Timu za soka za Simba na Yanga za Jijini Dar es Salaam zimezuiwa kutumia Uwanja wa Taifa kwa muda usiojulikana kutoka na mashabiki wao kusababisha uharibifu wa miumbombimu ya Uwanja wa Taifa yakiwemo mageti ya kuingilia Uwanjani na kung’oa viti kwa upande wa mashabiki wa Simba.
Uamuzi huo umetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye alipokuwa akikagua na kutembelea maeneo yalioathirika na uharibifu uliofanywa na mashabiki wa Simba na Yanga katika mechi iliyochezwa Octoba Mosi 2016 katika Uwanja wa Taifa.
“Hii si mara ya kwanza kwa mashabiki kuvunja mageti na kung’oa viti na sisi kama Serikali tumeamua kuzuia vilabu hivi vya Simba na Yanga kutotumia Uwanja wa Taifa mpaka tuitavyoamua vinginevyo hapo baadae” Alisistiza Mhe. Nnauye.
Mhe. Nape Nnauye ameongeza kuwa wameendaa mfumo wa kutumia kamera Uwanjani ili kubaini makosa yatakayokuwa yanafanyika ili kuzuia vitendo vya kihualifu na uharibifu katika Viwanja vya michezo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo Bw. Alex Nkenyenge amesema kuwa wamesikitishwa sana na uharibifu ulitokea katika mechi ya Simba na Yanga na kusababisha uharibifu wa viti na mageti ya kuingilia Uwanjani.
Ameongeza kuwa kwa tathimini iliyofanyika mageti manne yameng’olewa na mashabiki kwa upande wa Simba na Yanga na pia kwa upande wa ndani jumla ya viti 1781 vimeng’olewa katika upande wa mashabiki wa Simba.
“Mara nyingi tumekubaliana kutunza Uwanja huu kwa ajili ya matumizi ya watanzania wote na kama wasimamizi tunasikitika kwa kitendo hiki kilichotokea na tujue kuwa ni kodi za wananchi ndio zilitumika kujenga Uwanja huu na pia ndizo zitazotumika kukarabati Uwanja tuwe na tabia ya kupenda na kutunza vya kwetu.
Klabu za Simba na Yanga zimekuwa na ushindani mkubwa katika soka la Tanzania na kumekuwa kukitokea mambo mbalimbali pale timu hizo zinapokutana ikiwemo uharibifu wa miundombinu katika Viwanja na vurugu kwa mashabiki pale mmoja wao anapofungwa.
Wakati huo kuna taarifa inasambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu Simba Sports Club kutoa taarifa ifuatayo kwa umma
SIMBA SPORTS CLUB
DAR ES SALAAM
2-10-2016
TAARIFA KWA UMMA
Kwa masikitiko makubwa klabu ya Simba imesikitishwa sana na vitendo vilivyofanywa na baadhi ya washabiki wetu,cha kuvunja sehemu ya viti vya Uwanja wa Taifa.kitendo kilichotokea jana kwenye mchezo wetu wa Ligi kuu dhidi ya Timu ya Yanga.
Tungependa kuomba radhi kwa kadhia hii na klabu imekubali kulipia gharama za uharibifu huu.
Klabu itazungumza na wamiliki wa Uwanja huu kuona inalipaje gharama hizo.
Ni mategemeo yeti kuona jambo hili halitajikoze tena.
Lakini mbali na hayo klabu kesho Jumatatu itawasilisha malalamiko rasmi juu ya uchezeshaji mbovu wa waamuzi wa mchezo wa jana,hususan Mwamuzi wa kati Martin Sanya.
Sisi tunaamini vitendo viovu vilivyofanywa na washabiki wetu vilisababishwa na uamuzi wa hovyo kupita kiasi uliosababishwa na waamuzi hao.
Haieleweki ni kigezo gani mwamuzi huyo alitumia kulikubali goli la 'mpira wa pete'la mshambuliaji wa Yanga Amisi Tambwe na kulikataa goli halali la mshambuliaji wetu Ibrahim Ajibu.
