Mahakama
ya Wilaya ya Ilala imemhukumu Seleman Manoti, kifungo cha miaka miwili
jela kwa kupatikana na hatia ya kujifanya usalama wa Taifa.
Hata
hivyo, mahakama imetoa hukumu hiyo bila mshitakiwa kuwepo mahakamani
kutokana na kuruka dhamana kesi hiyo ilipokuwa inasikilizwa.
Akitoa
hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi, Flora Haule alisema kuwa upande wa
mashitaka, ulileta mashahidi wanne kwa ajili ya kuthibitisha tuhuma
hizo.
Alisema
kutokana na ushahidi uliotolewa, mahakama imeridhishwa na ushahidi huo
na kwamba mahakama inamtia hatiani mshitakiwa licha ya yeye kutokuwepo.
“Hati
ya kumkamata mshitakiwa itolewe na adhabu hii itaanza kutumika pindi
mshitakiwa atakapokamatwa kwani alitoroka akiwa na haki ya kusikilizwa,” alisema Hakimu Haule.
Wakili wa Serikali, Ester Kyara aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa iwe fundisho kwa wengine.
Inadaiwa
kuwa Novemba 19, 2014 maeneo ya Kariakoo Msimbazi wilayani Ilala,
mshitakiwa alijitambulisha kwa Issaya Odelo na Charles Odinga kuwa Ofisa
Usalama wa Taifa, kitu ambacho alijua si kweli.
Katika
hatua nyingine, kondakta Ally Salum (23), mkazi wa Mwananyamala,
amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia
ya kuiba daladala.
Mbali
na mshitakiwa huyo, Exavery Kaunga (44) ambaye ni mlinzi na mkazi wa
Kiwalani, Minazi Mirefu, aliachiwa baada ya ushahidi dhidi yake kuwa na
shaka.
Akitoa
hukumu hiyo jana katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Hakimu Mkazi
Mwandamizi, Juma Hassan, alisema kuwa upande wa mashitaka ulileta
mashahidi wanne kuthibitisha kosa hilo.
“Nimeridhika
na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka, nakutia hatiani
mshitakiwa kama ulivyoshitakiwa kwa kutumikia kifungo cha miaka mitano
jela,” alisema Hakimu Hassan.
Kabla
ya kutolewa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Grace Mwanga aliiomba
mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwa wengine.
Hata hivyo, mshitakiwa alipoulizwa ni kwa nini asipewe adhabu kali,
hakujibu chochote na mahakama kutoa adhabu hiyo.
Washitakiwa
hao walishitakiwa kwa makosa mawili ya kula njama kutenda kosa ambapo
inadaiwa kati ya Julai 5, mwaka jana, washitakiwa walikula njama kutenda
kosa.
Pia
inadaiwa Julai 5,2015 pembezoni mwa barabara ya Nyerere katika Kituo
cha Mafuta cha Victoria, washitakiwa waliiba gari lenye namba za usajili
T 624 CSH aina ya Eicher mali ya Kampuni ya White Swan.