YAH: MSIMAMO NA USHAURI WA MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA KUHUSU UONGOZI WA KITAIFA WA CHAMA CHA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF)
Tafadhali
husika na somo hapo juu pamoja na barua yako ya tarehe 23 Septemba 2016
yenye Kumb Na. HA.322/362/14/85 kuhusu somo tajwa.
Baraza
Kuu la Uongozi la The Civic United Front (CUF) – Chama Cha Wananchi,
kupitia Ofisi ya Katibu Mkuu wa Chama, limepokea barua yako tajwa hapo
juu pamoja na taarifa fupi inayoainisha msimamo na ushauri wa Msajili wa
Vyama vya Siasa kwa Chama cha The Civic United Front (CUF) na kuijadili
kwa kina. Yafuatayo ni majibu na msimamo wa Baraza Kuu la Uongozi la
Taifa la CUF ambayo tunapenda kuyawasilisha ili ofisi yako iyafanyie
kazi.
Awali
ya yote, tunakupongeza kwa namna ulivyofuatilia kwa kina, kupitia
wadhifa wako kama Msajili wa Vyama Vya Siasa Tanzania, malalamiko
yaliyowasilishwa kwako na watu uliowatambua kwenye taarifa yako fupi.
Aidha,
tumebaini kuwa ofisi yako imejikita katika kutoa tafsiri ya Katiba ya
Chama cha The Civic United Front (CUF) toleo la mwaka 2014 pamoja na
tafsiri ya matukio na maamuzi ya vikao vya Chama kwa mujibu wa ufahamu
wako.
Pili,
tumebaini kuwa ofisi ya Msajili wa Vyama vya siasa haina mamlaka ya
kisheria kutoa “Msimamo na Muongozo” kwa chama cha siasa kilichosajiliwa
nchini Tanzania.
Majukumu
ya ofisi yako kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha ofisi yako, Sheria ya
Vyama Vya Siasa Sura ya 258, haikupi mamlaka ya kutoa msimamo na
Muongozo.
Badala
yake, unapewa mamlaka ya kuhifadhi kumbukumbu na taarifa za vyama vya
siasa. Majibu haya yanatokana na ukweli kuwa ofisi yako imewahi kuonywa
na Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam katika shauri la Madai Na. 6
la mwaka 2003 baina ya Emmanuel Nyenyemela and Another Versus Registrar
of Political Parties and Others mbele ya Mheshimiwa Jaji Mihayo.
Mahakama ilieleza kama ifuatavyo kwenye ukurasa wa pili wa hukumu:
“In
the same vein, I do not see anywhere in the Political Parties Act where
the Registrar has power to bless or condemn meetings of political
parties or decisions that they make”. (Katika Muktadha huo huo sioni
mahali popote kwenye Sheria ya Vyama vya Siasa ambapo Msajili wa Vyama
ana mamlaka ya kubariki au kupinga vikao vya vyama vya suasa au maamuzi
yanayofanywa na vikao hivyo).
Tunapenda
utambue kuwa uamuzi na muongozo huo wa Mahakama Kuu ya Tanzania
haukuwahi kutenguliwa na Mahakama yoyote ile na hivyo tunaamini wewe
ukiwa na weledi katika taaluma ya sheria na Jaji wa Mahakama kuu,
unafahamu uamuzi huo na namna ya kuutumia.
Tatu,
pamoja na kubaini yaliyomo kwenye aya zilizotangulia hapo juu,
tunapenda upokee majibu yetu kuhusiana na kila kipengele ulichoongelea
kwenye Taarifa yako fupi kama ifuatavyo:
1. MAMLAKA NA WAJIBU WA MSAJILI KUSHUGHULIKIA MGOGORO HUU
Baraza
Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF linasikitika na
upotoshaji wa makusudi uliofanywa na ofisi yako kuhusu tafsiri ya
vifungu vya Sheria ya Vyama Vya siasa, Sura ya 258 ulivyovitaja katika
ukurasa wa pili wa Taarifa yako fupi ili kujipa mamlaka ya kushughulikia
kile ulichokiita mgogoro wa Uongozi katika Chama chetu.
