Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM CHATIMIZA MIAKA 55, JK ATAKA KIENDELEE KUWA CHUO KIONGOZI TANZANIA


Rais Mstaafu wa awamu ya nne ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na washiriki wa kongamano la kuadhimisha miaka 55 toka kuanzishwa kwa Chuo Kikuu hicho mapema hii leo Oktoba 24,2016 Chuo Kikuu jijini Dar es Salaam.

Mhadhiri wa Heshima Prof. Tade Aina toka nchini Nigeria akielezea hali ya vyuo vikuu vya Afrika katika muktadha wa Kimataifa wakati wa kongamano la kuadhimisha miaka 55 toka kuanzishwa kwa Chuo Kikuu hicho.
Baadhi ya washiriki wa kongamano maalum la kuadhimisha miaka 55 toka kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakimsikiliza kwa makini Mhadhiri wa Heshima Prof. Tade Aina kutoka nchini Nigeria wakati akielezea hali ya vyuo vikuu vya Afrika katika muktadha wa Kimataifa .
Rais Mstaafu wa awamu ya nne ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (kulia) akifurahia jambo na Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba (kushoto) wakati wa kongamano la kuadhimisha miaka 55 toka kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, katikati ni Mhadhiri wa Heshima Prof. Tade Aina toka nchini Nigeria.
Rais Mstaafu wa awamu ya nne ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Wakuu wa Vitivo wa Chuo hicho wakati wa kongamano la kusherehekea kutimiza miaka 55 toka kuanzishwa kwa chuo hicho.
Picha na Eliphace Marwa – Maelezo

*******

UONGOZI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) takiwa kuhakikisha Chuo hicho kinaendelea kuwa kiongozi miongoni mwa vyuo vikuu nchini.

Ushauri huo umetolewa na rais mstaafu wa awamu ya nne ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alipokuwa akifungua maadhimisho ya miaka 55 ya chuo hicho leo Jijini Dar es Salaam.

“Hiki ndicho chuo kiongozi kati ya vyuo vikuu vyote hapa nchini, mnatakiwa kuhakikisha kinaendelea kuwa kiongozi huku Vyuo vingine vikifuatia”, alisema Dkt. Kikwete

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Lwekaza Mukandara alisema pamoja na changamoto zinazokikabili chuo hicho wanaishukuru serikali kwa kuendelea kusaidia katika kuleta maendeleo ya chuo hicho.

Alisema baadhi ya changamoto zimetatuliwa kwa pamoja kati ya serikali na wahisani ambapo alieleza kuwa ujenzi wa kumbi mpya za mihadhara, maabara za kisasa na jengo la malazi,pamoja na ujenzi wa hosteli za wanafunzi unaoendelea katika kampasi ya Julius K. Nyerere ambayo itakuwa na uwezo wa kutumiwa na wanafunzi 4000 mara itakapo kamilika.

Akiwasilisha mada juu ya “Hali ya Taaluma Barani Afrika Katika Muktadha wa Kimataifa” Mhadhiri wa Heshima kutoka nchini Nigeria, Profesa Tade Aina alisema Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni moja kati ya vyuo vikuu mahiri barani Afrika ambapo kimetoa mchango mkubwa kwa ukombozi wa nchi nyingi za bara hili.

Aliongeza kuwa yeye binafsi ni mnufaika mkubwa wa UDSM kwani amekuwa na ushirikiano mkubwa na baadhi ya wahadhiri kutoka chuo hicho katika masuala mbalimbali ya taaluma.

Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba ambaye pia alikuwa mwenyekiti wakati wa uwasilishaji mada alisema  kipindi chuo hicho kinaanzishwa aina ya masomo yaliyokuwa yanafundishwa chuoni hapo yalikuwa na muelekeo kuandaa wafanyakazi wa serikali kwa wakati huo.

Aliongeza  kuwa muelekeo wa aina ya masomo uliendelea kubadilika kadri ya siku zilivyokwenda kutokana na mabadiliko ya teknolojia na uhitaji wa soko la ajira.

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinaadhimisha miaka 55 tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1961 kikiwa ni tawi la Chuo Kikuu cha London, ambapo awali kilianzia katika mtaa wa Lumumba jijini Dar es salaam kikiwa na wanafunzi 14 kabla ya kujengwa mahali kilipo sasa katika eneo la Mlimani.
 Habari na Frank Shija, MAELEZO.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com