Mama mjazito akihangaika na hatimaye kupoteza maisha kutokana na mimba za utotoni..Video ipo hapo chini baada ya maelezo mafupi |
Bongo Movie Shinyanga kwa kushirikiana na Shirika la Agape Aids Control Programme la mkoani Shinyanga wametualika kutazama filamu fupi “KIFO” inayoelezea madhara ya ndoa na mimba za utotoni ambazo zimeonekana kushamiri katika jamii.
Akizungumza na Malunde1 blog,Mwenyekiti wa Bongo Movie Shinyanga Ibrahim Juma Songoro amesema wameamua kushirikiana na shirika la AGAPE ambalo limekuwa mstari wa mbele kupiga vita mimba na ndoa za utotoni ili kuielimisha jamii kuhusu madhara ya ndoa na mimba za utotoni.
“Madhara ya mimba na ndoa za utotoni ni Kifo,ndiyo maana filamu hii tumeipa jina la kifo kwani watoto wengi wanaopata ujauzito au mimba katika umri mdogo wamekuwa wakipoteza maisha wakati wa kujifungua na pia watoto wengi wamekuwa wakifariki pindi akina mama hao wanapojifungua”,amesema Songoro.
“Tunaamini kabisa kuwa kupitia filamu hii jamii itabadili mienendo yao na kuachana na vitendo hivi viovu sambamba na kuachana na imani potovu kuwa akina mama wajawazito wanakufa kutokana na imani za kishirikina jamii ikiamini kuwa wamelogwa”,ameongeza Songoro.
Naye kaimu mkurugenzi wa Shirika la AGAPE Samwel Sasabo Magina amesema wameamua kushirikiana na Bongo Movie Shinyanga kutokana na kwamba wasanii hao wa uigizaji wana nguvu kubwa katika kuvuta watu wengi lakini pia sanaa inatumia muda mfupi kufikisha ujumbe kwa jamii.
“Unapotumia maigizo unavuta watu wengi na wanakuja kujifunza na kutokana na kwamba wenzetu Bongo Movie Shinyanga wana nguvu kubwa hivyo tunaamini kabisa kuwa tutaweza kuielimisha jamii kuhusu athari za mimba na ndoa za utotoni kupitia sanaa ya uigizaji”,ameeleza Magina.
“Sasa tunatekeleza mradi wa kuzuia mimba na ndoa utotoni 2016/2018 katika wilaya ya Shinyanga na Kishapu,mbinu kubwa tunayotumia sasa kuwafikia wananchi wengi ni njia ya sinema ndiyo maana tumetengeza filamu hii inaitwa KIFO lakini pia tunatumia njia zingine ikiwemo vipindi vya radio,Makala za TV,mabango,vipeperushi vya utoaji elimu na kadhalika”,ameongeza Magina.
Takwimu zinaonesha kuwa mkoa wa Shinyanga ukiongoza kitaifa kwa mimba na ndoa za utotoni kwa asilimia 59 ambapo wilaya inayoongoza ni Kishapu ikifuatiwa na Shinyanga vijijini huku mikoa mingine inayotajwa kuwa vinara wa vitendo hivyo kuwa ni mkoa wa Tabora 58%, Mara 55%, Dodoma 51% na Lindi 40%.
Tazama video hii fupi ya kusisimua hapa chini
Kwa mambo mbalimbali ya sanaa ya uigizaji ,wasiliana na mwenyekiti wa Bongo Movie Shinyanga Ibrahim Songoro kwa /whatsapp/simu namba 0767831036