Tunapenda urejee vifungu ulivyotumia ambavyo tunavichapisha tena hapa chini:
Kifungu
cha “8A (1) There shall be a Registrar of Political Parties into which
names, addresses, and other particulars of Registered Political Parties
or national leaders of Political Parties shall be entered.” (Kutakuwa na
Msajili wa Vyama vya Siasa ambako majina, anwani na taarifa zingine za
Vyama vya Siasa vilivyosajiliwa au viongozi wa kitaifa wa vyama vya
siasa zitawekwa).
Kifungu
cha 10(f) “No Political Party shall be qualified to be fully registered
unless …..(a)…….(e) (Hakuna Chama cha siasa kitakachofaulu kupewa
usajili wa kudumu hadi……)
(f)
it has submitted the names of the national leadership of the party and
such leadership draws its members from both Tanzania Zanzibar and
Mainland Tanzania, and” (kiwe kimewasilisha majina ya uongozi wa kitaifa
na uongozi wa chama hicho uundwe na wanachama kutoka Tanzania Zanzibar
na Tanzania Bara, na)
Ukivisoma
vifungu hivyo hapo juu, katika sheria tajwa, utabaini kuwa havina
kabisa uhusiano na kukupa wewe mamlaka au wajibu wa kuchunguza na
kujiridhisha kuhusu usahihi wa mabadiliko katika uongozi wa Kitaifa wa
Chama na ama kutengua au kubariki maamuzi halali ya vikao halali vya
chama chochote. Zingatia pia hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania ambayo
tayari tumeitaja hapo juu. Tumejiridhisha kuwa mamlaka uliyojitwisha
hayakuwa yako na pia hukuyatenda kwa kuzingatia misingi ya haki.
2. KUJIUZULU KWA PROFESA IBRAHIM LIPUMBA NA KUTENGUA BARUA YAKE YA KUJIUZULU
Baraza
Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF linatambua kuwa
Chama cha The Civic United Front (CUF) kinaongozwa na Katiba yake
halali, toleo la mwaka 2014. Tunapenda utambue kuwa kujiuzulu kwa
kiongozi ni wakati wowote kwa mujibu wa Ibara ya 117(1). Kuhusu
utaratibu uliowekwa na ibara ya 117(2) hauathiri haki ya kiongozi
kujiuzulu wakati wowote.
Prof.
Ibrahim Haruna Lipumba aliandika barua ya kujiuzulu nafasi ya
Mwenyekiti wa CUF Taifa kuanzia tarehe 5/08/2015 ambayo ni siku
aliyoandika barua hiyo na aliutangaza uamuzi wake huo mbele ya vyombo
vya habari tarehe 6/8/2015.
Katika Barua yake ya kung’atuka wadhifa wa Mwenyekiti wa Taifa wa CUF ilisema ;
”Leo
tarehe 5 Agosti 2015 najiuzulu rasmi nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa wa
CUF. Naendelea kuwa Mwanachama na kadi yangu nimeilipia mpaka 2020.”
Prof.
Lipumba alitekeleza kujiuzulu kwake bila kusubiri kukubaliwa na Mkutano
Mkuu wa Chama kwa mujibu wa Ibara 117(2) ya Katiba ya Chama. Prof.
Lipumba alikua na mamlaka ya kuhakikisha kuwa Mkutano Mkuu unaitishwa
ili kukubali kujiuzulu kwake lakini hakufanya hivyo.
Kama
ulivyoeleza katika taarifa yako, Katiba ya CUF inatambua haki ya
kujiuzulu uongozi lakini haizungumzii kutengua uamuzi wa kujiuzulu. Prof
Lipumba asingeweza kutengua uamuzi wake wa kujiuzulu kwa sababu
alishautekeleza. Na aliacha ofisi na majukumu ya Mwenyekiti wa Taifa wa
CUF kwa mujibu wa Ibara ya 91 ya Katiba ya Chama kwa zaidi ya miezi
kumi. Kuna msemo “you can not eat a cake and have it.”
