Kikosi
Maalumu cha Kupambana na Ujambazi wa Kutumia Silaha cha Jeshi la Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kilifanikiwa kukamata watuhumiwa wanne
wa ujambazi waliohusika katika mauaji ya askari polisi 4 katika benki ya
CRDB iliyopo maeneo ya Mbande, Mbagala jijini Dar es Salaam.
Kamishna
wa Kanda hiyo, Kamanda Simon Sirro wakati akizungumza na waandishi wa
habari leo jijini Dar es Salaam, amesema watuhumiwa hao walikamatwa
wakati wa majibizano ya risasi yaliyotokea Oktoba 11, 2016 katika pori
la Dondwe lililopo Chanika.
“Kikosi
kilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja, baada ya kupata taarifa kutoka
kwa raia wema kuwa ni jambazi na ndiye aliyehusika katika mauaji ya
askari polisi huko Mbande,” amesema.
Kamanda Sirro ameongeza kuwa “Baada
ya kumkamata mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na tukio hilo akiwa na
wenzie saba, alitupeleka mahala walipo wenzake, ila alikimbia, wenzie
walipojua polisi wapo maeneo hayo, walianza kurusha risasi ndipo polisi
nao wakaanza kurusha risasi.”
Kamanda
Sirro amesema kuwa, watuhumiwa hao walizidiwa na mashambulizi ya risasi
ambapo walijeruhiwa vibaya na kwamba walifariki dunia wakiwa wanapatiwa
matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Amesema
askari polisi walifanikiwa kuipata bunduki ya kijeshi aina ya SMG
iliyofutwa usajili ambayo watuhumiwa hao waliipora kutoka mikononi mwa
polisi waliowaua mbande ikiwa na risasi 22 ndani ya magazine.
Katika
tukio lingine, Kamanda Sirro amesema mnamo Oktoba 11, 2016 maeneo ya
magomeni polisi wakiwa doria walifanikiwa kukamata bastola moja aina ya
bereta baada ya kutelekezwa na kundi la vijana.
Pia
amesema Jeshi la Polisi limekamata watuhumiwa watatu wakiwa na bomu
moja la kienyeji, mapanga manne, visu viwili, na bisibisi moja.
Vilevile Jeshi la Polisi Dar es Salaam Oktoba 12, 2016 walikamata panya road zaidi ya 10 maeneo ya Mbagala.