MTOBOA MACHO ALISHINDA MILIONI 20 ZA DUME CHALLENGE, MSHIRIKI MWENZAKE AMWELEZEA ALIVYOMFAHAMU




Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akimsikiliza Said Ally akisimulia mkasa huo.

Wiki hii, habari kubwa nchini ilikuwa ni tukio la mfanyabiashara, Said Ally kutobolewa macho, usiku katika maeneo ya Buguruni Sheli jijini Dar es Salaam. 

Jina la ‘Scorpion’ – mtu aliyefanya unyama huo, limekuwa maarufu pia. Polisi tayari wamemkamata na Jumatano hii alipandishwa kizimbani kusomewa mashtaka mbalimbali yakiwemo kupora na kumjeruhi Said kwa kumchoma visu mwilini na kumtoboa macho yake na kumpa upofu wa ukubwani.



Scorpion baada ya kukamatwa na kupandishwa kizimbani
SCORPION NI NANI?

Jina lake halisi ni Salim H Njwete au Samjet. Unaweza ukawa umewahi kumuona sehemu. Mwaka 2012, alikuwa mshindi wa shindano la Dume Challenge lililowakutanisha vijana 20 wababe wa mazoezi na kazi ngumu. Salim alijinyakulia kitita cha shilingi milioni 20.


Salim Njwete aka Scorpion (Kushoto) akikabidhiwa mfano wa hundi kufuatia kutangazwa mshindi wa shindano la Dume Challenge, December 2012

Ni mwalimu wa karate na mbabe wa mapigano na ndio maana pindi anamshambulia Said hakuna aliyethubutu kumsaidia kwasababu kila mtu maeneo ya Buguruni anamhofia.

Ni muigizaji wa filamu pia na kwa mujibu wa Walter, aliyekuwa mshiriki mwenzake kwenye Dume Challenge, baada ya mashindano hayo Salim alitoa filamu moja.

Walter ameiambia Bongo5 kuwa Salim alikuwa mtu wa kawaida kabisa na ambaye isingekuwa rahisi kumdhania angekuja kuwa mnyama kiasi hicho.




Walter ambaye ni mwanamuziki na anayefanya kazi za ulinzi kupitia kampuni yake, ni mmoja wa washiriki 20 walioshiriki kwenye shindano hilo

Walter anasema, Salim ni mjuzi wa mchanganyiko mapigano ya aina nyingi. Anadai aliposikia kuwa ndiye Scorpion, alishangaa mno.

“Lazima nishangae kwasababu, ni kitu ambacho hujawasiliana na mtu kwa muda mrefu kidogo halafu ghafla unakuja kusikia negative side ya mtu ambaye mnafahamiana naye, na ambaye mlishirikiana naye kama wakati tupo kwenye mashindano kule tulikuwa tunalala yaani kitanda hiki hapa na hiki hapa,” Walter ameiambia Bongo5.


“Ni mtu ambaye mmeshirikiana kitu fulani ambacho tayari kilishakuwa on public na watu tayari washajua taswira yenu, sasa mtu anapokuja kufanya kitu kama hicho, ina maana hata wewe mwenyewe unahisi taswira yako inachukuliwa kama vile mshikaji,” ameongeza.

Walter anasema baada ya kushinda milioni 20 kwenye shindano hilo, anachojua ni kuwa Salim aliingia kwenye uigizaji wa filamu na pia alikuwa na mpango wa kwenda kufanya kilimo. Anaeleza kuwa kwenye filamu, Salim alikuwa chini ya Tuesday Kihangala maarufu kama Mr Chuzi.

“Aliamua kuspend hizo hela zake katika movie na akabahatika kutoa movie moja ambayo haikufanya vizuri katika industry,” anaeleza Walter. “Sasa maisha baada ya hapo, sijui ndio akaamua kuspend hela zilizobaki kwenye kitu gani, labda kwenye kilimo kwasababu wakati tulipokuwa naye kule kambini – maake si unajua unamuuliza hizi hela unazifanyia nini, yeye alikuwa amewaza kwenda kulima huko Morogoro.”

Walter amesema washiriki wenzake wengine wa Dume Challenge wameshangazwa na alichokifanya Salim. “Wako shocked yaani,” anasema. “Ni kitu ambacho hakuna aliyetegemea kwamba jamaa alikuwa anaweza kufanya kitu kama hicho.”

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post