Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKUU WA SHULE YA SEKONDARI SHINYANGA ATUMBULIWA KWA ULEVI SHULENI

MKUU wa Shule ya Sekondari Shinyanga Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Marxon Paul amevuliwa madaraka kutokana na tabia ya ulevi na kushindwa kusimamia taaluma.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga amechukua hatua hiyo baada ya kufika shuleni hapo na kukuta mgomo uliochangiwa na tabia ya mkuu huyo.

Kaimu Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari katika Halmashauri hiyo, Paul Kasanda amesema mkuu huyo wa shule ameshindwa kuwasimamia walimu anaowaongoza.

Kasanda alisema kutokana na kushindwa kuwasimamia walimu wamekuwa wakijiamulia wenyewe mambo yao na hivyo kutofundisha ipasavyo, hali iliyochangia kuporomoka kwa taaluma shuleni hapo.

“Ni kweli Mkurugenzi jana alitembelea shule hiyo na kupata malalamiko kutoka kwa wanafunzi, amechukua uamuzi wa kumvua madaraka mkuu wa shule,” alisema Kasanda.

Alibainisha kuwa, shule hiyo ambayo ni ya wavulana ya bweni imekuwa ikiporomoka siku hadi siku kutokana na kuwa na uongozi ambao haufanyi kazi yake ipasavyo.

“Tumeona tuchukue hatua stahiki dhidi ya mkuu huyo wa shule ili iwe fundisho kwa wengine, hebu fikiria kiwango cha ufaulu kimekuwa kikishuka kila mwaka tangu 2012 katika mitihani mbalimbali wanayofanya wanafunzi,” amesema Kasanda.

Kwa sasa shule hiyo inaongozwa na Makamu Mkuu, Marco Badalaha hadi pale uteuzi mwingine kuziba nafasi hiyo utakapofanywa na Katibu Tawala wa Mkoa.

Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com