mkabatunzi alidai, Agosti mwaka huu katika eneo la Manzese, washitakiwa hao walisambaza taarifa zenye lengo la kumuudhi Rais Magufuli.

Inadaiwa kwa makusudi, washitakiwa hao kupitia mtandao wa YouTube, walisambaza wimbo uliopewa jina la ‘Dikteta Uchwara’ ambao umebeba maudhui ya kumdhalilisha na kumuudhi Rais Magufuli.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo, washitakiwa wote walikana kutenda kosa hilo. Wakili Mkabatunzi alidai upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea pia hawana pingamizi na dhamana kwa washitakiwa.

Hakimu Simba alisema, washitakiwa wataachiwa kwa dhamana endapo watakuwa na wadhamini wawili wakuaminika watakasaini hati ya dhamana ya Sh milioni 10. Washitakiwa walitimiza masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana hadi Oktoba 12, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

Imeandikwa na Flora Mwakasala-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com