Kamanda wa jeshi jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne akionesha vifaa vya uganga vya waganga wa kienyeji 22 waliokamatwa wakidaiwa kujihusisha na upigaji ramli chonganishi na kukutwa na nyara za serikali ambazo ni ngozi za wanyama-Picha zote na Kadama Malunde- Malunde1 blog
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga akionesha jino la tembo na nyara zingine za serikali ikiwemo vipande vya ngozi ya samba,nyati,fisi,nyiriri na kenge,mikia 10 ya nyumbu,kucha za kenge,jino la ngiri na pembe za nyati na tandala.
Waandishi wa habari wakichukua matukio
Kamanda Muliro akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo
Kamanda Muliro akionesha silaha aina ya bastola browing yenye namba BIPNB-YE- 0041 ikiwa na risasi 6 inayodaiwa kutumika katika matukio ya uhalifu wa unyang’anyi wa kutumia silaha aliyokutwa nayo Nicholaus Daniel (23) mkazi wa Manzese wilayani Kahama
Kamanda Muliro akionesha silaha aina ya gobore aliyokamatwa nayoPeter Mganda(56) mkazi wa kijiji cha Buyenge .Silaha hizo zinadaiwa kutumika katika matukio ya uhalifu ndani na nje ya mkoa wa Shinyanga
Kamanda Muliro akionesha kamera mbili zinazotumika katika zoezi la kuandikisha vitambulisho zilizokuwa zimeibiwa katika la halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga
Kamanda Muliro akionesha kamera mbili zinazotumika katika zoezi la kuandikisha vitambulisho zilizokuwa zimeibiwa katika la halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga ambazo zimekutwa nyumbani kwa mlinzi wa jengo la halmashauri ya wilaya ya Kishapu
Kamanda Muliro akionesha stand za kamera mbili zinazotumika katika zoezi la kuandikisha vitambulisho zilizokuwa zimeibiwa katika la halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga
Kamanda wa Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga Muliro Jumanne Muliro akionesha begi lenye madawa ya kulevya aina ya bangi “cannabis sativa” yenye uzito wa kilogramu 35 lililokuwa linasafirishwa kutoka Isaka wilayani Kahama kwenda Jijini Dar es salaam na Sophia Kiboa (29) mkazi wa Kilimahewa jijini Mwanza .
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga akionesha vitu mbalimbali vilivyokamatwa na jeshi la polisi zikiwemo kamera,nyara za serikali na vitu vya wizi vilivyomakatwa nyumbani kwa mlinzi wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu Mustapha Mabula.
********
Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga limefanikiwa kukamata
watuhumiwa 28 wanaodaiwa kujihusisha na
mauaji ya vikongwe kwa kisingizio cha kuwa ni wachawi pamoja na waganga wa
kienyeji 22 wanaopiga ramli chonganishi na kusababisha kuendelea kutokea kwa
mauaji katika jamii.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Oktoba 12,2016 ,kamanda wa polisi
mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro alisema watuhumiwa hao wamekamatwa
katika operesheni ya jeshi hilo inayoendelea ndani na nje ya mkoa wa Shinyanga
kuzuia,kupambana na wahalifu.
Kamanda Muliro alisema katika operesheni hiyo isiyokuwa na
mipaka wamekamata wauaji ambao hukodishwa na baadhi ya wanafamilia kutekeleza
mauaji ya vikongwe hasa wanawake ,wanaodaiwa kuwa ni wachawi.
“Watu hawa wazima huambia wao ni wachawi na huzingiziwa kuwa
wao ndiyo wamesababisha matatizo kama vile magonjwa au vifo vilivyotokea katika
jamii husika”,alieleza Kamanda Muliro.
“Tumekamata watuhumiwa 28 wenye umri kati ya miaka 25 hadi
50 wote wanaume,kundi hili hufanya mauaji zaidi nyakati za usiku wakati wazee
hawa wakiwa wanapata chakula au wamelala kwa kuwakata mapanga”,aliongeza
Kamanda Muliro.
Alieleza kuwa watuhumiwa hao wamehojiwa kwa kina na wamekiri
kujihusisha na kufanya matukio ya mauaji ya vikongwe maeneo mbalimbali ya mkoa
wa Shinyanga na mikoa jirani hasa katika wilaya za Uyui na Kaliua mkoani Tabora
na Mbogwe na Nyangh’wale mkoani Geita.
Kamanda Muliro aliongeza kuwa tayari watuhumiwa 10
wamepelekwa mkoani Tabora kwenye maeneo walikofanya matukio na watuhumiwa
wengine 10 wamefikishwa mahakamani mkoani Shinyanga.
Katika hatua nyingine Kamanda Muliro alisema katika
operesheni hiyo endelevu iliyoanza Septemba 19,2016 walikamata waganga wa
kienyeji 22 wanaodaiwa kujihusisha na upigaji wa ramli chonganishi
zinazosababisha mauaji katika jamii baada ya kuwadanganya wananchi.
Alisema waganga wa kienyeji 11 kati ya hao 22 walikutwa na
nyara za serikali ikiwemo jino la tembo,vipande vya ngozi ya
samba,nyati,fisi,nyiriri na kenge,mikia 10 ya nyumbu,kucha za kenge,jino la
ngiri na pembe za nyati na tandala.
Alieleza kuwa vitu hivyo vilivyokamatwa vimekuwa vikitumiwa
pia kama nyenzo za kuwadanganyia wananchi na kuwachonganisha kwa kueleza kuwa
matatizo yanayotokea katika familia yanasababishwa na mtu fulani kwa kuwataja
wazee kuwa wao ndiyo wachawi.
“Baada ya kuwataja kuwa ni wachawi,wanafamilia huchukua
maamuzi ya kushirikisha kundi la wauaji wa kukodi ambapo kundi hilo ovu
hujipatia kipato kutoka kwa ndugu hao kwa kufanya kazi ovu ya kuua”,alifafanua
kamanda Muliro.
Alisema tayari pia watuhumiwa hao wamehojiwa kwa kina na
baadhi yao wamefikishwa mahakamani.
Aliongeza kuwa pia wamekamata watuhumiwa wawili wa uhalifu
wa unyang’anyi wa kutumia silaha ambao ni Nicholaus Daniel (23) mkazi wa
Manzese wilayani Kahama na aliyekamatwa
na silaha aina ya bastola browing yenye namba BIPNB-YE- 0041 ikiwa na risasi 6.
Alimtaja mtuhumiwa mwingine kuwa Peter Mganda(56) mkazi wa
kijiji cha Buyenge akiwa na silaha aina ya gobore na kwamba silaha hizo
zinadaiwa kutumika katika matukio mbalimbali ya unyang’anyi wa kutumia silaha
mkoa wa Shinyanga na mikoa jirani.
Aidha jeshi hilo limemkamata Sophia Kiboa (29) mkazi wa
Kilimahewa jijini Mwanza akiwa na begi lenye madawa ya kulevya aina ya bangi
“cannabis sativa” yenye uzito wa kilogramu 35 aliyokuwa akisafirisha kutoka
Isaka wilayani Kahama kwenda Jijini Dar es salaam.
“Alikuwa amefunga madawa hayo kiustadi mkubwa kama nguo na kuviringisha
kwa mfuko wa nailoni ili isiwe kwa maafisa wa polisi kuhisi au kupata harufu ya
madawa hayo na mtuhumiwa amefikishwa mahakamani baada ya kuhojiwa kwa
kina”,aliongeza kamanda Muliro.
Na Kadama Malunde- Malunde1 blog