Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema ni uongo na ni
propaganda za wapinzani wao kwamba Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa
alimhonga Mwenyekiti Freeman Mbowe ili kupata nafasi ya kugombea urais
mwaka 2015.
Dkt.
Mashinji ameyasema hayo katika kipindi cha Kikaangoni kinachorushwa na
kituo cha EATV kupitia ukurasa wa facebook ambapo wananchi walikuwa
wakimuuliza maswali ya papo kwa papo naye anayajibu.
“Si
kweli kwamba Mwenyekiti Freeman Mbowe alimhonga Lowassa ili agombee
urais kupitia CHADEMA , ni propaganda zinazoenezwa na wapinzani wetu ili
kuwadanganya wananchi” Amesema Dkt. Mashinji.
Amesema
Lowassa alijiunga na CHADEMA kwa njia halali kwa mujibu wa taratibu za
chama, na maamuzi ya kumteua kugombea urais yalifanywa na vikao halali
kuanzia ngazi ya Kamati Kuu hadi Mkutano Mkuu.
Kuhusu
sababu za CHADEMA kumkaribisha Lowassa licha ya kumtaja miaka mingi
kuwa alihusika na ufisadi, Dkt Mashinji, hakutaka kulifafanua kwa
undani, lakini aliishia kusema kuwa wao walijiridhisha kuwa hakuwa na
hatia yoyote na kwamba kama kweli alikuwa ni fisadi, basi vyombo vya
dola vingemchukulia hatua.
"Kama mtu kweli alikuwa ni fisadi, kwanini hakuwahi kuchukuliwa hatua, hata kufikishwa mahakamani?, nadhani hilo tuliache" Alisema kwa ufupi Dkt Mashinji.
Aidha
Dkt. Mashinji amewataka watanzania na wapenzi wa CHADEMA kufahamu
kwamba chama hicho hakipo kimya bali kinaendelea na mikakati ya
kuhakikisha kwamba kinawafikia watanzania kwa kuwatetea kwa kila hali
kutokana na mambo yanayoendelea nchini.