Kwa
hiyo suala la Prof. Ibrahim Haruna Lipumba kurudi kwenye nafasi ya
Mwenyekiti wa CUF Taifa baada ya zaidi ya miezi kumi ni wazo chelewefu
(afterthought) na ndiyo maana amekua akiitika wito wa Baraza Kuu la
Uongozi la Taifa kama Mwalikwa kutoa maoni juu ya mambo mbalimbali.
3) BAADHI YA WAJUMBE WA MKUTANO MKUU MAALUM KUHITAJI PROFESA LIPUMBA AITWE KATIKA CHUMBA CHA MKUTANO KUJIELEZA.
Baraza
Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF limesikitishwa
kwamba hujajielekeza kabisa juu ya namna Prof. Lipumba alivyovamia
Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa tarehe 21/08/2016 akiwa na genge la
wahuni ambao sio wajumbe wala waalikwa wa mkutano huo (kama yeye) na
wahuni hao wakiwa na silaha mbalimbali na kwa hiyo tunachukulia kwamba
unaunga mkono vitendo hivyo.
Ibara
ya 117(2) ya Katiba ya CUF haitoi fursa kwa kiongozi aliyejiuzulu
kujieleza juu ya kujiuzulu kwake mbele mkutano husika. Hata hivyo,
umuhimu huo haukuwepo kwa sababu chama kiliridhika kwamba ni yeye ndiye
aliyejiuzulu na aliondoka ofisini na akaacha kutekeleza majukumu yake ya
Mwenyekeiti wa CUF Taifa.
Pia
alikabidhi barua yake ya kujiuzulu kwa mkono wake mwenyewe tarehe
05/08/2015 na siku iliyofuata ya tarehe 06/08/2015 aliufahamisha umma
kupitia vyombo vya habari kwamba alijiuzulu na alithibitisha hiyo.
Maelezo ya Profesa Ibrahim Lipumba yalikuwa tayari yanafahamika kwa
wajumbe wengi wa Mkutano na hakukuwa na suala jipya kuhusiana na
kujiuzulu kwake.
Hivyo haukuwa sahihi hata kidogo kusema kuwa Profesa Lipumba alipaswa kujieleza mbele ya Mkutano Mkuu.
Msimamo
wako huo ni kinyume na Katiba ya CUF na hali halisi ilivyokuwa. Mashaka
uliyojijengea kuwa huenda barua iliyosomwa haikuwa yake hayana msingi
wowote maana tangu mwaka 2015 ofisi yako imekuwa ikifanya kazi na Chama
cha CUF kupitia viongozi wengine na ukiwa Mtanzania tunaamini ulipata
taarifa za kujiuzulu kwake kwa njia nyingi. Ofisi yako pia ilipokea
taarifa rasmi kutoka CUF, kwa hiyo inashangaza sana kusikia kuwa hata
ofisi yako haikuwa na taarifa za kujiuzulu kwa Profesa Lipumba.
4). UHALALI WA KURA ZILIZOPIGWA KUKUBALI AU KUKATAA PROFESA LIPUMBA KUJIUZULU.
Baraza
Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF linabaini tafsiri
ya matumizi ya ibara ya 77(8) (d) ya Katiba ya CUF ambayo tunapenda
kuidurusu hapa chini:
“77(8) Kwa madhumuni ya kijifungu cha (7) cha kifungu hiki, maamuzi muhimu ni pamoja na
(d)
kuwasimamisha, kuwaachisha au kuwafukuza uongozi na/ au uanachama
viongozi wakuu wa Kitaifa wa Chama pamoja na viongozi wengine wa Kitaifa
kama ilivyoainishwa ndani ya Katiba hii.”
Kijifungu
hicho hakihitaji tafsiri yoyote na kiko wazi, kwamba matumizi ya
kifungu hiki ni pale ambapo yanajadiliwa masuala ya kuwasimamisha,
kuwaachisha au kuwafukuza uongozi na au uanachama viongozi wakuu wa
Kitaifa wa Chama. Katiba hii haitoi wajibu wala haifanyi suala la
kujiuzulu Kiongozi wa Kitaifa wa Chama kuwa ni jambo muhimu linalohitaji
kupigiwa Kura kwa mujibu wa tafsiri yako. Ikiwa Lipumba angelikuwa
anasimamishwa, anaachishwa au kufukuzwa uongozi au uanachama ndipo
matakwa ya uamuzi muhimu kikatiba yangelifanyika.
