Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS MAGUFULI AFUNGUA KUHUSU UTITIRI WA VYUO VIKUU 'SIO LAZIMA KILA MAHALI KUWE NA CHUO, VINGINE VIKO VICHOCHORONI KWELI'

RAIS John Magufuli amesema kumekuwa na utitiri wa vyuo vikuu nchini, hivyo ni lazima sifa za vyuo hivyo ziangaliwe upya na kwamba sio lazima kuwepo na vyuo vikuu kila mahali, ila vinaweza kuwa vichache vilivyoboreshwa kupokea wanafunzi wengi.


Hivyo, ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi na mamlaka husika, kuangalia upya utaratibu wa utoaji vibali vya kuanzisha vyuo hivyo kwa sababu vyuo vingine havina sifa wala havina walimu hivyo vinachangia kushusha ubora wa elimu nchini.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ameagiza uwepo utaratibu wa vyuo vikuu vyote nchini, viwe vinafungua kwa nyakati moja ili kuwe na mpango mzuri kwa kupeleka fedha kwa ajili ya wanafunzi wanaopata mikopo kwa lengo la kuondoa usumbufu usio wa lazima.

Rais Magufuli alisema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati akiweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa mabweni 20 ya wanafunzi katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Mabweni hayo kila moja lina ghorofa nne na ujenzi wake unatarajiwa kukamilika Desemba 30, mwaka huu na yatakuwa na uwezo wa kubeba wanafunzi 3,840.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Rais Magufuli alisema kuna haja ya Wizara ya Elimu, Sayansi,Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi na mamlaka nyingine husika, kuangalia upya sifa za uanzishwaji wa vyuo nchini kwa maana hakuna sababu ya kuwa na vyuo vikuu kila kona nchini.

“Huu utitiri wa vyuo vikuu lazima uangaliwe upya, lazima sifa ziainishwe sio shule ya sekondari inageuka eti nayo ni chuo na inafikia wakati wanagombania wanafunzi, mfano Chuo Kikuu cha Dodoma uwezo wake ni kudahili wanafunzi 45,000 walioko sasa ni 30,000, halafu unafungua Chuo Bagamoyo hakina hata maabara wala mabweni unapeleka wanafunzi 20, sasa hiki ni chuo au?” Alihoji Rais Magufuli.

Aliongeza, “Wizara pitieni vibali vya kuanzisha vyuo vikuu kwa sababu vilivyopo havijajaa wanafunzi; na vyuo vingine havina walimu, mnapotoa vibali kila kona kuanzishwa vyuo vikuu hata ubora wa elimu unashuka”.

Alisema hatua ya nchi kuwa na vyuo vikuu kila kona, inachangiwa pia na wasomi kupenda kuitwa ‘Vice Chancellor’, na kumuagiza Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako, kusimamia hilo ili kuwe na vyuo vichache hata vinne tu.

Rais alitaka nchi iwe na vyuo vikuu vichache vitakavyoboreshwa ili vibebe idadi kubwa ya wanafunzi, hata wafike milioni moja kwa chuo kikuu kimoja na mazingira yaboreshwe na wawepo walimu wenye sifa wa kutosha, watakaohudumiwa vizuri ili wafundishe kwa tija.

Alisema vyuo vya aina hiyo vitatoa wasomi wenye sifa, badala ya kuwa na utitiri wa vyuo usio na tija.

“Sio lazima kila mahali kuwe na chuo, vingine viko vichochoroni kweli, tumepoteza mwelekeo, tumevuruga elimu vya kutosha ni lazima tujirekebishe sio kila chuo lazima kiwe chuo kikuu,” alisisitiza Rais Magufuli.

Alitoa mfano kuwa vyuo vya ufundi vilivyokuwepo, kama vile Moshi Ufundi na Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT), vilipaswa kuboreshwa na kuendelea kutoa mafunzo hayo, badala ya kugeuzwa kuwa vyuo vikuu.

Aidha, alisema sio lazima kila mtu asome chuo kikuu, bali kuna fani nyingine za ufundi zinazopaswa kusomewa, ili taifa liwe na wasomi wenye taaluma mchanganyiko na sifa tofauti.

“Nasema kwa uwazi, wala siogopi, lazima tukae, tuchanganue vizuri, tunataka kujenga elimu gani, ndio maana kila mahali wanaomba mikopo, tungekuwa tuna mipango mizuri suala la mikopo lisingeleta mchanganyiko huu,” alisema Rais Magufuli.

Alitoa mfano wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kusema hakuna sababu ya kudahili wanafunzi wa udaktari, kwa sababu kuna Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili na Mloganzila, ambacho kimebobea kwenye fani hizo.

“Watu walijua UDSM ni Sheria, Uhandisi na kozi nyingine, Chuo cha Sokoine Mogororo(SUA) watu walijua ni mahususi kwa ajili ya kilimo, Mzumbe tulijua ni kwa ajili ya maofisa utumishi, sijui kama leo kinatoa fani hiyo, sasa lazima tuangalie upya vibali vya kusajili vyuo vikuu,” alisisitiza Rais Magufuli.

Mikopo kwa wanafunzi

Akizungumzia mikopo kwa wanafunzi, Rais Magufuli alisema bajeti iliyopita ya mwaka 2015/16 ilitengewa Sh bilioni 340 kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ambao wanufaika takribani 60,000 walipata.

