Kama mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema anapambana na Mrisho Gambo ili kujijenga kwa wananchi wake, basi mkuu huyo wa mkoa ananufaika na vita hiyo na anatarajia makubwa zaidi baada ya mzozo wa mwanzoni mwa wiki.
Wakati Gambo akitarajia kupandishwa cheo na Rais John Magufuli, madiwani wa jiji hilo wametangaza kususia vikao vyote hadi viongozi wa juu wa Serikali watakapoingilia kati mgogoro uliopo.
Wawili hao waliingia kwenye mzozo mwingine mapema wiki hii wakati Gambo alipoalikwa kuzindua ujenzi wa hospitali ya mama na mtoto, itakayojengwa kwa ufad kwa ufadhili wa taasisi ya Martenity Africa alipojaribu kueleza historia ya kiwanja cha jengo hilo, maelezo ambayo Lema aliyapinga kwa sauti kubwa na kusababisha shughuli hiyo kuvurugika.
Baada ya mzozo huo, Gambo amedokeza kuwa kuna makubwa yanafuata.
“Baada ya hilo, simu zilikuja kibao, lakini bahati nzuri kabla sijauliza kokote, na Mheshimiwa Rais ndio akawa ananipigia akaniambia nina full confidence (nina imani) na wewe. Labda wafikirie promotion (kupandisha cheo), lakini hayo mengine hayapo,” alisema Gambo akiwaeleza wafanyabiashara wa mjini hapa kuhusu barua iliyosambaa juzi kwenye mitandao ya kijamii kuwa Rais ametengua uteuzi wake.
“Baadaye (Rais) akaniambia kwamba sasa ili (wafanyabiashara) wajue kwamba kweli nimekupigia simu, niitie mmoja uliye naye karibu ili niongee naye. Ndio (mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Arusha) akapata previledge (bahati) naye ya kuongea na Mheshimiwa Rais.”
Iwapo Gambo atapandishwa cheo, ambacho kwa mukhtadha wa utumishi wa umma chaweza kuwa ni kuteuliwa kuwa mbunge na baadaye waziri, itakuwa ni mara ya pili kupanda cheo siku chache baada ya kuzozana na Lema.
Gambo, ambaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha Juni 26, alilumbana na Lema Agosti Mosi mbele na Naibu Waziri wa Tamisemi, Suleiman Jafo.
Katika tukio hilo, Lema alisema Gambo haheshimu mipaka ya kazi zake, akimtuhumu kuingilia maamuzi ambayo tayari yameshajadiliwa kwenye vikao halali vya halmashauri na kupitishwa na ofisi ya mkuu wa mkoa katika kikao cha wakuu wa idara, maofisa tarafa, waratibu wa elimu kata watumishi wa Mamlaka ya Maji Safi na Mazingira (Auwsa) jijini hapa.
“Nimeona nizungumze hapahapa ili naibu waziri ufahamu hali ilivyo hapa. Kwa mfano Baraza la Madiwani la mwaka 2008, ndilo lililopitisha kiwango cha posho kwa madiwani kutoka Sh100,000 hadi 120,000. Jambo la kushangaza DC ameandika barua Tamisemi na nakala kwa Takukuru ili wachunguze jambo ambalo limeshapata baraka za Tamisemi,” alisema Lema.
Hali hiyo ilimfanya naibu waziri kuingilia kati na kuahidi kuzishughulikia changamoto hizo na kumpa nafasi Gambo, ambaye wakati huo alikuwa mkuu wa wilaya, kujibu hoja hizo.
“Mheshimiwa mbunge nataka ujue mimi ndiyo mkuu wa shughuli za Serikali hapa wilayani. Muda wowote nina uwezo wa kuingilia kati mambo ambayo naona hayaendi sawa, hata kama yupo katibu tawala na viongozi wengine,” alisema Gambo.
“Rais aliona ninafaa ndiyo maana akaniteua na sihitaji kujifunza namna ya kuwa mkuu wa wilaya kwa kuwa huu ni mwaka tano.”
Malumbano hayo yaliendelea na kumuhusisha pia Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro ambaye aliungana na Lema na madiwani wengine kupinga jambo hilo.
Baada ya vuta nikuvute hiyo mbele ya waziri, Agosti 18 Gambo aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha kuchukua nafasi ya Felix Ntibenda.
Siku chache baada ya uteuzi huo, Gambo aliagiza halmashauri ya jiji kutafuta fedha za kupunguza deni la walimu ambalo ni Sh154 milioni.
Mkurugenzi wa jiji hilo, Athuman Kilamia alitangaza posho za madiwani ambazo zilikuwa zinalipwa kinyume cha taratibu, zitumike kupunguza deni la walimu na zikatolewa.
Mgogoro ukaibuka kati ya madiwani wa jiji hilo ambao wengi ni kutoka Chadema.
Sakata la Jumanne wiki hii linaweza kumpa cheo kikubwa zaidi kutokana na Rais Magufuli kumpigia simu kwa lengo la kumthibitishia kuwa yuko pamoja naye siku ambayo barua ya kughushi ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa mkuu huyo wa nchi ametengua uteuzi wa Gambo.
Sakata hilo lilitokea katika uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali ya mama na mtoto jijini Arusha ambao utagharimu Sh9 bilioni, sehemu kubwa ya fedha hizo zikitoka taasisi ya Martenity Africa.
Mvutano huo ulianza baada ya Gambo kusema kuwa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa hospitali imetolewa na Taasisi ya Mawalla Fund kwa kuwa muasisi wake, Nyaga Mawalla alikuwa na maono ya kusaidia afya ya mama na mtoto.
Kauli yake ilikuwa ikimaanisha kuwa Mfuko wa Maendeleo wa Arusha (ArDF) haikutoa kiwanja hicho kwa Martenity Africa wala kutafuta mfadhili.
Jambo hilo liliwakera viongozi wa ArDF, ambayo imeanzishwa na Lema na Elifuraha Mlowe, ambaye ni mwenyekiti.
Lema alimtaka ndugu wa wakili huyo amsahihishe Gambo, lakini hakuna kilichofanyika, ndipo aliposimama na kuanza kupinga kwa sauti maelezo ya Gambo.
Lema alikuwa akisema mkuu huyo wa mkoa anapotosha ukweli kwa misingi ya kisiasa, kwa kuwa Mawalla Fund ilitoa kiwanja hicho kwa ArDF, ambayo ilitafuta wafadhili na kusaini nao mkataba wa ujenzi wa hospitali.
Wageni kwenye hafla hiyo iliyofanyika Bulka walijaribu kuwatuliza wawili hao, hawakufanikiwa kutokana na Lema kuendelea kueleza kwa sauti kuwa Gambo anapotosha, huku mkuu huyo wa mkoa akizungumza kwenye kipaza sauti kumtaka mbunge huyo atulie.
Shughuli hiyo ilimalizika kiutata na hivyo waandaaji wakashindwa kuendesha harambee iliyopangwa kufanyika baada ya uzinduzi.
Social Plugin