Lakini
Profesa Lipumba alijiuzulu mwenyewe, hakusimamishwa, hakuachishwa na
wala hakufukuzwa uanachama au uongozi kwa hiyo Mkutano Mkuu wa CUF
kikatiba hauwezi kushughulikia suala la kujiuzulu kwa kiongozi kama
uamuzi muhimu.
Tambua
pia kuwa Katiba ya CUF ni yetu wenyewe na wewe ni Msajili, tunaifahamu
vyema sisi wanachama na viongozi kuhusu maudhui yake kuliko wewe ambaye
mara zote tunakupa taarifa baada ya maamuzi ya vikao na Katiba hiyo
kuwasilishwa kwako kwa usajili tu. Kujiuzulu kwa Profesa Ibrahim Haruna
Lipumba kulifanyiwa maamuzi kwa mujibu wa Ibara ya 115(1) ya Katiba ya
CUF na siyo ibara ya 77(7).
Kura
zilizotakiwa ni zaidi ya nusu tu na siyo 2/3 (theluthi mbili) na kura
zilizopigwa kubariki kujiuzulu kwake ni 476 ambazo ni asilimia 70 ya
idadi ya wajumbe wote wa Mkutano Mkuu na kwa hiyo maamuzi ya ibara ya
117 (2) yalifanywa kwa uhakika, kikatiba na bila shaka yoyote.
Taarifa
za vurugu wakati wa maamuzi siyo ya kweli. Unatambua kuwa vurugu hizo
zilitokea baada ya ajenda ya kukubali kujiuzulu kwa Profesa Ibrahim
Haruna Lipumba kukubaliwa na ajenda hiyo kufungwa na mkutano kuahirishwa
kwa mapumziko na kwamba baada ya mapumziko na wakati mkutano uko kwenye
ajenda ya pili ndipo vurugu zilitokea.
Hata
hivyo, unatambua kuwa vurugu hizo alizisababisha yeye mwenyewe Prof.
Lipumba alipofahamu maamuzi ya Mkutano na wakati wa Kuchagua Mwenyekiti
mpya wa kujaza nafasi yake iliyoachwa wazi kwa kujiuzulu.
5). UHALALI WA KIKAO CHA BARAZA KUU LA LA UONGOZI LA TAIFA CHA TAREHE 28 AGOSTI 2016.
Baraza
Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF limebaini kuwa
ofisi yako imetambua Kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa cha tarehe
28 Agosti 2016. Hatuna mashaka na mtazamo huu kwani ndiyo ukweli.
6). MAMLAKA YA BARAZA KUU LA UONGOZI KUCHUKUA HATUA ZA KINIDHAMU.
Baraza
Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF halina mashaka na
utambuzi wako wa mamlaka ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kuchukua
hatua za kinidhamu dhidi ya viongozi wa Kitaifa wa Chama.
Tunakushauri kifungu ulichotumia ukisome pamoja na vifungu vingine ambavyo ni Ibara ya 82(1) (m) na 83(1).
7). UTARATIBU WA KUCHUKUA HATUA ZA INIDHAMU.
Baraza
Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF linapenda
kukufahamisha kuwa taarifa ya Kikao cha dharura ilikuwa sahihi na ajenda
ilikuwa inafahamika kwa wajumbe wa Kikao kuwa ni kujadili hujuma. Hata
hivyo, tunakanusha tuhuma kuwa Maamuzi muhimu kwa mujibu wa ibara ya
77(8) na 81(4) hayakufanyika kwa kuzingatia matakwa ya 2/3 ya wajumbe.
Utatambua
kuwa maamuzi yote ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa yanaweza kufanyika
kwa maafikiano au kwa wingi wa kura. Tunakushauri urejee Ibara ya 81 (3)
ya Katiba ya chama ambapo hata maamuzi muhimu yanahusika.
