Mwanafunzi
wa mwaka wa tatu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii (CDTI) cha mkoani
Arusha, Allan Mbando, ameibwaga Serikali katika kesi ya kudaiwa
kusambaza ujumbe kupitia Mtandao wa Facebook akimtaka Mwamunyange
apindue nchi.
Katika mtandao huo wa kijamii, Mbando, anadaiwa kutuma ujumbe uliosomeka kwamba: “Mwamunyange pindua nchi haiwezekani wote wawe nje, halafu hakuna aliyepewa mamlaka ya kukalia kile kiti.”
Kutokana
na madai hayo, Jeshi la Polisi mkoani Arusha lilimfungulia mashtaka
Mbando ya kudaiwa kusambaza ujumbe huo uliokusudia kueneza na kufanya
uchochezi.
Akisoma
hukumu ya kesi hiyo mjini hapa juzi, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama
ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Arusha, Augustine Rwizile, alisema mahakama
hiyo imepitia kwa kina hoja na ushahidi wa pande zote mbili katika kesi
hiyo.
Hakimu
Rwizile alisema baada ya kupitia ushahidi katika kesi hiyo, mahakama
imejiridhisha kuwa upande wa Jamhuri katika kesi hiyo haukuweza
kuwasilisha ushahidi unaoweza kumtia hatiani mshtakiwa.
Alisema
mbali na ushahidi huo kutojitosheleza, pia hapakuwapo na jambo lolote
lenye nia ovu ya kusababisha au kufanya uchochezi katika ujumbe
uliosambazwa na mshtakiwa.
“Sasa
mahakama hii inamwachia huru mshtakiwa baada ya upande wa Jamhuri
kushindwa kuthibitisha mashtaka yake pasipo kuacha shaka yoyote.
“Lakini pia kama kutakuwa na upande ambao haujaridhika katika hukumu hii unaweza kukata rufaa,” alisema Rwizile.
Akisoma
hukumu hiyo, alisema ujumbe uliosambazwa haukuwa na umuhimu wowote kwa
kuwa haukumwelezea Mwamunyange ni nani katika nchi anayotakiwa kuipindua
huku pia ujumbe huo ukiwa haukutaja nchi iliyolengwa kupinduliwa.
“Ujumbe
ulioandikwa katika Facebook haumtambulishi Mwamunyange ni nani. Lakini
ujumbe hauonyeshi jambo la msingi lenye uhusiano wa kisiasa katika Taifa
linalodaiwa,” alisema Rwizile.
Kutokana
na sababu hizo ikiwamo ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo
kushindwa kuthibitisha ujumbe uliosambazwa na mshtakiwa, mahakama
ililazimika kumwachia mshtakiwa.
Mshtakiwa huyo katika kesi hiyo alikuwa akitetewa na Wakili Moses Mahuna.
Mbando
anaongeza idadi ya watu walioshtakiwa mahakamani kutokana na makosa ya
mtandaoni baada ya Aprili, mwaka huu mkazi mwingine wa Arusha, Isack
Habakuki (40), kufikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka ya kusambaza
lugha ya matusi na dhihaka kwa Rais Dk. John Magufuli.
Baada
ya kesi hiyo kuendelea kusomwa mahakamani hapo, Isack alihukumiwa
kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh milioni saba na yeye
alikubali kuzilipa kwa awamu.
Mtu
mwingine aliyeshtakiwa Aprili, mwaka huu kwa makosa ya mtandaoni ni
kondakta wa daladala, Hamimu Seif (42), aliyepandishwa kizimbani kwa
kosa analodaiwa kulifanya Machi 10, mwaka huu alipotishia kumuua Rais
Magufuli kwa maneno akiwa katika Baa ya Soweto iliyopo Makumbusho,
Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.