Amiri Jeshi Mkuu Rais Dkt John Pombe Magufuli akipiga ngoma za bendi ya jeshi ya Mwenge Jazzz wana Paselepa wakati wa kufunga Zoezi la medani katika kilele cha maadhimisho ya miaka 52 ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) huko Baatini, Bagamoyo mkoa wa Pwani leo Septemba 30, 2016
***
RAIS John Magufuli amesema anaamini yuko salama kwa kuwa vyombo vya ulinzi na usalama nchini ni imara, vinaheshimika ndani na nje ya nchi na hakuna anayeweza kuichezea nchi.
Aidha ameagiza askari 40 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na mgambo 30 walioshiriki kwenye zoezi la ‘Amphibious Landing’, kuajiriwa rasmi katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuanzia leo, huku pia akitoa agizo la kutowapelekea fedha wafungwa katika Magereza yaliyoharibiwa na tetemeko la ardhi mkoani Kagera na badala yake wafungwa hao watumike kukarabati gereza hilo.
Hayo yalibainishwa mjini hapa jana na Rais Magufuli wakati akifunga rasmi mazoezi ya kutua ardhini kutoka majini, kukomboa eneo lililotekwa na adui (Amphibious Landing) ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya miaka 52 ya JWTZ.
Akizungumza baada ya zoezi la jeshi kukamilika, Rais Magufuli alisema ameridhika na kazi inayofanywa na jeshi hilo na kuwa hakuna mtu anayeweza kuichezea nchi.
“Tuna jeshi imara, linaloheshimika, sina mashaka, niko salama, chombo hiki ni nguzo muhimu ya amani nchini, ndio maana nataka linitumie kwa sababu lina nidhamu sana,” alisisitiza Rais Magufuli ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu.
Alisema uwezo uliooneshwa na askari hao hususani komandi zote zilizoshiriki kwenye mazoezi ya mafunzo hayo mahsusi kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano na utendaji kazi wa vikosi vyote vya jeshi, ni wa hali ya juu na wanapaswa kuheshimiwa kwa uadilifu wao na uzalendo wa kweli kwa nchi yao.
Akizungumzia uimara wa jeshi hilo, Rais Magufuli alisema umetokana na misingi imara iliyowekwa na marais waliotangulia, huku akimshukuru Rais mstaafu Jakaya Kikwete kwa kuhakikisha ameliwezesha jeshi kuwa na vifaa imara, ambavyo jana vilitumika kuonesha uimara wa chombo hicho.
“Niwashukuru marais wote waliotangulia, ila nimshukuru sana Rais Kikwete yeye ndiye aliyewezesha jeshi kuwa na vifaa imara kama hivi, mimi sijanunua kitu hapa, siwezi kujisifu, ni juhudi za Kikwete na mimi nitaendeleza na kuhakikisha tunakuwa na jeshi imara na ikiwezekana kuzidi majeshi yote duniani,” alisema.
Akizungumzia ajira kwa JKT na mgambo, Rais alisema; “ Chief Secretary (Katibu Mkuu Kiongozi) kuanzia kesho (leo), hawa mgambo na JKT walioshiriki kwenye zoezi hili waingizwe kwenye ajira rasmi jeshini, nguvu zao hazipotei, hata kama hawajaenda mafunzo ya jeshi waingizwe wataenda baadaye.”
Katika hatua nyingine, alisema hafurahishwi na vitendo vya Jeshi la Magereza kuombaomba serikalini fedha kwa ajili ya kukarabati gereza mjini Bukoba lililoharibiwa na tetemeko na kuagiza ni marufuku fedha kutolewa kwa ajili ya ukarabati wake.
“Ni marufuku fedha kupewa Magereza kwa ajili ya wafungwa kwenye gereza lililoharibiwa na tetemeko, wale wanaotumikia adhabu wafanye kazi kujenga maeneo yaliyobomoka,” alisema.
Katika tukio hilo lililokuwa la aina yake, ndege vita saba zilipita kwa kasi angani huku zikidondosha mabomu, ambapo pia meli vita tatu zilijipanga baharini zikiwa na askari huku vifaru saba vikiwa baharini na kisha kwenda nchi kavu kumshambulia adui.Imeandikwa na Ikunda Erick- Habarileo -Bagamoyo