RAIS
Dk. John Magufuli, amemwagiza Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara,
Charles Mwijage kumrudishia mfanyabiashara maarufu nchini, Said Salim
Bakhresa sukari yake iliyozuiwa bandarini kwa sababu biashara yake ina
tija kwa taifa.
Mbali
na hayo, Rais pia amelipa Shirika la Umeme (Tanesco) miezi miwili
kufikisha huduma ya umeme katika kiwanda cha kusindika matunda na
kuzalisha juisi cha Bakhresa Food Products Ltd kilichopo Mwandege
wilayani Mkuranga, mkoani Pwani.
Rais
alitoa maagizo hayo jana wakati wa hafla ya uzinduzi wa kiwanda hicho
ambapo alisema ameridhishwa na uwekezaji wa kampuni hiyo.
Sukari
hiyo ya Bakhresa ilizuiwa katika Bandari ya Dar es Salaam pamoja na
wafanyabiashara wengine miezi michache iliyopita wakati Rais Magufuli
alipotangaza kusitisha vibali vya kuagiza sukari kutoka nje kwa madai ya
kulinda viwanda vya ndani.
Agizo
hilo lilisababisha uhaba mkubwa wa sukari ambapo ilipanda na kufikia
wastani wa Sh 4,500 hadi 6,000 katika baadhi ya mikoa nchini.
“Tena
ndugu yangu, nitakupa eneo ulime miwa ili upate sukari ya viwandani na
ya majumbani, tena nitakupa bure, wewe Bakhresa umenifurahisha sana kwa
uwekezaji wako na sukari yako niliyoizuia bandarini leo namwagiza
Waziri Mwijage itoke na upatiwe,”alisema Rais Magufuli bila kufafanua kiasi gani cha sukari kilichozuiwa.
Aidha
Rais alisema kutokana na uhaba wa sukari unaoikumba Tanzania kwa miaka
mingi ni vyema kushirikiana na wawekekzaji ili kuondokana na tatizo
hilo.
Katika tamko lake Rais aliagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuipatia kampuni hiyo ya Azam eneo la ekari 10,000 kwa ajili ya kilimo cha miwa.
“Kupitia
kilimo hicho Watanzania wengi watapata ajira na pia kiwanda kitatumia
sukari ambayo ni salama kwa afya zetu na pia kuongeza upatikanaji wa
sukari hapahapa nchini,” alisema.
Kuhusu
Tanesco, Rais Magufuli alisema suala hilo hawezi kulifumbia macho
kwakuwa Tanzania ya viwanda inategemea zaidi upatikanaji wa umeme wa
uhakika.
“Saa
nyingine inashangaza kweli, kiwanda kinaanza kujengwa, watu wapo,
kinakamilika, watu wapo, kinaanza kufanya kazi watu wapo, kinaajiri watu
wote hawa, wanafunga jenereta lao, tena makao makuu ya Wizara ya
Nishati na Madini ipo kilomita chache kutoka hapa,”alisema Rais Magufuli.
Rais
pia alisema Serikali yake inaangalia namna ya kukutana na wataalamu
kuangalia mfumo mzuri wa kuwatoza kodi wawekezaji bila usumbufu.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Kampuni ya Bakhresa, Aboubakari Salim alisema kuna urasimu
mwingi katika upatikananji wa maeneo mapya ya kuanzisha viwanda.
“Tasisi
za utozaji kodi zimekuwa nyingi ambapo utendaji wake ni ule ule hivyo
zinatupa usumbufu katika utendaji wetu, tungeomba zipungue ili tufanye
kazi kwa ufanisi zaidi,”alisema Salim.
Naye
Meneja Mawasiliano wa Kampuni ya Azam, Hussein Ally, alisema kiwanda
hicho kimeweza kutoa ajira 600 kwa Watanzania, ambapo kati ya hizo
wenye ajira za kudumu ni 380.
Kampuni ya Azam ina jumla ya viwanda 13 ambapo viwanda 11 vipo Dar es Salaam na vingine viwili vipo Pwani.
Kwa
upande wake Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage
alisema kuwa uwekezaji uliofanywa na makampuni ya Bakhresa unasaidia
kuchochea kilimo cha matunda na kutoa fursa ya soko la uhakika kwa
wakulima.
Social Plugin