Mahakama ya Wilaya Wilaya ya Mpanda Mkoa wa Katavi imewahukumu Watu wawili Nzira Luhemeja (42) na Vicent Makelele (32) wakazi wa Kijiji cha Mwamkulu Wilaya ya Mpanda jumla ya kifungo cha miaka 40 jela baada ya kupatikana na hatia ya kukamatwa na nyama ya kiboko kilo 70 wakiwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi.
Hukumu hiyo imetolewa jana na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda Odira Amwol baada ya Mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka uliokuwa unaongozwa na Elieza Chitalya mwendesha mashitaka wa TANAPA ulikuwa na mashahidi wanne na washitakiwa walijitetea wenyewe.
Wakati wa usomaji wa hukumu hiyo Mahakama ililazimika kusimama kwa muda wa dakika kumi baada ya mshitakiwa wa kwanza Nzira Luhemeja kubanwa na haja ndogo na kutokwa na jasho jingi wakati wakisomewa hukumu ya kesi hiyo na Hakimu Amwol.
Na ililazimika apelekwe chooni kwenye choo cha mahakamani hapo na askari polisi na kisha alirudishwa kizimbani na mahakama iliendelea.
Awali katika kesi hiyo mwendesha mashtaka wa TANAPA alidai kuwa washitakiwa hao walikamatwa Julai 21 mwaka huu huko katika eneo la Mto Katuma ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi .
Chitalya alidai kuwa washitakiwa hao wote wawili kwa pamoja walikamatwa katika eneo hilo na askari wa Hifadhi ya Katavi walikuwa doria na waliwakamata wakiwa na nyama ya kiboko yenye uzito wa kilo 70 yenye thamani ya shilingi milioni tatu .
Ilielezwa mahakamani hapo washitakiwa hao walikamatwa wakiwa na mguu mmoja wa mnyama Kiboko ambapo ni sawa na kiboko mmoja ambaye yuko hai wakiwa wamepakia kwenye mfuko wa sandarusi na wakiwa na baiskeli mbili .
Katika utetezi wao mshitakiwa wa kwanza Nzira Luhameja alikana kukamatwa na nyara hizo za serikali bali alidai kuwa yeye alikamatwa wakati akiwa njiani anakwenda kuoga katika mto Mafunsi ambao upo nje ya Hifadhi ya Katavi na wala hakuwa na nyara hizo za serikali.
Mshitakiwa wa pili alidai kuwa yeye hakukamatwa na nyama hiyo ya Kiboko bali Askari wa Tanapa walimkamata wakati akiwa njiani anaelekea kuvua samaki katika mto Mafunsi.
Kabla ya Hakimu Odira Amwol hajatoa hukumu hiyo, mwendesha mashitaka wa TANAPA Elieza Chitalya aliiomba mahakama hiyo itoe adhabu kwa washitakiwa hao kwa mujibu wa sheria ya kosa walilopatikana nalo ili iwe fundisho kwa jamii nyingine .
Kabla ya kutoa adhabu kwa washitakiwa Hakimu Amwol aliwapa nafasi washitakiwa na aliwaeleza kama wanayo sababu yoyote ya msingi ya kuishawishi mahakama iwapunguzie adhabu wanayo nafasi ya kujitetea .
Katika ombi lake la mshitakiwa wa kwanza aliomba mahakama imwachie huru kwani yeye hakutenda kosa hilo bali alisingiziwa tu na askari wa Tanapa hata majirani zake wanajua yeye hana tabia hiyo .
Mshitakiwa wa pili aliiomba Mahakama isimpe dhabu ya kifungo bali impe adhabu ya kulipa faini kwani kuna familia ambayo inamtegemea yeye ambao ni mama yake mzaz ambaye ni mzee sana pia ana watoto .
Baada ya Mahakama kusikiliza pande zote mbili za mashitaka na utetezi Hakimu Mkazi Odira Amwol alisoma hukumu na kuiambia mahakama kuwa washitakiwa wote wawili mahakama imewahukumu kutumikia kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja kuanzia jana na kama hawajaridhika na hukumu hiyo wanayo nafasi ya kukata rufaa.
Na Walter Mguluchuma-Malunde1 blog Katavi
Social Plugin