Alisema serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani, bajeti iliyotengwa kwa ajili ya mikopo ilikuwa Sh bilioni 340, lakini fedha hizo ziliongezwa kutokana na makusanyo ya mapato na kufikia Sh bilioni 475 ambazo zilipewa wanufaika 124,358.

Aidha, mwaka huu bajeti ya mikopo kwa wanafunzi hao imeongezeka na kufikia Sh bilioni 483 na hiyo inatoa fursa kwa wanafunzi wapya karibu 25,000 kupata pamoja na wale wanaoendelea ambao idadi yao ni takribani 63,000.

Hata hivyo, alisema ni lazima akiri kwamba awali hapakuwepo na mfumo wa mawasiliano mzuri baina ya vyuo na taasisi zinazohusika na elimu na mikopo na kuagiza kuanzia sasa utaratibu wa vyuo kufunguliwa, lazima uwe unafanana ili kuweka maandalizi mazuri ya kusambaza mikopo kwa wanafunzi.

“Ni lazima nikiri hapakuwepo na utaratibu mzuri kwa vyuo na taasisi za elimu zinazoshughulika na wanafunzi na hata mikopo, kwanza vyuo vyote vya elimu ya juu vingekuwa na tarehe moja ya kufungua chuo, kwa maana sasa vipo vilivyofungua jana (juzi) vingine vina wiki kadhaa sasa na vingine vinafungua kesho kutwa… …ukifungua harakaharaka wanafunzi wanakuwa hawajapata mkopo halafu unasema wafanye usajili ilihali majina ya wanufaika wa mikopo hayajatolewa hii inaleta mkanganyiko kwa wanafunzi, lazima kuwe na mawasiliano baina ya taasisi zote kuonesha majina, muda wa chuo na wanaostahili kunufaika, hivi mnawachanganya,” alisema Rais Magufuli.

Aidha alisema wizara inatakiwa kujipanga kwenye hilo na wananchi wanapaswa kutambua kuwa lengo la serikali sio kuwasumbua wanafunzi, lakini pia alisisitiza serikali haitatoa mikopo kwa wanafunzi walio na uwezo bali mkopo ni kwa wale tu wasio na uwezo ila wana sifa za kupewa mikopo husika.

Alisema anafahamu kuwa hata kwenye Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), kuna upendeleo hata wasiostahili wanapewa mikopo sasa na kuwataka wajirekebishe kwa sababu anaweza akaenda na kuomba orodha ya wanufaika kuikagua.

“Naomba nisifike huko, na Profesa Ndalichako baada ya kuona kuna changamoto kwenye mikopo, alinitaarifu na kuagiza Wizara ya Fedha itoe Sh bilioni 80 na nimeambiwa zimeshapelekwa, sasa ni vyema wanaonufaika nao wakawa wazalendo wakarejesha mkopo,” alisema.

Alisema hadi sasa serikali inadai Sh trilioni 2.6 ambazo zilikopeshwa kwa wanufaika mbalimbali wa elimu ya juu lakini bado hadi sasa hawajarejesha na hiyo inaleta changamoto kwa waombaji wapya.

Akizungmzia ujenzi wa mabweni hayo, Rais Magufuli alisema anajua kero ya wanafunzi kukosa mahali pa kulala na ujenzi wa mabweni hayo utapunguza uhaba huo na kuwafanya wanafunzi kusoma kwenye mazingira mazuri na salama zaidi.

Mabweni hayo yanajengwa na Wakala wa Majengo nchini (TBA), na mradi huo umegharimu Sh bilioni 10, na kwamba awali Rais Magufuli alisema mkandarasi kutoka nje alisema angejenga mradi huo kwa gharama ya Sh bilioni 100.

Akiwapongeza TBA, Rais Magufuli alisema wametekeleza mradi bila faida na kwamba wameufanya kwa weledi na kwamba atawapa mradi mwingine mjini Dodoma kuutekeleza kwa sababu wanafanya kwa kiwango kizuri na gharama nafuu.

Hata hivyo, alisema elimu ina changamoto yake lakini serikali imeipa kipaumbele cha pekee na ndio maana iliamua kutoa elimu bure kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha nne na kila mwezi serikali inatoa Sh bilioni 18.77.

“Ni bahati mbaya kila kizuri kina changamoto zake, tulipoanza kutoa ndio kukaibuka hata wanafunzi hewa, kule Mwanza kuna wilaya moja wanafunzi hewa ni zaidi ya 5,000, kule Arusha ni 9,000, hapa Dar ni 7,000,”alisema Rais Magufuli.

Alisema watumishi hewa nao wamefikia 16,500 na kwamba inawezekana pia kuna hata ndoa hewa na kwamba amejaribu kuwa wazi ili wananchi wajue mipango ya serikali.

“Nimejaribu kuwa wazi na serikali yangu ili mfahamu kuwa tunapitia kipindi cha mabadiliko,tubadilishe tabia tulizozijenga huko nyuma na tunapitia kipindi hiki ni kukugumu kwa sababu kila unapogusa unakutana na hewa, naomba mnivumilie nataka kujenga serikali nzuri,” alisisitiza Rais Magufuli.

Imeandikwa na Ikunda Eric-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com