Bodi
ya wadhamini ya Chama cha Wananchi (CUF), imegawanyika vipande viwili
kutokana na mgogoro wa uongozi unaoendelea ndani ya chama hicho.
Kugawanyika
kwa bodi hiyo kumekuja siku moja baada ya Mwenyekiti wake, Abdallah
Katau kutangaza kutomtambua Profesa Lipumba, huku baadhi ya wajumbe
wakipinga tamko hilo wakiliita ni batili kwa mujibu wa katiba ya CUF.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kwa niaba ya wajumbe
wenzake, mjumbe wa bodi ya chama hicho, Peter Malebo, alisema hawatambui
tamko lililotolewa na mwenyekiti wao kwani bodi hiyo inajiandaa
kuwakutanisha mwenyeki wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu
Mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad ili kuweza kutafuta suluhu ya
mgogoro huo.
Alisema
kutokana na hali hiyo, watakaa na wajumbe wenzao na kujadili suala hilo
kabla ya kuwaita viongozi hao ikiwa ni pamoja na kujadili ushauri wa
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi.
“Tutakaa
na wajumbe wenzetu ili tuweze kujadiliana mgogoro wa viongozi wetu
pamoja na kupitia maazimio ya Msajili wa Vyama Vya Siasa ili tuweze
kupata hoja ya kuwahoji kwenye kikao hicho.
“Lengo
letu ni kuhakikisha kuwa chama chetu kinarudi kwenye hadhi yake kama
ilivyokua awali kuliko hivi sasa ambapo kimegubikwa na mgogoro wa
uongozi wa kitaifa,” alisema Malebo.
Alisema
ikiwa watashindwa kupata mwafaka wataitisha Mkutano Mkuu wa dharura
ili waweze kuwaeleza wajumbe wa mkutano huo hali ya chama na hatua za
kuchukua.
“Kama
mwafaka hautapatikana katika kikao hicho, tutalazimika kuitisha Mkutano
Mkuu Maalumu ambao pamoja na mambo mengine, tutawaeleza mgogoro wa
viongozi wetu ili wajumbe waweze kutoa uamuzi,” alisema.
Alisema Bodi ya Wadhamini wa CUF inaundwa na wajumbe wanane ambapo kutoka upande wa bara ni watano na Zanzibar watatu.
Aliwataja
wajumbe hao kuwa ni pamoja na Abdalah Katau, Peter Malebo, Ally
Mbarouk, Amin Mrisha, Zacharia Kwangu, Yohana Mbelwa na Dk. Juma Muchi.
Alisema
mpaka sasa bodi hiyo imegawanyika ambapo wajumbe kutoka Zanzibar
wanamwunga mkono Maalim Seif huku wale wa bara wakimwunga mkono Profesa
Lipumba hali inayozidi kupandisha joto ndani ya chama hicho.
“Kinachotutafuna
ndani ya CUF ni ubaguzi unaoonyeshwa waziwazi kutoka kwa viongozi wa
Zanzibar jambo ambalo limechangia kila mtu kuwa upande wake, lakini
tutaitana na kujadiliana suala hili ili tuweze kupata mwafaka,” alisema.
Alisema
bodi hiyo inafanya kazi ndani ya kipindi cha miaka mitano ambapo
iliteuliwa mwaka 2011 na itamaliza muda wake, Desemba mwaka huu.
Atoa onyo Chadema
Katika
hatua nyingine, Malebo aliwataka viongozi wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) kutoingilia mgogoro huo kwa madai hauwahusu.
Alisema,
kitendo cha Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kujitokeza hadharani
na kudai hamtambui Profesa Lipumba inaonyesha wazi kuwa ameshiriki
kuongeza mgogoro ndani ya chama hicho.
“Mbowe
haumhusu mgogoro wa viongozi wa CUF, huu ni mgogoro wa ndani ya chama,
tunamshangaa kujitokeza hadharani na kudai hamtambui Lipumba, yeye ni
nani ndani ya chama?, tunamuonya asirudie,” alisema.
Alisema,
chama hicho kimejipanga kupambana na watu wanaoingilia mgogoro wao
wakati si wanachama wa chama hicho, jambo ambalo limechangia kuendelea
kuchochea vurugu hizo.
Social Plugin