MKUU wa Mkoa wa Singida, Mathew Mtigumwe ameagiza uchunguzi wa kina ufanyike mara moja kutokana na utata uliogubika kifo cha mjamzito anayedaiwa kufufuka akiwa chumba cha kuhifadhia maiti alikopelekwa baada ya kuthibitika amekufa wakati akijifungua.
Mjamzito huyo, Rahel Erasto (28) mkazi wa Minga mjini hapa alipelekwa hospitali ya mkoa wa Singida, Septemba 29, mwaka huu, kwa ajili ya kujifungua na Septemba 30, mwaka huu alasiri, alijifungua kwa njia ya upasuaji baada ya kushindikana kujifungua kwa kawaida.
Hata hivyo, inadaiwa baada ya mama huyo kujifungua mtoto wa kiume akiwa mzima wa afya njema, hali yake ilizorota na hatimaye kusababisha kifo chake na baada ya kuthibitika kuwa amefariki mwili wake ulipelekwa chumba cha kuhifadhia maiti.
Katika tukio la aina yake, inadaiwa kuwa askari mgambo Emmanuel Daghau (42) ambaye alikuwa doria usiku huo, alisikia mtu akipiga chafya na alipochungulia dirishani alimwona mama huyo akipepesa macho, ndipo alipotoa taarifa kwa uongozi wa hospitali kuhusu tukio hilo.
Baada ya kutoa taarifa alichukuliwa kutoka mochwari na kupelekwa chumba cha upasuaji kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi kisha kurudishwa wodini ambako hata hivyo uchunguzi ulibaini amekufa.
Kutokana na utata wa kifo hicho, mkuu huyo wa mkoa aliagiza wataalamu wa afya na vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa kina na kumpa mrejesho mapema.
Wakati polisi wanasema wanamshikilia mgambo huyo kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kwa ndugu wa marehemu juu ya kifo hicho, ndugu wa marehemu akiwemo wifi yake Maria Mpaki na shemeji yake John Mwanduu wanadai ndugu yao amekufa kutokana na uzembe uliokithiri wa watumishi wa Hospitali ya Mkoa wa Singida.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Ramadhan Kabala alisema jopo la wataalamu wa afya, akiwemo Dk Ahmed Makata kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani, pamoja na wapelelezi kadhaa wanaendelea na uchunguzi kuhusu kifo hicho.
- Imeandikwa na Abby Nkungu- Habari leo Singida
Social Plugin