Pia tumeshangazwa na kitendo cha kumpa kadi nyekundu nahodha wetu Jonas Mkude.ilhali kama nahodha alimfata kwenda kumlalamikia kitendo chake cha kukubali goli la 'hovyo 'la Tambwe.
Sote tumeona Sanya alijikwaa wakati anarudi nyuma na kuanguka,kisha kuanguka na kutoa kadi nyekundu kwa Mkude.
Kimsingi huyu mwamuzi ana historia ovu ya kuwabeba Yanga.
Hakuna asiyesahau msimu uliopita kwenye kombe la Shirikisho,Yanga walipocheza na Coastal Union kule Mkwakwani Tanga.nini kilitokea!
Tunajua safari hii Tff na bodi ya Ligi zitatoa adhabu kali kwa waamuzi hawa ili iwe fundisho kwa maamuzi ya hovyo ya aina hii.
Pia klabu italalamika kitendo cha vyumba vyetu vya kubadilishia nguo(dressing room)kupuliziwa dawa zilizokuwa na nia ya kuwaathiri wachezaji wetu kabla ya mechi kuanza.
Tutaziomba mamlaka zifanye uchunguzi wa kina kubaini kitendo hiki kisicho cha kiungwana kinachosadikiwa kufanywa na wapinzani wetu.
Tunajua dhamira yao ni kuwafanya wachezaji wetu wachoke,lakini timu yetu ya Matabibu ilichukua hatua sahihi za kuwafanya wachezaji wetu waweze kumaliza dakika Tisini za mchezo kwa uwezo na weledi mkubwa.
Na mwisho klabu itoe malalamiko yake kwa Waziri wa mambo ya nchi,Mh Mwigulu Nchemba.
Waziri huyu bila shaka amesahau majukumu yake yake ya kazi na kugeuka kiongozi wa klabu ya Yanga.
Tunajua ni haki yake kuwa na mapenzi kwa klabu aliyoichagua.lakini vitendo vyake anavyovifanya vinaacha maswali mengi kuliko majibu.ukizingatia nafasi yake kama Waziri mwenye dhamana ya kuongoza Wizara nyeti.
Itakumbukwa majuzi waziri huyu alifanya ziara Mkoani Morogoro kuzungumza na vikosi anavyoviongoza.
Na inajulikana pia Refarii wa mchezo wa jana Martin Sanya ni mwajiriwa wa Jeshi la Magereza mkoani Morogoro
Sote tulishuhudia Jana Mwigulu alishangilia goli la hovyo la mwajiriwa wake Sanya.
Pia waziri huyu alitoa kauli tata kuwa angetamani siku moja klabu inayoshangilia wapinzani wa Yanga wakipigwa mabomu ya machozi na Askari wa jeshi la Polisi.
Kauli hii aliitoa wakati wa sherehe za kukabidhi zawadi kwa timu zilizoshinda msimu uliopita zilizoandaliwa na wadhamini wa ligi.kampuni ya Vodacom.
Tunajiuliza yale mabomu ya jana pale Uwanja wa Taifa ndio utekelezaji wa maagizo ya boss Mwigulu?
Lakini pia matumizi ya rasilimali za umma yakiwemo magari ya serikali ktk shughuli za mara kwa mara za klabu ya Yanga napo kunaacha maswali mengi mno.
Wanasimba wanauliza kila Waziri anayeshabikia Simba akiwepo Waziri Mkuu akifanya vitendo hivi kutakuwa na utawala gani serikalini?
Imani yetu viongozi wakuu wa nchi watamuonya mh Mwigulu,vingenevyo atatengeneza chuki baina ya washabiki wa Simba dhidi ya serikali yao.
Mwigulu atambue klabu ya Simba ina mamilioni ya washabiki kama ilivyo klabu yake anayoishabikia.
Hatutarajii kuona 'mahaba'yake yasio na staha yanachochea jambo ovu kwa wanasimba na serikali yao wanayoiamini na kuipenda sana.
IMETOLEWA NA
KLABU YA SIMBA
SIMBA NGUVU MOJA
Social Plugin