Tafsiri
ya neno “Unanimously” hayamaanishi “Consensus”. Tunajiridhisha kuwa
neno Unanimously kwa muktadha wa Chama chetu ni kuwa wajumbe wote
walipiga kura na hakukuwa na mjumbe aliyepinga. Hatukuwahi kupata
taarifa za mtu yeyote aliyethibitika kuwa alinyimwa fursa ya kupiga
kura. Kama maamuzi yalifanyika unanimously, basi yalifanyika kwa wingi
wa wajumbe zaidi ya 2/3 kila upande. Katiba ilizingatiwa.
8. UTEUZI WA VIONGOZI WA KITAIFA ULIOFANYWA NA BARAZA KUU LA UONGOZI LA TAIFA.
Baraza
Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF linapenda ufahamu
kuwa ibara ya 101 inalipa Baraza Kuu la Uongozi Taifa uwezo wa kuunda
Kamati yoyote na hivyo kujumuisha uwezo wa kuunda Kamati ya Uongozi
ilipoona kuna haja hiyo. Kamati iliyoundwa ni halali kwa ajili ya
utekelezaji mzuri wa sera na itikadi za chama. Majukumu ya Mwenyekiti na
Makamu Mwenyekiti wa Chama Taifa yana lengo la kusaidia utekelezaji
mzuri wa sera na itikadi za Chama, kwa hiyo majukumu ni yale yale na
siyo tofauti.
Kwa
mantiki hiyo, Kamati zote mbili yaani ile ya awali iliyokuwa chini ya
Mwenyekiti Mhe. Wakili msomi Twaha Issa Taslima na hii ya sasa iliyo
chini ya Mhe. Julius Mtatiro zote ni halali kwa mujibu wa katiba ya
Chama. Ofisi yako ilipokea taarifa ya Chama na inayo (ambalo ndilo
jukumu lako) iliyokuwa ikikueleza kuundwa kwa Kamati ya Uongozi ya awali
iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Mhe. Twaha Taslima ambayo hukuhoji
uhalali wake na uliitambua na hata kufanya kazi nayo ilipokuwa
ikiwasiliana na wewe. Haiwezekani uone na utambue uhalali wa Baraza Kuu
la Uongozi la Taifa kuunda Kamati ya Uongozi kwa kipindi cha Agosti 2015
hadi Agosti 2016 lakini usione uhalali wa kuundwa Kamati ya aina hiyo
hiyo iliyoundwa tarehe 28 Agosti, 2016.
9. UHALALI WA UTEUZI WA VIONGOZI WA KITAIFA ULIOFANYWA NA KIKAO CHA BARAZA KUU LA TAREHE 28 AGOSTI 2026.
Baraza
Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF linapenda
kusisitiza kuwa uteuzi ulikuwa halali kama tulivyoeleza hapo juu. Kama
ulivyoeleza wewe, utabaini kuwa mamlaka ya uteuzi wa viongozi wa Kitaifa
ni Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na ndicho kilichofanyika na ambacho
ni msimamo wa Chama. Na hiyo ina maana kuwa msimamo wa Baraza Kuu la
Uongozi la Taifa la CUF ni kuwa Ndugu. Julius Mtatiro, Ndugu. Severina
Mwijage na Ndugu. Katani Katani ndiyo wajumbe wa kamati hiyo ya uongozi
na wanatambulika kikatiba katika chama chetu kama Wajumbe wa Kamati ya
Uongozi hadi hapo chama kitakapochagua Mwenyekiti mwingine.
10). HITIMISHO
Baraza
Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF limejiridhisha
kuwa katika taarifa yako fupi umeweka hitimisho ambalo linatoa hukumu
(judgment) badala ya kushauri au kutoa taarifa kama ulivyoitaja.
Kama
tulivyokwisha kueleza kwenye utangulizi wa barua yetu na kwa kuzingatia
Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258 toleo la mwaka 2015 na kwa
kuzingatia hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam, mbele ya
Mhe. Jaji Mihayo ambayo tunaiambatanisha na barua hii kwa taarifa,
tafadhali tambua kwamba hukumu yako ni batili na haina mashiko kisheria.
Kwa
yale ambayo umetoa ushauri kwa mujibu wa Katiba ya Chama chetu, Chama
kina hiyari ya kuukubali au kuukataa ushauri huo kwa kuzingatia misingi
ya Katiba yake, Kanuni zake na kuhakikisha haki sawa kwa wote inatendeka
wakati wote.
