Nimeipata taarifa ya Benki ya Dunia kuhusu kupungua kwa idadi kubwa ya watu masikini duniani licha ya ongezeko la idadi ya watu ulimwenguni.
Kwa mujibu wa Benki ya Dunia ripoti inasema kuwa, idadi ya watu masikini sana imepungua kwa zaidi ya watu milioni 100 licha ya kwamba uchumi wa dunia unakuwa kwa kusua sua.
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni kutoka Benki ya Dunia, mwaka 2013 karibu watu milioni 767 walikuwa wanaishi kwa pato la dola 1.90 kwa siku wakati mwaka 2012 idadi ya watu masikini sana ilikuwa ni milioni 881 kote ulimwenguni.
Ripoti hiyo pia imeonesha kuwa, mwaka 2013 idadi ya watu masikini zaidi ilipungua kwa karibu watu bilioni moja na milioni mia moja ikilinganishwa na mwaka 1990 licha ya idadi ya watu kuongezeka duniani huku ikieleza kuongezeka kwa misaada kwa watu masikini duniani.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa, dunia imekaribia kufikia malengo yaliyokusudiwa na Umoja wa Mataifa ya kupunguza umaskini kwa kiwango kikubwa ifikapo mwaka 2030.