WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amefanya ziara ya kukagua ujenzi wa makazi mapya
ya Waziri Mkuu katika eneo la Mlimwa na kuagiza umalizike kwa wakati ili
aweze kuhamia kama alivyoahidi.
Katika ziara hiyo aliyoifanya jana mchana (Jumatano, Septemba 7, 2016) Waziri Mkuu alisema ameridhishwa na namna kazi ya ujenzi inavyofanyika.
“Nimekuja
kukagua makazi mapya na mahali pa kufanyia kazi. Kazi ya ujenzi
inaendelea vizuri, nimejionea mwenyewe na naamini katika kipindi kifupi
watakuwa wamekamilisha,” alisema.
Alisema
kutokamilika kwa ujenzi huo hauwezi kukwamisha azma yake ya kuhamia
Dodoma kwa sababu tayari inafahamika kuwa Makao Makuu ya Ofisi ya Waziri
Mkuu yako Dodoma.
Alisema
uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma hautokani na shinikizo la kisiasa
bali ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao chimbuko
lake ni agizo lililotolewa Oktoba Mosi, 1973 kwenye Mkutano Mkuu wa 16
wa chama cha TANU.
“Tangu
wakati huo Serikali zote ziliendelea kufanya juhudi mbalimbali za
kuandaa miundombinu na hata awamu ya nne ilisimamia kwa kiwango kikubwa
uwekaji wa miundombinu hiyo,” alisema.
“Pia
tukumbuke kauli ya Mheshimiwa Rais aliyotoa kwenye hotuba yake ya Julai
23, 2016 alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM, na akairudia tena
Julai 25, kwenye maadhimisho ya kumbukumbu ya Mashujaa na mimi siku hiyo
hiyo nikaweka msisitizo,” alisema.
Alisema
uamuzi wa Serikali ya awamu ya tano wa kuhamia Dodoma unakuja baada ya
kuridhishwa na ujenzi wa miundombinu na maeneo ya kutolea huduma za
kijamii kwa wageni na wenyeji ikiwemo Hospitali ya Benjamini Mkapa
iliyopo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) yenye uwezo wa kutibu
magonjwa makubwa kama ya moyo na figo.
Waziri
Mkuu alisema tayari Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA) ina
mpango kamambe (master plan) na ina viwanja vya kutosha kujenga makazi
na ofisi mbalimbali.
IMETOLEWA NA:
Social Plugin