RAIS mstaafu Jakaya Kikwete, amechukizwa na matumizi mabaya ya picha zake katika mitandao ya kijamii zinazoambatana na kuzushiwa maneno.
Jana kupitia akaunti yake ya mtandao wa twitter, Kikwete alisema aachwe apumzike kwa sababu ameshastaafu na asingependa kuhusishwa na siasa za mtandaoni dhidi ya Serikali.
“Nimestaafu, naomba niachwe nipumzike. Nisingependa kuhusishwa na siasa za mtandaoni dhidi ya Serikali.
“Nasikitishwa sana na matumizi mabaya ya picha zangu mtandaoni hususani watu kunilisha maneno kwa kutaka kutimiza malengo yao ya kisiasa,” aliandika Kikwete katika akaunti hiyo.
Kauli ya Kikwete inakuja ikiwa ni siku chache baada ya kutamka maneno yaliyoibua mijadala katika mitandao ya kijamii na kutafsiriwa tofauti kuwa alikosoa mwenendo wa utawala wa Rais Dk. John Magufuli.
Oktoba 24, mwaka huu akizungumza katika sherehe za maadhimisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kikwete ambaye pia ni Mkuu wa chuo hicho, alisema: “Unapokuwa mpya watu wanataka mambo mapya pia, lakini yawe mapya ya maendeleo na si (mapya) ya kuharibu kule tulikotoka.”
Kikwete alitoa kauli hiyo wakati anazungumzia wadhifa wake mpya wa ukuu wa chuo hicho, lakini baadhi ya watu wakaitafsiri kuwa ilikuwa ni mbinu ya kumkosoa Rais Magufuli.
Hata hivyo, Kikwete, anakanusha tafsiri hiyo kwa kusema kuwa hajakosoa mabadiliko hayo ya Serikali ya Rais Magufuli kwa kuandika katika akaunti hiyo kuwa: “Namuunga mkono Rais na Serikali yake.”
Katika historia yake ya siasa hususani wakati akiwa rais na baada ya kustaafu, Kikwete, amekuwa si mtu wa kupenda kujibu tuhuma mbalimbali zinazotolewa dhidi yake au Serikali yake aliyoiongoza kwa kipindi cha miaka 10 (kuanzia mwaka 2005 hadi 2015).
Na JONAS MUSHI -MTANZANIA DAR ES SALAAM
Social Plugin