Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BIASHARA YA NGONO YASHAMIRI MJI WA DAR- PORI MPAKANI MWA MSUMBIJI NA TANZANIA

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dk Binilith Mahenge akiangalia jiwe linalotambulisha mpaka eneo la dar-Pori wilayani Nyasa wakati alipokuwa na ziara eneo hilo kukutana na wananchi wa mpakani. ( Na Mpigapicha Maalumu)
WANANCHI wanaoishi mpakani mwa Msumbiji na Tanzania wameiomba serikali kukomesha biashara ya ngono kwa watoto chini ya miaka 18 katika mji wa machimbo wa Dar Pori.


Walitoa ombi hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika mpaka wa Msumbiji na Tanzania katika kata ya Unyere, Tarafa ya Mpepo uliohudhuriwa na viongozi wa Msumbiji na Tanzania.

Katika mkutano huo Mkuu wa Mkoa Ruvuma, Dk Binilith Mahenge alikuwa mgeni rasmi. Wazazi hao walizitaka serikali za pande zote mbili kudhibiti mpaka na kuwakemea watu wanaowaingiza watoto walio chini ya miaka 18 katika biashara ya ngono.

Mzazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Mohamed alisema wao wakiwa kama wazazi wanaona huruma kwa watoto walio chini ya miaka 18 wakifanya kazi za ngono ili waweze kujikimu kimaisha.

“Watoto hawa wanachukuliwa wakidaiwa wanakwenda kufanya kazi za majumbani, kumbe wanaenda kufanya kazi za baa kwa malipo ya mlo mmoja , mlo mwingine wajitafutie na mtu akifika dau anamlipa anayewahifadhi,” alisema mzazi huyo na kuongeza kwamba mwenye baa analipwa kati ya shilingi 20,000 na Sh 50,000 kutegemea urembo wa binti mhusika.

Dar-Pori, mji uliochipuka kutokana na kuwapo kwa machimbo ya dhahabu unasifika kwa ngono toto kama sehemu ya burudani baada ya kazi nzito.

Aidha biashara hiyo inafanyika upande wa pili wa mpaka ambapo wasichana hao wadogo huvuka kwa maelezo kwamba wanakwenda kutembelea ndugu zao na kuishia katika madanguro yanayohifadhi watu kuanzia 10 hadi 20.

Kwa sasa dhahabu inapatikana kwa wingi upande wa pili na kufanya kuwapo na machimbo manne yanayotumika kutafuta dhahabu huku wachimbaji wake wakiwa ama Tura au Dar–Pori.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dk Binilith Mahenge akijibu hoja hizo alisema biashara ya kusafirisha binadamu ni kinyume cha sheria na kwamba mtu atakayekamatwa atafikishwa mahakamani.

Aidha alipiga marufuku biashara hiyo ya kusafirisha watoto ambao wanatumbukizwa katika kumbi zao za starehe ili kuwafanya kivutio na chambo ili kufanikisha biashara zao. Aliwataka viongozi wa vijiji, watendaji pamoja na wananchi wa kawaida kuingia katika vita ya kupambana na biashara hiyo haramu ya kusafirisha watoto kwa madhumuni ya kuwatumbukiza katika biashara ya ngono.

Viongozi wa Msumbiji wakiongozwa na Mwenyekiti wa Wachimbaji Msumbiji, Alexanda Ndekiso walimuahidi Mkuu wa mkoa wa Ruvuma kuwa watakomesha biashara hiyo na kuwarudisha watoto walio chini ya miaka 18 ambao wanatumika kwenye biashara hiyo.

Walisema watafanya kila njia kuhakikisha watoto wanaohitajika kuwa shuleni wanarudishwa Tanzania ili waweze kushiriki masomo, jambo lililoungwa mkono na mkuu wa askari wa mpakani Komezi Amanzi.

Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com