Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU ATOA MUDA WA SIKU 10 KWA TAASISI YA HIFADHI YA BAHARI KULIPA DENI LA MIL 100

WAZIRI MKUU  Mhe. Kassim Majaliwa ametoa muda wa siku 10 kwa Taasisi ya Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu kulipa deni la sh. milioni 100 inayodaiwa na Halmashauri ya wilaya ya Mafia.
 
Deni hilo linatokana na malimbikizo ya miaka mitatu ya maduhuri yatokanayo na makusanyo yanayofanywa na taasisi hiyo katika maeneo ya hifadhi ya bahari wilayani humo.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo Ijumaa, Septemba 23, 2016 wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya wilaya hiyo katika ukumbi Caltas akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake ya kikazi siku mbili.
 
“Waandikieni barua na muitume leo hii kwa njia ya mtandao (email) kuwajulisha kuwa wanatakiwa kulipa deni hilo ndani ya siku 10. Hakikisheni wanalipa deni hili ili Halmashauri iweze kufanya kazi zake vizuri,” amesema.
 
Waziri Mkuu amesema Serikali inataka kuona Halmashauri hiyo ikinufaika kutokana na vyanzo vyake vya mapato, hivyo haitakuwa tayari kuona ikihangaika.
 
Mbali na agizo hilo, Waziri Mkuun amesema atafuatilia kuona wajibu wa taasisi hiyo na mipaka yao ikiwa ni pamoja na kujua mapato yatokanayo na shughuli hizo katika maeneo ya hifadhi.
 
Awali mkuu wa wilaya ya Mafia Shaib Nnunduma alisema kuwa miongoni mwa changamoto zinazoikabili wilaya hiyo ni kutolipwa kwa wakati fedha za maduhuri yatokanayo na makusanyo yanayofanywa na Taasisi ya Hifadhi ya Bahari.
 
Mkuu huyo wa wilaya ameiomba Serikali kuangalia upya majukumu ya taasisi hiyo na nafasi ya halmashauri katika kuendesha shughuli za uwekezaji pamoja na kupata mapato yatokanayo na shughuli hizo katika maeneo ya hifadhi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com