Baraza
Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF linasisitiza kuwa
maamuzi yaliyofanywa na vikao halali vya Chama vya Mkutano Mkuu Maalum
wa tarehe 21/08/2016 na Baraza Kuu la Uongozi la Chama Taifa la tarehe
28/08/2016 ni halali na tunakusihi uyatambue hivyo.
Tunakukumbusha
na kukukusihi usiruhusu Ofisi yako itumike vibaya kutuletea mitafaruku
na migogoro isiyo ya lazima katika Chama chetu na hata kusababisha
uvunjifu wa amani kama ilivyotokea Jumamosi, tarehe 24 Septemba, 2016
katika Ofisi Kuu ya chama chetu Buguruni Dar Es Salaam. Ushauri huu
unazingatia ukweli kuwa Msajili wa Vyama Vya Siasa Tanzania ni mteule wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni mwenyekiti wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) Taifa. Nguvu ya Chama cha CUF Tanzania inafahamika
na hasa katika ushiriki wake na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Rais,
Wabunge na Madiwani mwaka 2015.
Matukio
yaliyojitokeza Zanzibar na siasa za nchi hii ni lazima yazingatiwe
wakati ukitekeleza majukumu yako ili kuepuka kutumiwa vibaya na watu
walioshiriki kuhujumu chama chetu na demokrasia wakati wa uchaguzi mkuu
wa 2015 na marudio yake 2016 kwa Zanzibar. Taarifa tulizo nazo za
malengo ya Profesa Lipumba kuhujumu siasa za Chama Cha Civic United
Front (CUF) na mahusiano ya Chama na taasisi nyingine zinajidhihirisha
katika matukio yaliyofanywa na Profesa Lipumba tarehe 21 Agosti 2016
(Ubungo Plaza, Dar Es Salaam – kwenye Mkutano Mkuu Maalum) na tarehe 24
Septemba 2016 (wakati akitekeleza kwa nguvu kile anachokiita
“kurudishiwa uenyekiti wake na Msajili) baada ya barua yako tajwa.
Mwisho,
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front CUF
haliukubali ushauri wako kwa sababu umevuka mipaka ya mamlaka yako
uliyokabidhiwa na Sheria namba 5 ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992,
imekiuka miongozo ya mhimili wa Mahakama ambayo imekwishatolewa juu ya
mamlaka yako na unakiuka misingi ya katiba ambayo inamtaka kila mtu
aliyepewa mamlaka katika nchi yetu azingatie sheria za nchi.
Kwa
sababu hiyo Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la The Civic United Front
CUF linakujulisha rasmi kuwa, maamuzi ya vikao halali vya chama kwa
maana ya Mkutano Mkuu wa Taifa tarehe 21 Agosti 2016 na Baraza Kuu la
Uongozi la Taifa la tarehe 28 Agosti 2016 yanabakia pale pale na kwamba
Profesa Lipumba siyo Mwenyekiti wa The Civic United Front CUF Chama Cha
Wananchi na kuwa, wanachama na viongozi wote waliosimamishwa na ama
kufukuzwa katika kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa cha tarehe 28
Agosti 2016 wanaendelea kuwa chini ya maamuzi hayo hadi pale mchakato wa
kikatiba wa kuwasikiliza (kwa waliosimamishwa) utakapokamilika.
Hatua
yoyote ile ya kutengua maamuzi yoyote ya vikao halali vya chama chetu
itafanywa na vikao husika vya chama au vikao vya juu yake kama ambavyo
katiba yetu imeelekeza na kwamba hatutakubali Ofisi yako kutuamulia nani
anapaswa kuongoza chama chetu kwa wakati gani ama tujiongoze katika
chama chetu kwa namna gani.
Tunawasilisha.
HAKI SAWA KWA WOTE
…………………………………..
MAALIM SEIF SHARIF HAMAD
KATIBU MKUU
NAKALA;
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba
Kilongawima, Kunduchi,
Dar es Salaam.
Bwana Ridhiwani H. Kilala na Wenzako wawili
Bwana Abdul Kambaya na Shashu Lugeye.