Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATOA SIRI ZA WATU WANAOTOA TAARIFA ZA UHALIFU NA WATOA TAARIFA FEKI ZA UHALIFU KUTOA FAINI YA MIL 3

WIZARA ya Katiba na Sheria imesema watakaobainika kutoa siri za watu wanaotoa taarifa za uhalifu na wale ambao watabainika kutoa taarifa za uongo za uhalifu, watatozwa faini ya Sh milioni tatu au kifungo cha mwaka mmoja jela au vyote kwa pamoja.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Msaidizi Utekelezaji wa Katiba, Kamana Stanley alisema kumekuwepo na watu wanaovujisha siri za watoa taarifa na mashahidi wa matukio ya uhalifu, kitendo ambacho kinasababisha watu hao kupata madhara na kuingiwa na hofu ya kuendelea kutoa taarifa.

Alisema kuwepo kwa Sheria ya Kuwalinda Watoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi ya mwaka 2017, iliyoanza kutumika rasmi Julai Mosi mwaka huu, itasaidia kuwapatia ulinzi wa kisheria wale wote wanaotoa taarifa za uhalifu wa makosa mbalimbali wanayoyashuhudia yakitekelezwa.

“Kumekuwa na woga kwa wale walikuwa wakitoa taarifa lakini tunaamini kupitia sheria hii kutawafanya wao kuwa huru na kuleta matokeo chanya katika kupambana na uhalifu wa aina zote nchini,” alisema Stanley.

Pia alisema katika sheria hiyo wameweka utaratibu wa kuwapa motisha wale wote wanaofanikisha kuokoa mali ya umma, kupatikana kwa wahalifu, kulinda mazingira na maisha ya binadamu kutokana na uhalifu uliopangwa kufanyika lakini uhalifu huo ukazuiwa na taarifa waliyoitoa katika mamlaka husika.

Aidha alisema sheria hiyo pia itawafidia wale wote ambao wataathirika kutokana na taarifa watakazozitoa.

Pia alitoa wito kwa wananchi kujitokeza bila woga kutoa taarifa dhidi ya matendo ya aina zote yanayofanywa kinyume cha sheria ili kusaidia serikali katika mapambano dhidi ya uhalifu na kujenga jamii na taifa linalopinga uhalifu.

“Wananchi wakishiriki kufichua maovu ikiwa ni pamoja na yale yanayosababisha hasara kwa taifa itasaidia kukua kwa uchumi, ninaomba mjitokeze kwa wingi bila woga kutoa taarifa za uhalifu,” alisisitiza.

Imeandikwa na Sophia Mwambe-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com